Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema wawekezaji wazawa kuendelea kuwekeza fedha zao nchini ni ishara kuwa Zanzibar inaaminika kutokana na mazingira mazuri ya biashara na sera nzuri.
Rais Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Julai 12, 2025, wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa hoteli ya nyota tano ya Golden Tulip, iliyopo eneo la Uwanja wa Ndege, Unguja. Inamilikiwa na kampuni ya wazawa ya Royal Suites of Zanzibar Ltd.
“Hii ni ishara tosha kwamba Zanzibar inazidi kuaminika katika uwekezaji, mazingira na sera zake za uwekezaji zinavutia wengi,” amesema.
Dk Mwinyi amesema Serikali inaendelea kufanya jitihada za kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa kuhakikisha maeneo yote ya uwekezaji Zanzibar yanaunganishwa na miundombinu ya barabara bora, umeme, maji safi na salama.
Amesema Serikali inarahisisha taratibu za uwekezaji, akieleza kuwa sasa inatumia mfumo wa kituo kimoja cha utoaji huduma za uwekezaji ndani ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa).
Kwa hatua hiyo, kuna uwezekano sasa cheti cha uwekezaji kutolewa ndani ya saa 24 baada ya mwekezaji kukamilisha taratibu zote zinazohusika.
Rais Mwinyi amesema nchi inatekeleza Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020–2050 na mpango wa maendeleo wa miaka mitano, ambao utalii ni moja ya sekta kiongozi katika kukuza uchumi na kutoa ajira.
“Ni dhahiri kuwa mradi huu utachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wetu, kuongeza fursa za ajira, hususani kwa vijana na wanawake katika sekta za utalii, na kukuza taswira ya Zanzibar kama kivutio cha mikutano ya kimataifa kwa lengo la kuongeza watalii wanaotembelea nchi yetu,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha uwekezaji unakuwa na manufaa katika pande zote; lengo ni kuona miradi inachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo kupitia matumizi ya rasilimali, uwezeshaji wa wafanyakazi wazawa, na uwekezaji wa utalii wa kijani na endelevu Zanzibar.
Dk Mwinyi amewaahidi wawekezaji wote Zanzibar kwamba Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kutafuta miradi ya maendeleo, ikiwamo kujenga viwanja vya ndege, barabara za ndani na kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi na nishati.
“Kuimarika kwa miundombinu ya kiuchumi na huduma za kijamii kuitafanya Zanzibar kuwa kitovu cha biashara ya utalii katika ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), Seif Abdalla Juma, amesema mradi huo umezingatia vigezo vya ulinzi na usalama kama inavyotakiwa kwenye viwanja vya ndege.
Amesema zamani viwanja vya ndege vilitumika kama maeneo ya kuwasili na kuondokea abiria, lakini sasa kuna dhana ya mabadiliko ya kuvifanya kuwa vituo vya biashara na uwekezaji, vikijumuisha vituo vya biashara, makazi, maduka na hoteli.
“Kwa hiyo, hata sisi tumehakikisha uwanja huu unakuwa kitovu kamili cha huduma na biashara ili kuendana na mabadiliko haya. Hivyo tunatarajia kuzindua kituo cha biashara,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Zipa, Saleh Saad Mohamed, amesema tangu kuanzishwa kwake, imesajili miradi 1,380 yenye mtaji wa zaidi ya Dola milioni 12.5 za Marekani (Sh23.389 bilioni), lakini kwa kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nane, mamlaka imesajili zaidi ya miradi 483 yenye mtaji wa zaidi ya Dola milioni 6.1 (Sh15.806 bilioni), sawa na asilimia 50 ya mtaji wote.
“Miradi yote inatarajia kutoa ajira zaidi ya 25,000. Miradi 145 imesajiliwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi, yenye mtaji wa zaidi ya Dola milioni 3.1 (Sh8.032 bilioni), ikiwa ni sawa na asilimia 50 ya mtaji wote ambao umewekezwa Zanzibar katika kipindi hiki,” amesema.
Mwekezaji wa mradi huo, Hassan Mohamed Raza, amesema katika awamu ya kwanza wametoa ajira za moja kwa moja 98, na awamu hii ya pili wametoa ajira 90. Hivyo kufanya jumla ya ajira 188, kati ya hizo 180 ni za wazawa sawa na asilimia 96; wageni ni asilimia nne.
Amesema kwa kipindi cha miaka minne kupitia uwekezaji huo, wamelipa serikalini Sh6 bilioni.
“Katika awamu zinazokuja, tunatarajia kujenga miradi minne ambayo itakuwa na thamani ya Dola milioni 25 (sawa na Sh64 bilioni). Kulingana na azma ya Serikali ya kuwa na mikutano ya kimataifa, itakuwa ni sehemu ya miradi hiyo ambayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2028,” amesema.