Afungwa miaka 10 kwa jaribio la kumuua mkewe kwa wivu wa mapenzi

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Daniel Mwangaya (35) kutumikia kifungo cha miaka 10 jela baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kumuua mkewe kwa kumcharanga mapanga.

Mwangaya, maarufu kama Ibrahim Maiko Mangaya, ambaye ni mlinzi na mkazi wa Bunju, anadaiwa kujaribu kumuua mke wake, Pili Musa kwa kumcharanga mapanga mwili mzima kutokana na wivu wa mapenzi.

Baadaye, alidaiwa kumtumbukiza katika shimo ambalo halijaezekwa kwa juu, lenye urefu wa futi 10 na kuanza kumpiga mawe sehemu mbalimbali za mwili wake akiwa ndani ya shimo hilo.

Hukumu hiyo imetolewa jana, Julai 11, 2025, na Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya, aliyeongezewa mamlaka ya ziada kusikiliza kesi ya mauaji, baada ya mshtakiwa kukiri shtaka lake.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Erick Kamala, alimkumbusha mshtakiwa shtaka lake kwa kumsomea upya hati ya mashtaka.

Mshtakiwa, baada ya kukumbushwa shtaka hilo, alikiri kutenda kosa hilo, ndipo upande wa mashtaka ulipomsomea maelezo yake na kisha mahakama kumtia hatiani.

Akimsomea shtaka lake, Wakili Kamala anadai kuwa kosa hilo limetendwa kinyume na Kifungu 211(a) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2025.

Kamala anadai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na shtaka la kujaribu kuua, kinyume na kifungu hicho.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 26, 2024, eneo la Bunju A, Gosheni lililopo Wilaya ya Kinondoni, na anadaiwa kujaribu kumuua mkewe, Pili Musa kwa kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.

Akisoma maelezo yake, Wakili Kamala alidai siku hiyo ya tukio, mke wa mshtakiwa alienda nyumbani kwao na watoto wake kusalimia na alivyorejea jioni alikuta mume wake ameshapika chakula (ugali na dagaa) wakala kwa pamoja.

Baada ya kula, mke wake alioga na alimwambia kuna kitu amesahau nyumbani kwao, hivyo anaomba amruhusu kwenda kuchukua.

Mume alimruhusu kwenda, lakini naye alimfuata nyuma bila mke kujua hadi karibu na barabara na alianza kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake, huku akimtuhumu kuwa ana mpenzi.

“Baada ya kumkata mapanga, Mangaya alimburuza mkewe kutoka barabarani hadi kichakani, kisha kumtumbukiza katika shimo lililosakafiwa pembeni huku juu likiwa wazi, na kisha kumuacha hapo,” alidai wakili wakati akisoma maelezo hayo.

Siku iliyofuata, yaani Jumamosi asubuhi, mshtakiwa alienda katika shimo akiwa na ngazi.

Alipofika katika shimo hilo alimhoji mke wake kuwa kumbe bado hajafa, na hivyo alichukua ile ngazi na kuiweka ndani ya shimo na kisha kuanza kumpiga na baadaye kumchoma kisu tumboni, kisha kuondoka.

Mshtakiwa huyo alivyotoka hapo, alienda kwa Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa eneo hilo na kudai kuwa mke wake amepotea.

Usiku alirudi katika shimo hilo na kumpiga mawe na kisha kuondoka.

Upande wa mashtaka uliendelea kudai kuwa siku ya Jumapili, mshtakiwa alienda tena kwa Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa na kudai kuwa bado hajampata mkewe, na baada ya nusu saa alirudi kwa mwenyekiti na kumueleza kuwa kuna watu wamemkuta kwenye shimo na kumuokoa.

ilielezwa mkewe alikaa katika shimo hilo kwa siku tatu hadi alivyokuja kuokolewa na mchungaji wa ng’ombe aliyekuwa anachunga pembezoni mwa eneo hilo.

Ilidaiwa kuwa Pili alisikia sauti za mifugo zikipita karibu na shimo hilo, ndipo alipoita kwa sauti akiomba msaada.

Mchungaji huyo alipofika na kuchungulia ndani ya shimo hilo, alimuona mtu anayemfahamu na kumuita kwa jina lake, na alipoitika alienda kuomba msaada kwa watu na majirani wa eneo hilo.

Pili aliokolewa na kupelekwa hospitalini, na baadaye mume wake alikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi.

Mshtakiwa, baada ya kutiwa hatiani, aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni wivu wa mapenzi ndio ulimpelekea kufanya hivyo.

“Mheshimiwa, naomba mahakama yako inipunguzie adhabu kwa sababu ni wivu tu ndio umenipelekea kufanya hivyo,” alidai na kuongeza:

“Mimi ni kijana mdogo na nguvu kazi ya Taifa, na ni kosa langu la kwanza. Nina mke na watoto wawili ambao ni wadogo, mmoja ana umri wa miaka miwili, na wote wananitegemea. Hivyo naomba mahakama yako inipunguzie adhabu,” alidai mshtakiwa.

Kwa upande wa mashtaka, ulidai hauna kumbukumbu za makosa ya jinai dhidi ya mshtakiwa huyo, lakini uliomba apewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine, kwani kitendo alichofanya ni cha kinyama na hakikubaliki.

Akitoa adhabu, Hakimu Mbuya alisema baada ya kupitia shufaa zilizotolewa na mshtakiwa pamoja na hoja za upande wa mashtaka, na kwa kuzingatia kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, mahakama inamhukumu kutumikia kifungo cha miaka 10 gerezani ili iwe fundisho.

Related Posts