MABOSI wa Fountain Gate wamefanikisha kumnunua moja kwa moja mshambuliaji Edgar William aliyekuwa akiitumikia timu hiyo kwa mkopo kutoka Singida Black Stars.
Edgar aliitumikia Fountain Gate kwa mkataba wa mwaka mmoja ambao ulikuwa ni wa mkopo na kuifungia timu hiyo mabao sita.
Chanzo cha kuaminika kutoka Fountain Gate kililiambia Mwanaspoti, kutokana na kuvutiwa na uwezo wa mchezaji huyo uongozi umeamua kumalizana na Singida Black Stars ili kuendelea kupata huduma ya mchezaji huyo msimu ujao.
“Mkopo wake ulikuwa wa mwaka mmoja na umemalizika mwisho wa msimu, lakini baada ya benchi la ufundi kuonyesha nia ya kutaka kuendelea naye tumefanya mazungumzo na Singida na kufikia makubaliano ya kumsajili moja kwa moja, hivyo ataendelea kuwa sisi msimu ujao,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Tumefanya makosa msimu ulioisha tukibaki kwa kucheza mechi za mtoano ‘Playoff’ mipango yetu sasa ni kufanya usajili mzuri ambao utatuweka kwenye nafasi nzuri ya ushindani na hili linaanza kwa kuhakikisha tunazungumza na wachezaji muhimu ambao wamemaliza mikataba yao kabla ya kurudi sokoni kusajili nyota wengine.”
Alisema mikakati ya kusuka kikosi bora cha ushindani imeanza na wanatarajia kufanya uwekezaji mkubwa kwenye usajili ili wasirudie makosa waliyoyafanya msimu huu wakianza vizuri mzunguko wa kwanza na kupoteza uelekea mzunguko wa pili.