Malala Fund yatenga Sh7 bilioni kusaidia wasichana waliokatishwa masomo Tanzania

Dodoma. Shirika la kimataifa la Malala Fund limetenga takriban Sh7.7 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha wasichana waliokatishwa masomo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ujauzito wa mapema, kurejea shuleni na kuendelea na elimu yao.

Lengo la mpango huu ni kuhakikisha wasichana hao wanapata fursa ya pili ya kujifunza, kujijengea maisha bora, na kuchangia maendeleo ya jamii zao.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Malala Fund, Malala Yousafzai ambaye yuko nchini katika ziara iliyolenga kuwatembelea na kuzungumza na baadhi ya wasichana waliopata fursa ya kurejea shule baada ya kukatizwa masomo yao.


Malala ambaye alinusurika kifo mwaka 2012 baada ya kupigwa risasi na kundi la Tehrik-e-Taliban Pakistan (TTP) maarufu kama Taliban wa Pakistan kwa sababu ya kutetea haki ya wasichana kupata elimu, amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma akizungumza na wasichana waliorejea shule.

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, kupitia shirika analoliongoza la Malala Fund ameanza kuwekeza nchini Tanzania tangu mwaka 2022, kwa lengo la kuimarisha usawa wa kijinsia katika elimu.

Miongoni mwa vipaumbele vya shirika hilo nchini ni kutetea na kuhimiza utekelezaji wa sera za kupunguza ndoa za utotoni, pamoja na aina nyingine za ukatili wa kijinsia dhidi ya wasichana.

Katika muktadha wa Tanzania, mbali na kutoa ufadhili wa kifedha, Malala Fund pia imewekeza katika kuhakikisha utekelezaji wa sera zinazowawezesha wasichana waliopata mimba wakiwa shuleni kurejea na kuendelea na masomo yao.

Vilevile, shirika hilo linatoa msaada mahsusi kwa wasichana kutoka jamii za pembezoni na vijijini, ili kuwapa fursa ya kupata elimu yenye ubora na inayojali usalama wao.

Malala ambaye shambulio la risasi alilopitia limeongeza hadhi yake kama shujaa wa elimu ya wasichana duniani, katika ziara yake wilayani Kongwa ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha kuwawekea vikwazo wasichana waliopata ujauzito kurejea shuleni.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za kipaumbele kwa Malala Fund, shirika analoliongoza, sambamba na Afghanistan, Brazil, Ethiopia, Nigeria na Pakistan.

Malala alikulia katika eneo la Bonde la Swat nchini Pakistan, ambako kundi la Taliban liliweka marufuku kwa wasichana kuhudhuria shule.

Licha ya mazingira hayo ya vitisho na ukandamizaji, hakuacha kusimamia imani yake kwamba kila msichana anastahili haki sawa ya kupata elimu.

 “Tumeona Tanzania mabinti wengi wanakatisha masomo kwa sababu ya changamoto mbalimbali, ikiwemo umbali mrefu kwenda shuleni. Malengo yetu ni kushirikiana na taasisi kama Msichana Initiative kutatua changamoto hizi,” alisema Malala.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Simon Mayeka, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaondoa watoto shuleni na kuwapeleka kufanya kazi za ndani, akibainisha kuwa hali hiyo inaathiri maendeleo ya elimu na kuongeza mzigo kwa familia na jamii.


“Mtoto akifanya kazi za ndani ni kwa miaka michache tu, baada ya hapo anarudi nyumbani akiwa hana msaada wowote zaidi ya kuwa mzigo. Mbaya zaidi, huko anakumbana na ukatili, magonjwa na mimba zisizotarajiwa,” amesema Mayeka.

Mkurugenzi wa Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, ambaye pia ni mdau wa Malala Fund, amesema kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kuwarejesha shule wasichana takribani 600 waliokuwa wameacha masomo kutokana na sababu mbalimbali kama vile mimba, ndoa za utotoni, umbali wa shule na ajira za ndani.

 “Wazazi hupeleka watoto mijini kufanya kazi za ndani kwa matumaini ya kusaidia familia. Lakini kwa waliorejea shule bado kuna changamoto kubwa ya mazingira rafiki, hasa kwa wale wenye watoto,” alisema Gyumi.

Kwa upande wake, Esther Michael, mmoja wa walionufaika na mradi huo, amesema kuwa fursa ya kurejea shule imekuwa kama mwanga mpya katika maisha yake na ameahidi kuendelea kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zake.

Malala alianzisha shirika la Malala Fund kwa ushirikiano na baba yake, Ziauddin Yousafzai, kwa lengo la kutetea haki ya wasichana kupata elimu bora, salama, na bila malipo kwa kipindi cha angalau miaka 12.

Malala Fund hutoa msaada kwa programu za kielimu, inatetea mabadiliko ya sera zinazoboresha mazingira ya elimu kwa wasichana, na kukuza sauti zao ili waweze kuwa na uwezo wa kuchagua mustakabali wao kwa uhuru na uelewa.

Malala alizaliwa tarehe Julai 12, 1997 katika mji wa Mingora, ulioko katika Bonde la Swat, nchini Pakistan.

Related Posts