Rais Mwinyi ataja mambo matatu yanayoongeza wawekezaji Zanzibar

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema wawekezaji wazawa kuendelea kuwekeza fedha zao nchini ni ishara kwamba Zanzibar hivi sasa inaaminika kutokana na mazingira mazuri ya biashara, sera nzuri na maendeleo yanayofanyika katika sekta mbalimbali yanayochangia kukua kwa sekta ya utalii.

Ametoa kauli hiyo leo Julai 12, 2025 wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa hoteli ya nyota tano Golden Tulip, inayomilikiwa na kampuni ya wazawa ya Royal Suites of Zanzibar Ltd.

“Hii ni ishara tosha kwamba Zanzibar inazidi kuaminika katika uwekezaji na mazingira na sera zake za uwekezaji zinavutia wengi,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema Serikali inaendelea kufanya jitihada kubwa katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa kuhakikisha kuwa maeneo yote ya uwekezaji Zanzibar, yanaunganishwa na miundombinu ya barabara bora, umeme na maji safi na salama.

Pia amesema Serikali inarahisisha taratibu za uwekezaji ambapo kwasasa inatumia mfumo wa kituo kimoja cha utoaji wa huduma za uwekezaji ndani ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa) kwasasa ina uwezo wa kutoa cheti cha uwekezaji ndani ya saa 24 baada ya mwekezaji kukamilisha taratibu zote zinazohusika.

Amesema nchi inatekeleza dira ya maendeleo ya mwaka 2020-50 na mpango wa maendeleo wa miaka mitano ambapo utalii ni moja ya sekta kiongozi katika kukuza uchumi na kutoa ajira.

“Ni dhahiri kuwa mradi huu utachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wetu, kuongeza fursa za ajira hususani vijana na wanawake katika sekta za utalii na kukuza taswira ya Zanzibar kama kivutio cha mikutano ya kimataifa kwa lengo la kuongeza watalii wa hali ya juu wanaotembelea nchi yetu,” amesema.

Kiongozi huyo wa nchi, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha uwekezaji unakuwa na manufaa katika pande zote, lengo ni kuona miradi inachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya nchi kupitia matumizi ya rasilimali, uwezeshaji wafanyakazi wazawa na uwekezaji utalii wa kijani na endelevu Zanzibar.

Ametumia fursa hiyo kuwaahidi wawekezaji wote Zanzibar kwamba Serikali itaendelea na jitihada zake kuhakikisha mazingira mazuri ya kufanya biashara yanaimarishwa siku hadi siku ili kuwafanya wawekezaji waendelee kuwekeza nchini, na itaendelea kutafuta miradi mbalimbali ya maendeleo kujenga viwanja vya ndege barabara za ndani na kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi na nishati.

“Kumarika kwa miudombinu ya kiuchumi kwa huduma za kijamii, kuitafanya Zanzibar kuwa kitovu cha biashara ya utalii katika ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati,” amesema Mwinyi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), Seif Abdalla Juma amesema mradi huo umezingatia vigezo vya ulinzi na usalama, kama inavyotakiwa kwenye viwanja vya ndege.

Amesema zamani viwanja vya ndege vilitumika kama eneo la kuwasili na kuondokea abiria, lakini kwa sasa kuna dhana ya mabadiliko ya kuvifanya viwanja vya ndege kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji ambapo kwasasa vinajumuisha vituo vya biashara, makazi, maduka na hoteli.

“Kwa hiyo hata sisi tumehakikisha kuwa uwanja huu kinakuwa kitovu kamili cha huduma na biashara ili kuendana na mabadiliko haya, hivyo tunatarajia kuzindua kituo cha biashara ili kuimarisha biashara na huduma katika uwanja huu,” amesema Seif.

Mkurugenzi Mtendaji wa Zipa, Saleh Saad Mohamed amesema tangu kuanzishwa kwake imesajili miradi 1,380 yenye mtaji wa zaidi ya dola za marekani 12.5 milioni (Sh23.389 biliioni) lakini kwa kipindi cha serikali ya awamu ya nane mamlaka imesajili zaidi ya miradi 483 yenye mtaji zaidi wa Dola za Marekani milioni 6.1 (Sh15.806 bilioni) sawa na asilimia 50 ya mtaji wote.

“Katika miradi yote inatarajia kutoa ajira zaidi ya 25,000, miradi 145 imesajiliwa katika mkoa wa Mjini Magharib yenye mtaji zaidi ya Dola za Marekani milioni 3.1 (Sh8.032 bilioni) ikiwa ni sawa na asilimia 50 ya mtaji wote ambao umewekezwa Zanzibar katika kipindi hiki,” amesema Saleh.

Mwekezaji wa mradi huo, Hassan Mohamed Raza amesema katika awamu ya kwanza ya mradi huo wametoa ajira za moja kwa moja 98 na awamu hii ya pili wametoa ajira 90, hivyo kufanya awamu zote mbili kutoa ajira 188 kati ya hizo ajira 180 ni za wazawa sawa na asilimia 96. Wageni ni asilimia nne.

Amesema kwa kipindi cha miaka minne kupitia uwekezaji huo tayari wamelipa Serikalini jumla ya Sh6 bilioni.

“Katika awamu zinazokuja tunatarajia kujenga miradi minne itakayokuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 25 sawa na Sh64 bilioni, kulingana na azma ya serikali ya kuwa na mikutano ya kimataifa itakuwa ni sehemu ya miradi hiyo ambayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2028,” amesema.

Related Posts