Dar es Salaam. Ndani ya wiki moja, maeneo ya biashara katika masoko yaliyopo mikoa ya Iringa, Tabora na Singida yameteketea kwa moto, ulioathiri uchumi wa wafanyabiashara na Taifa kwa ujumla.
Wakati soko maarufu la Mashine Tatu lililopo Manispaa ya Iringa limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo, Julai 12, 2025, tukio lingine la namna hiyo liliteketeza maduka matano katika eneo la Salmini, Kata ya Chemchem, Manispaa ya Tabora, usiku wa kuamkia Julai 7.
Vilevile, vibanda 13 vilivyomo ndani ya Soko Kuu la Singida, usiku wa kuamkia Jumamosi, Julai 5, 2025, viliteketea kwa moto.
Ofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Meja Hassan Mande, alisema moto uliteketeza fremu tano za maduka, ambako kulikuwa na matoroli, masufuria na dalili za uwepo wa majiko ya kupikia.
Moto katika Soko Kuu la Singida moto ulianza saa nne usiku. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale, alisema sehemu kubwa ya mali za wafanyabiashara ziliokolewa.
Wakati hayo yakitokea mwezi huu, vibanda vya wafanyabiashara zaidi ya 30 wa mbao katika Soko la Mbao Sabasaba, wilayani Ilemela, mkoani Mwanza, viliteketea kwa moto Machi, 2025.
Kaimu Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Elisa Kamugisha, Machi 17, 2025, alilieleza Mwananchi kuwa moto huo ulianza saa saba usiku wa kuamkia siku hiyo.
Kutokana na matukio hayo, Mwananchi leo, Julai 12, imezungumza na wadau mbalimbali, likiwamo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambalo limeeleza kuwa chanzo cha majanga ya moto katika masoko nchini ni pamoja na uzembe wa baadhi ya mama lishe, uunganishwaji holela wa umeme na ujenzi usiozingatia taratibu za kiusalama.

Mkaguzi na Ofisa Habari wa jeshi hilo kutoka Makao Makuu, Inspekta Damian Muheya, amesema uchunguzi unaofanywa baada ya matukio ya moto umebaini kuwa biashara zinazochanganyika kwenye masoko, hasa kati ya wauza chakula na wafanyabiashara wengine, zimekuwa chanzo cha majanga hayo.
Baadhi ya mama lishe wamesema wamekuwa wakiacha majiko yakiwaka usiku, hali inayochangia matukio mengi ya moto.
Muheya amesema changamoto nyingine ni uunganishaji wa umeme usiofuata taratibu kwa baadhi ya wafanyabiashara, ambao huongeza vibanda kiholela na kuunganisha nyaya bila kutumia mafundi walioidhinishwa au bila kupitisha mipango yao kwa mamlaka husika. Amesema wapo pia wanaotumia nyaya zisizo na viwango.
Mbali ya hayo, amesema baadhi ya masoko yanajengwa bila kuacha njia za dharura, hali inayowafanya zimamoto kushindwa kuyafikia maeneo ya tukio kwa haraka janga linapotokea.
“Ukiangalia soko lina vibanda kila sehemu, hakuna njia ya dharura. Moto ukianza, kufika pale ni mtihani mkubwa. Ndiyo maana tumekuwa tukishirikiana na mameneja wa masoko kuwaelekeza waondoe vibanda vilivyojengwa kinyume cha taratibu,” amesema.
Amesema kwa mujibu wa sheria, ramani za majengo yote, yakiwamo masoko, lazima zipitishwe na Jeshi la Zimamoto kabla ya ujenzi kuanza.
“Changamoto ni kuwa baadhi ya vibanda huongezwa baada ya sisi kufanya ukaguzi na kuridhika, hapo ndipo hatari inapoanzia kwa sababu sisi hatuhusishwi tena,” amesema.
Kwa upande wake, Suleiman Kova, mshauri katika masuala ya usalama na majanga, amesema moja ya sababu zinazochangia matukio ya majanga kama moto katika masoko nchini ni ukosefu wa mipango thabiti ya usalama na kutokuwapo kwa usimamizi wa kina kutoka mamlaka husika.
Kova, ambaye ni Kamanda wa zamani wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, amesema masoko mengi, hasa ya wazi na yasiyo rasmi, hayafuati taratibu na miundombinu ya msingi ya usalama inayoweza kusaidia kuzuia au kupunguza madhara ya majanga yanapotokea.
“Kuna masoko ambayo hata ukitembea ndani yake, unakuta watu wanapika, wanachomelea, wanapiga pasi, wanapika supu hadi asubuhi… Mtu anapewa fremu tu, hana mwongozo wowote wa usalama, anaingiza fundi wa umeme anaweka nyaya bila kufuata viwango,” amesema.
Kova amesema mazingira hayo huruhusu moto kutokea kwa urahisi na endapo ajali itatokea, madhara huwa makubwa kwa sababu hakuna maandalizi yoyote ya dharura wala vifaa vya kuzimia moto.
“Moto unapoanza mara nyingi ni kitu kidogo sana, kama kungekuwa na vifaa na watu wenye uelewa, ungeweza kuzimwa mapema. Lakini kwa kuwa hakuna ulinzi wala vifaa, watu wanakimbia, moto unatawala,” amesema.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Gelardine Kikwasi, amesema majanga ya moto katika masoko ni kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuzimia moto na ujenzi usiozingatia viwango vya usalama.

Amesema hata panapowekwa vifaa hivyo, baadhi ya watu wamekuwa wakivichukulia kama mapambo kwa sababu hawana elimu ya matumizi yake.
“Baadhi ya masoko yanajengwa kwa kutumia vifaa vinavyoweza kushika moto kwa haraka, hali inayoongeza tatizo, kwani moto unaweza kuanzia kwa jambo dogo tu, halafu ukaenea haraka kwa sababu vifaa vinavyotumika si vya kudhibiti moto,” amesema.
Mtaalamu wa masuala ya bima, Dk Anselmi Anselmi, amesema licha ya kuwapo sheria mpya ya fedha ya mwaka 2022 inayolazimisha majengo ya umma pamoja na masoko kuwa na bima, changamoto kuu ya utekelezaji wake ni ukosefu wa miongozo inayoweka utaratibu wa wazi wa namna ya kuwalazimisha watu walioko kwenye masoko kukata bima.
“Sheria ipo, lakini bado haijatungiwa kanuni za utekelezaji. Kwa hiyo, hata kama sheria inataka watu walioko kwenye masoko kuwa na bima, utekelezaji wake bado hauwezekani,” amesema.
Amesema pia kuna tatizo la uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa bima, si kwa wafanyabiashara pekee bali hata kwa jamii kwa ujumla.
“Watu wengi hawajui kuwa bima ni sehemu ya ulinzi kama ilivyo kwa walinzi tunaowaweka sokoni au sungusungu mitaani. Moto au ugonjwa ni kama mwizi, yanapokuja ghafla madhara yake ni makubwa,” amesema.
Amesema jamii imekuwa na tabia ya kusubiri matatizo yatokee ndipo waanze kutafuta bima, jambo linalopotosha dhana halisi ya uwepo wa huduma hiyo.
Mchumi Sophia Mussa amesema majanga ya moto katika masoko huathiri moja kwa moja uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Amesema wafanyabiashara hupoteza bidhaa na mitaji, hali inayosababisha kurudi nyuma kiuchumi, hasa kwa wale wanaoendesha biashara zao kwa mkopo, kupotea kwa ajira na kusababisha mzunguko wa fedha kupungua.
Sophia amesema uharibifu wa miundombinu ya soko unaigharimu Serikali fedha nyingi za matengenezo au ujenzi upya, fedha ambazo zingeweza kuelekezwa kwenye huduma nyingine za kijamii kama afya na elimu.
“Ukosefu wa maandalizi ya kukabiliana na majanga kama haya ni hasara kwa Taifa. Muhimu kuweka mikakati ya kinga, si kusubiri hadi tukio litokee,” amesema.
Muheya kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji amesema jeshi hilo linaendesha programu mbalimbali za kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu kinga na tahadhari dhidi ya moto, ikiwamo uwepo wa vifaa vya kuzimia moto masokoni.

Muonekano wa Soko la Mashine Tatu lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa likiwa linaungua usiku wa kuamkia leo Julai 12, 2025.
“Tunashirikiana na mameneja wa masoko kuhakikisha vifaa vya dharura vinapatikana. Pia tumeanzisha mpango wa kuwa na fire volunteers (zimamoto wa kujitolea) kwenye kila soko. Hawa watafundishwa na watakuwa msaada kabla ya gari la zimamoto kufika,” amesema.
Jeshi hilo pia limeanzisha mikakati ya kuhakikisha kila soko linakuwa na fire hydrant (bomba la dharura la maji kwa ajili ya kuzima moto), kutokana na changamoto ya magari ya zimamoto kuishiwa maji na kukosa sehemu ya karibu ya kujaza.
“Unakuta tukifika kwenye tukio gari limeisha maji, lakini hakuna fire hydrant ya karibu. Tunataka kila soko liwe na hiyo miundombinu,” amesema.
Kova, mshauri wa masuala ya usalama na majanga, amesema suluhisho si kuwalaumu wafanyabiashara pekee, bali ni kuwajengea uelewa na kushirikiana na uongozi wa masoko kuhakikisha usalama unazingatiwa.
“Halmashauri hazitakiwi kusubiri hadi majanga yatokee. Lazima ziwe na vikao vya mara kwa mara na viongozi wa masoko na wafanyabiashara. Pia kuwe na ulinzi shirikishi, vijana wawe kwenye zamu, wazunguke, waangalie kama kuna hatari yoyote,” amesema.
Amesema kuna haja ya kuwa na askari maalumu au walinzi waliofunzwa kuhusu usalama wa masoko, pamoja na kuwa na vifaa vya kisasa vya kuzimia moto vinavyopatikana kwa gharama nafuu kupitia mashirikiano na kampuni binafsi au wadau wa maendeleo.
Amesema suala la usalama masokoni halipaswi kuchukuliwa kama jambo la kawaida, bali ni ajenda ya kitaifa inayoathiri maisha ya watu, uchumi na ustawi wa jamii.
“Kama Taifa tunapaswa kuangalia masoko kama maeneo ya kimkakati, kama ilivyo viwanja vya ndege. Huko hatuachi hewa ya gesi iruke hovyo, basi kwa nini kwenye masoko turuhusu fujo na hatari zote hizi?” amehoji.
Amesema hatua madhubuti zinaweza kuchukuliwa ikiwa kila mamlaka ya mtaa, kata na manispaa itawajibika ipasavyo na kuhakikisha kuwa kila soko lina mpango wa usalama, ulinzi shirikishi, vifaa vya dharura na mafunzo kwa wahusika wote.
Profesa Kikwasi ametoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha masoko mapya na ya zamani yanazingatia sheria za ujenzi zinazohusiana na usalama wa moto, ikiwamo kutumia vifaa vinavyochelewesha moto, kuweka nafasi za kupitisha hewa na vifaa vya kuzima moto. Pia elimu itolewe kwa watumiaji wa maeneo hayo. nafasi za kupitisha hewa na vifaa vya kuzima moto. Pia elimu itolewe kwa watumiaji wa maeneo hayo.