Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Faustina Mfinanga maarufu Nandy, amesema kuzinduliwa rasmi kwa nembo ya Made in Tanzania ni ishara kuwa kama nchi inaweza kufanya vitu vikubwa, ikiwemo uzalishaji wa bidhaa.
Nandy ambaye pia ni mfanyabiashara wa bidhaa mbalimbali za ngozi zilizopewa jina la Shushi, kwa sasa anatengeneza bidhaa zake nchi za nje na kuziuza katika soko la Tanzania.
Amesema hayo leo Jumamosi, Julai 12, 2025, katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini hapa.
Nandy amesema baada ya kutembea na kuona bidhaa nyingi zinazozalishwa nchini, amebaini kuwa inawezekana, hasa baada ya kuona baadhi ya watu tayari wanamiliki viwanda.
“Ni kitu kikubwa kimenipa motisha kuwa inawezekana Tanzania kufanya vitu vikubwa, kwani mara nyingi tumeona bidhaa zinavyotengenezwa zinatoka nje, wakati ndani tunaweza kutengeneza,” amesema.

“Na hii imenipa motisha kuwa naweza kuwa na kiwanda changu na kutengeneza bidhaa hapa nchini badala ya kutoa nje ya nchi.”
Nandy ambaye mbali na kutembelea maonyesho ya Sabasaba kwa ajili ya kutumbuiza katika Tamasha la Sabasaba chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, pia amepata fursa ya kuhudumia wateja kupitia banda lake lililopo ndani ya kijiji hicho cha wizara.
Mwanamuziki huyo ni kati ya wasanii wengi waliopewa mabanda ya kuuza bidhaa zao katika kijiji hiki, ikiwa ni moja ya hatua ya kukuza biashara zao kupitia watembeleaji waliofika kupata huduma.
“Wengi wamefanya, nimeona sisi tutafuata nyayo ili tuwe wakubwa zaidi na tutajipa muda wa kujifunza zaidi ili kupata mwongozo mzuri wa kwenda mbele, ili tutangaze nembo ya Made in Tanzania kimataifa,” amesema Nandy.
Nandy ambaye alikusanya umati wa watu kila alipopita ndani ya mitaa ya uwanja wa Sabasaba, walinzi wake wawili waliovalia mavazi meusi walikuwa wakihakikisha msanii huyo hasukumwi na mashabiki waliokuwa wakitaka kupiga naye picha.
Kuzinduliwa kwa nembo ya Made in Tanzania, kunatajwa kuwa hatua muhimu ya maendeleo nchini na itaitambulisha Tanzania kimataifa kama Taifa lenye bidhaa zenye ubora, ubunifu na fahari ya Kiafrika.
Nembo hiyo ilizinduliwa Julai 7, 2025, na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, alipofungua rasmi maonyesho hayo.
Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Dk Mwinyi alisema Made in Tanzania iwe chachu ya kukuza uzalendo wa kibiashara na kila Mtanzania atumie bidhaa za ndani.
“Nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kupenda na kuthamini bidhaa zetu ili kuzidi kuimarisha biashara na viwanda vyetu vya ndani na kuchangia ukuaji wa uchumi wetu,” alisema Dk Mwinyi.
Aliziagiza Wizara za Viwanda na Biashara katika pande zote mbili za nchi, na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), kuhakikisha elimu ya alama hiyo inawafikia wazalishaji, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
“Alama hii iwe chachu ya kukuza uzalendo wa kibiashara, kuhamasisha kila Mtanzania kujivunia, kutumia na kutangaza bidhaa zetu,” alisema Dk Mwinyi.