Pacome awatema Chama na Kibu MVP, Juni

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Juni wa Ligi Kuu Bara akiwaacha Clatous Chama na Kibu Denis wa Simba.

Mbali na Pacome lakini aliyekuwa kocha wa Yanga, Miloud Hamdi pia amechaguliwa kocha bora wa mwezi mbele ya Rachid Taoussi wa Azam FC na Fred Felix wa Pamba Jiji.

Pacome alionesha mwendelezo wa kiwango chake akiwashinda Chama na Kibu wa Simba, alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo mitatu ambayo Yanga ilicheza mwezi huo akifunga mabao matatu na kuhusika na bao moja kwa dakika 242 alizocheza.

Nyota huyo alijiunga na Yanga msimu 2023/24 akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast na amefunga jumla ya mabao 19 ndani ya Ligi Kuu.

Kwa upande wa Hamdi aliyeingia fainali na Rachid Taoussi wa Azam FC na Fred Felix wa Pamba Jiji, aliiongoza Yanga kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo na kutwaa ubingwa wa wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu wa 2024/2025. Yanga ilizifunga Tanzania Prisons (0-5), Dodoma Jiji (5-0) na Simba (2-0).

Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara, Jackson Mwendwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Juni kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

Related Posts