Mastaa Simba wampitisha Tshabalala | Mwanaspoti

MASHABIKI wa Simba huenda wameshtushwa na taarifa za kuondoka kwa beki wa kushoto, Valentin Nouma, aliyeaga mapema tangu juzi kuonyesha hatakuwa sehemu ya kikosi hicho kwa msimu ujao wa mashindano wa 2025-2026, huku nahodha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akiwa hajapewa mkataba.

Tshabalala ni mmoja ya wachezaji waandamizi wa klabu hiyo ambao bado hajapewa mkataba mpya hadi sasa, huku akitajwa kunyemelewa na klabu nyingine, lakini kuna msimamo uliotolewa na malejendi wa klabu hiyo ya Msimbazi kuhusu nahodha huyo aliyepo Simba tangu 2014.

Malejendi hao wa Simba, wamesisitiza kwamba nahodha wa kikosi hicho, Mohamed Tshabalala bado ana nafasi kubwa ya kung’ara Msimbazi na miguu yake inamsemea.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ amesema Tshabalala atacheza sana Simba kutokana na kuipa thamani nafasi anayoipata lakini hilo lisiwafanye Simba kushindwa kutafuta mbadala sahihi.

“Tshabalala atacheza sana Simba labda waamue kumuacha lakini kujituma kwake na kujiongeza thamani ndio kitu kinachompa nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kujiweka kwenye ushindani ambao wachezaji wengi wanashindwa,”alisema na kuongeza;

“Wanatakiwa kutafuta mchezaji ambaye wanamuandaa endapo kuna shida itatokea azibe nafasi lakini sio kushindana na beki huyo ambaye tayari amejitengenezea namba na uaminifu wa kutosha kutokana na namna anavyotumia nafasi kwa kila kocha anaempa nafasi.”

Batgol alisema Tshabalala amejitofautisha na nyota wengi wa kigeni ambao wakipata nafasi ya kucheza timu kubwa za Simba na Yanga wanaridhika na kuamini kuwa hakuna mchezaji mwingine anaweza kufanya kile wanachokifanya kwa wakati huo na kujikuta wanapotea kwa muda mchache.

Nahodha na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema juhudi binafsi na kuheshimu kazi yake ndio vitu vinavyomtofautisha Tshabalala na nyota wengine.

“Tshabalala ni beki ambaye anamuendelezo wa ubora hii ndio sifa kubwa kwake na imekuwa ikimfanya apenye kwa makocha wengi ni muumini wa kufanya mazoezi na kutumia nafasi anazopewa kwa kufanya kitu sahihi,” alisema na kuongeza;

“Sina maana kwamba wachezaji wengine wanaopita Simba mfano Valentine Nouma ni mbaya hapana ni mzuri lakini alishindwa kumshawishi kocha na amekutana na mchezaji ambaye tayari anauzoefu mkubwa na tayaria meshafanya mambo makubwa hivyo anaaminiwa.”

Kwa upande wa aliyekuwa beki wa Simba, Boniface Pawasa alisema; “Nidhamu ndiyo ambayo inamfanya Tshabalala afike hapa alipo leo kwa sababu ni mchezaji ambaye hana mambo mengi na amekuwa akiamini katika mazoezi kitu ambacho kinamfanya ahudumu kwa ubora ule ule muda mrefu.”

Valentino Nouma aliyesajili Simba msimu huu kushindania namba na Tshabalala tayari ametangaza kuachia ngazi kutafuta changamoto mpya.

Beki huyo mwanzoni mwa msimu wa 2024/25 alisaini mkataba wa miaka miwili akitokea ASEC Mimosas lakini ameitumikia Simba kwa msimu mmoja na kufikia makubaliano na timu hiyo kuvunja mkataba.

Tshabalala aliyejiunga na kikosi cha hicho mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar ni usajili bora uliofanywa na Simba katika muongo mmoja sasa kwani  nyota huyo ametimiza miaka 12 ndani ya kikosi hicho tangu ameungana nayo na amekuwa akicheza kikosi cha kwanza panga pangua.

Klabu hiyo imekuwa ikisajili wachezaji wengi lakini hakuna hata mmoja aliyefikia rekodi za beki huyo pale Msimbazi kuanzia mataji hadi mechi za kucheza kwa waliopo sasa.

Nahodha huyo amedumu kwenye kikosi cha kwanza cha Simba kwa miaka 12 mfululizo chini ya makocha zaidi ya kumi na amekuwa nyota wa kikosi cha kwanza bila kujali nani ameongezwa nani kutoka Taifa gani.

Ukiondoa Nouma, katika eneo lake aliletewa washindani wa namba zaidi ya 20 lakini wote waligonga mwamba. Jamal Mwambeleko baada ya msimu bora akiwa na Mbao FC, alisajiliwa na Simba ili kuongeza nguvu kwa Tshabalala na ikiwezekana kumpumzisha lakini alijikuta akisugua benchi na baadaye kuondoka Msimbazi na kutimkia Stand United.

Mghana, Asante Kwasi aliyejiunga na Simba mwaka 2017 akitokea Lipuli. Huyu kwa kiasi alifurukuta na kumuweka benchi Tshabalala kwenye baadhi ya mechi lakini baadaye alipoteza namba na mwisho wa yote kuondoka Simba na kujiunga na Hafia ya Guinea mwaka 2019.

Simba ikamsajili Gadiel Michael Kamagi akiwa wa moto kutoka Yanga. Kipindi hicho hata timu ya taifa Tshabalala alikuwa akisubiri kwa Gadiel lakini pale Msimbazi mambo yakabadilika kwani alisota benchi na baadaye kuamua kuondoka kujiunga na Singida Big Stars kabla ya kwenda Afrika Kusini.

Kwa sasa yupo Tshabalala amebaki mwenyewe kwenye eneo lake. Hakuna beki wa kushoto asilia ndani ya kikosi cha Simba na mara nyingi Israel Mwenda ambaye asili yake ni kulia ndiye hupewa nafasi ya kucheza eneo hilo kama Tshabalala hayupo.

Akiwa na jezi ya Simba, Tshabalala ametwaa mataji mengi ikiwemo ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne, Ngao ya Jamii mara tano, Kombe la Mapinduzi mara mbili na Kombe la Muungano mara moja.

Pia ameisaidia Simba kufanya vizuri kwenye michuano ya CAF akiifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne, robo fainali ya Kombe la Shirikisho mara moja na amecheza fainali ya Kombe la Shirikisho hivyo amevaa medari ya CAF.

Aidha, ni mchezaji muhimu katika kikosi cha Taifa Stars ambapo amecheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mara mbili kati ya tatu ambazo Stars imeshiriki na sasa ni sehemu ya kikosi kinachojiandaa na mechi za mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) 2025.

Related Posts