Richard Huff: Mwanaume mwenye tattoo zaidi ya 240

Dar es Salaam. Methali ya Kiswahili isemayo “Usimhukumu mtu kwa sura yake” ni ya zamani lakini bado ina maana, hasa wakati ambao mwonekano wa mtu hauendani na matarajio ya jamii.

Richard Huff (51), ambaye mwili wake umejaa tattoo zaidi ya 240, zikiwemo kadhaa usoni, ni baba wa watoto watano na mume mwenye mapenzi ya dhati.

Sanaa hiyo ya mwilini, ikiwemo majina ya watoto wake na midomo ya binti zake, ni njia yake ya kujieleza. Lakini badala ya kuvutiwa naye, watu wengi humhukumu kwa ukali kutokana na mwonekano wake.

“Iligeuka kuwa kama uraibu,” Richard ameeleza. “Nilianza na miguu, na nikapanda juu.” Sasa, akiwa na asilimia 85 ya mwili wake yenye tattoo, analenga kuufunika mwili wake wote kwa tattoo ndani ya miaka minne ijayo.

“Sijui kama ni maumivu au uzuri wa sanaa yenyewe, lakini ni kitu cha kuvutia,” ameongeza.

Licha ya kujihusisha kikamilifu na maisha ya watoto wake, ikiwemo kuhudhuria vikao vya shule, mwonekano wake huvutia mitazamo isiyotarajiwa.

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule ya watoto wake humwona ni mtu wa kutisha. Hata hivyo, binti yake humtetea mara kadhaa;

“Wanasema anaogopesha, lakini mimi huwaambia, ‘Hapana, baba yangu haogopeshi, ni mtaalamu tu wa tattoo,’” anasema binti yake.

Hata mke wake, Marita, anakiri kwamba awali alimwelewa vibaya. “Nilimwogopa mwanzoni, na nilimhukumu kutokana na sura yake, lakini nilipomfahamu vizuri, nikagundua kuwa ni mtu mwema na mwenye mapenzi ya dhati.”

Marita, ambaye alikuwa na watoto watatu kutoka mahusiano ya awali, anasema Richard aliwapokea kama wake kabisa. “Yeye ni zaidi ya baba wa kweli kwao.”

Amesema mara kwa mara hushiriki maisha yao ya kifamilia mtandaoni, akichapisha picha na video zinazoonyesha upendo na huruma.

Lakini bado, si kila mtu huweza kuona zaidi ya tattoo zake. Mtu mmoja aliandika, “Sina shida na tattoo, lakini kwa kweli, je, alihitaji kuwa nazo hadi usoni?”

Wapo pia wanaomtetea. “Anapenda tattoo zake za usoni. Yeye ni baba mzuri. Mwacheni aishi,” aliandika shabiki mwingine.

Richard hajali maneno ya chuki. “Mtu akitoa maoni mabaya, inaonyesha zaidi kuhusu wao kuliko kuhusu mimi,” amesema. “Sisi tuko na furaha, watoto wetu wako na furaha, na hicho ndicho cha muhimu zaidi.”

Ameongeza, “Kuwa na tattoo hakunifanyi niwe baba mbaya, inawapa watoto wangu mtazamo mpana zaidi wa maisha. Hawaogopi, wananipenda jinsi nilivyo.”

Mwisho wa siku, Richard Huff ni kumbusho muhimu kuwa mapenzi, siyo mwonekano, ndiyo yanayomfanya mtu awe mzazi wa kweli.

Related Posts