Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, imemuachia huru Elisha Eliah, aliyekuwa amehukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kosa la ulawiti.
Uamuzi huo umetolewa Julai 8, 2025 na Jaji John Nkwambi kutokana na rufaa aliyoikata Elisha akipinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya chini iliyomtia hatiani na kumhukumu adhabu hiyo.
Jaji Nkwabi amefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na sababu zake za rufaa, ambazo pia ziliungwa mkono na Serikali kuwa hapakuwa na ushahidi wa kumtia hatiani kwa kosa hilo, kutokana na ushahidi wa upande wa mashtaka kuacha mapengo.
Jaji John Nkwabi ametoa hukumu hiyo na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama hiyo.
Amesema kuwa anakubali msimamo unaoshikiliwa na pande zote mbili za rufaa, ikiwemo mjibu rufaa (Jamhuri) ambao uliunga mkono rufaa hiyo kwani kesi haikuthibitishwa kama inavyoelekezwa kisheria.
Jaji Nkwabi amesema amepitia kumbukumbu hasa ushahidi wa shahidi wa kwanza, shahidi wa tatu na mwathirika wa tukio hilo na kuwa ushahidi wao siyo wa kuaminika kama alivyoeleza Wakili Maricha.
Amesema kama alivyoeleza wakili huyo, baba wa mwathirika wa tukio hilo ambaye alikuwa chumbani (eneo la tukio) hakutoa ushahidi wake mahakamani.
Amesema kutokutoa ushahidi huo, kunakinzana na uamuzi wa Boniface Kundakira Tarimo dhidi ya Jamhuri, Rufaa ya Jinai namba 350/2008, ambapo ilisisitizwa kuwa:
“Hivyo sasa imeamuliwa kwamba, pale ambapo shahidi ambaye yuko katika nafasi nzuri zaidi ya kueleza baadhi ya viungo vinavyokosekana katika kesi ya chama, hataitwa bila sababu za kutosha kuonyeshwa na upande, hitilafu mbaya inaweza kutolewa dhidi ya upande huo, hata kama maoni hayo yanaruhusiwa.”
Jaji amesema anakubaliana na msimamo unaoshikiliwa na pande zote mbili kwenye rufaa hiyo, kwamba ushahidi wa mashtaka haukuthibitishwa kwa kiwango kinachohitajika.
“Rufaa inaruhusiwa, hukumu ya kifungo cha maisha iliyotolewa na mahakama kwa mrufani ikitenguliwa na mahakama inaamuru mrufani aachiwe huru kutoka gerezani isipokuwa awekwe humo kwa sababu nyingine yoyote halali,” amesema.
Katika kesi ya msingi, mrufani huyo alishtakiwa kwa kosa la ulawiti kinyume na kifungu cha 154 (1) (a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu, kosa alilodaiwa kutenda Mei 10, 2024 mkoani Kigoma.
Mahakama ya Wilaya ya Kigoma baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka na ushahidi wa mrufani huyo ambaye alijitetea mwenyewe, ilimtia hatiani na kumhukumu adhabu hiyo.
Hata hivyo Elisha hakuridhika na hukumu hiyo, kutiwa hatiani, hivyo alitaka rufaa Mahakama Kuu akiwasilisha sababu mbili.
Sababu hizo ni Hakimu alikosea kisheria kumtia hatiani na kumhukumu kwa kuzingatia ushahidi dhaifu uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka ambao haukuthibitisha kesi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa vya ushahidi katika kesi za jinai.
Mrufani huyo ambaye mahakamani hapo alijiwakilisha mwenyewe bila uwakilishi wa wakili, aliiomba mahakama ifute hukumu na adhabu iliyotolewa dhidi yake itenguliwe na aachiliwe huru.
Wakili wa Jamhuri, Fortunatus Maricha aliunga mkono rufaa hiyo kwa misingi kwamba shtaka hilo halikuthibitishwa bila shaka yoyote pamoja na baadhi ya mashahidi muhimu hawakutoa ushahidi.
Amesema kuwa ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo na mama yake (aliyekuwa shahidi wa tatu) siyo mashahidi wa kutegemewa.
Wakili Maricha aliieleza mahakama kuwa mwathirika wa tukio hilo alidai akiwa amelala na ndugu wengine na baba yake, ndipo mrufani akamlawiti ila baba huyo hakutoa ushahidi mahakamani hapo.
Wakili huyo aliielekeza mahakama katika rufaa ya jinai namba 739/2025 kati ya Begaya Paulo dhidi ya Jamhuri katika ukusara wa 217 na kuhitimisha kuwa mashahidi hao wawili hawakuwa mashahidi wa kuaminiwa.
Alieleza kuwa kwa vile baba wa mwathirika wa tukio hilo alikuwepo na alihusika katika kumpeleka mshitakiwa polisi, alipaswa kutoa ushahidi kwani kutokutoa ushahidi kunadhoofisha kesi ya mashtaka.