WAKATI Azam FC ikimpigia hesabu aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Clatous Chama ikiwa ni pendekezo pia la kocha wa timu hiyo, Florent Ibenge, kikosi hicho kinakabiliwa na ushindani kutoka kwa Zesco United ya Zambia inayomuhitaji.
Nyota huyo aliyezichezea timu mbalimbali zikiwemo Ittihad Alexandria SC ya Misri, Lusaka Dynamos FC ya Zambia, Simba ya Tanzania na RS Berkane ya Morocco, kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Yanga kufikia tamati.
Chama aliyejiunga na Yanga Julai 1, 2024, kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuachana na Simba, inadaiwa ameshindwa pia kuongeza mwingine na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, hivyo yupo huru kutafuta changamoto mpya.
Wakati hayo yakiendelea, chanzo cha ndani kutoka Azam kimelidokezea Mwanaspoti Chama ni miongoni mwa nyota wanaohitajika kwa ajili ya kuongeza nguvu, ingawa dili hilo bado halijakamilika na sasa Zesco United imeingilia kati ikimhitaji pia.
“Baada ya Azam kuona kuna nafasi ya kumpata ilianza mazungumzo haraka na menejimenti yake, wanaamini ni mchezaji mzoefu na mkubwa atakayewasaidia sana hasa katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa kwa msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilidokeza Mwanaspoti, Chama anaonekana ni mtu sahihi anayeweza kuvaa viatu vya kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambaye bado hatima yake ya kubakia au kuondoka kikosini humo haijafahamika hadi sasa.
“Viongozi wamechoka na suala la Feisal na kinachofanyika kwa sasa wao wapo tayari mkataba wake wa mwaka mmoja uishe ili aondoke bure kuliko kuendelea kumzungumzia yeye kila siku, ndio maana wanamuangalia Chama zaidi,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, wakati Azam ikipiga hesabu hizo, Zesco United ambayo mchezaji huyo aliwahi kuitumikia mwaka 2013 hadi 2017, akitokea Nchanga Rangers FC ya Zambia, inadaiwa pia inamhitaji kumrejesha na mazungumzo yanaendelea vizuri.
Msimu uliomalizika 2024-2025, Chama amehusika katika mabao tisa ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga sita na kuasisti matatu, huku akiwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichotwaa mataji matano msimu huo ambayo ni Kombe la Toyota, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).