Rose autaka urais kupitia chama cha CUF

Mbeya. Mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), Rose Kahoji amekuwa mwanamke wa tatu nchini kutangaza nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Kwa hatua hiyo, Kahoji anaungana na Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan wa CCM, ambaye tayari amepitishwa na chama chake kuwania nafasi hiyo.

Rais Samia alipitishwa rasmi na Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliofanyika Januari 19, 2025, kuwa mgombea urais wa Jamhuri kupitia tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Mbali na Rais Samia, Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Dorothy Semu, naye alichukua fomu Aprili 22, 2025, kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Jamhuri kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, hadi sasa wanawake watatu wamejitokeza kuwania nafasi hiyo kupitia vyama tofauti vya siasa, hatua inayoashiria kuimarika kwa ushiriki wa wanawake katika uongozi wa kitaifa.

Akizungumza leo Julai 12, baada ya kukabidhiwa fomu ya kugombea urais, Rose Kahoji mkazi wa Mbeya amesema ameamua kujitosa katika uchaguzi huo ili kupigania masilahi na maisha bora ya wananchi katika huduma mbalimbali.

Mtia nia katika nafasi ya urais kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), Rose Kahoji (kushoto) akipokea fomu ya kugombea nafasi hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Mbeya, Yassin Mrotwa. Picha na Saddam Sadick



“Uchumi wa wananchi ni mdogo hadi kufikia hatua ya kukosa milo mitatu kwa siku, huduma za afya vituo vipo lakini lakuna huduma ikiwamo vifaatiba, madawa na wahudumu na muda mwingine gharama ziko juu.

“Chama changu kikinipa ridhaa nitapambana na wasiojulikana, kuimarisha uchumi, miundombinu na huduma za kijamii, nimejipima nimeona nafaa kuwaongoza Watanzania,” amesema Kahoji.

Mtia nia huyo amesema ana uzoefu na uwezo wa kutosha, akiwa amehudumu katika nafasi mbalimbali ndani na nje ya chama.

Ameongeza kuwa amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya kisiasa kwa zaidi ya miaka 30, akishiriki katika nafasi tofauti ndani ya chama hicho, jambo linalompa ujasiri wa kuwania nafasi ya urais.

“Kwa sasa ni Mjumbe wa Baraza Kuu CUF Taifa, nimewahi kuwa Mwenyekiti wa Wanawake Wilaya ya Mbeya Mjini, nimewahi kugombea ubunge Afrika Mashariki 2013, nimewahi kugombea ubunge 2000 na nafasi nyingine serikalini hadi kufukuzwa kazi kwa ajili ya siasa,” amesema Rose.

Kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba, Kahoji amewataka wananchi kuwa watulivu, akibainisha kuwa CUF kimeshachukua msimamo wa kuunga mkono mabadiliko hayo.

Amesema suala hilo ni la mchakato unaohitaji uvumilivu, likiwemo kuundwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Ameeleza kuwa CUF ni miongoni mwa waasisi wa madai ya mabadiliko ya Katiba na imekuwa mstari wa mbele kushinikiza mageuzi hayo muhimu kwa mustakabali wa taifa.

“Niwaombe wananchi wenye nia kugombea nafasi yoyote kwa sifa, wajitokeze katiba inaruhusu, tunahitaji mabadiliko na CUF ndio waasisi wa kutaka katiba mpya na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ” amesema.

Mwenyekiti wa chama hicho wa mkoa huo, Yassin Mrotwa amesema hadi sasa mwitikio wa uchukuaji na urejeshaji fomu ni mzuri na mwisho wa zoezi hilo kwa nafasi za udiwani, ubunge na urais ni Julai 15 mwaka huu.

“No Reforms, No Election haina tatizo, kinachohitajija ni kuona mabadiliko, miaka tuliyoishi kwa chama kimoja madarakani lazima tupate nguvu mpya na CUF ndio suluhisho, wananchi watuunge mkono tuweze kuwatumikia wananchi,” amesema Mrotwa.

Katibu wa chama hicho mkoa, Ibrahim Mwakwama amesema hadi sasa wagombea katika nafasi ya udiwani ni 34 kwa ngazi ya mkoa, huku wabunge wakiwa watano katika majimbo ya Mbeya Mjini, Mbeya Vijijini, Kyela, Uyole na Rungwe.

“Tunaamini hadi kufikia muda uliowekwa idadi inaweza kuongezeka kutokana na muitikio ulivyo, tunaendelea kuwahamasisha wanachama kutimiza haki yao kikatiba,” amesema Mwakwama.

Related Posts