Simba Queens kuanza upya | Mwanaspoti

KOCHA msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan Mgosi amesema kipindi cha usajili kinachoendelea kwa sasa, wanafumua kikosi hicho na kuingiza sura nyingi chipukizi, lengo ni kutengeneza ushindani wa ndani na nje.

Mgosi alisema mipango ya Simba Queens msimu ujao ni mikubwa baada ya uliyoisha 2024/25 kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake (TWPL) huku JKT Queens ikiwa bingwa.

“Simba Queens msimu ujao itakuwa na sura mpya nyingi na chipukizi, kwani tunahitaji kujenga timu upya ambayo itakuwa na ushindani wa namba hadi na ushindani kwa timu pinzani,” alisema Mgosi na kuongeza.

“Tutaachana na wachezaji wengi mtakaowaona timu pinzani na sisi kikosi chetu kitakuwa na sura mpya nyingi, jambo la msingi tumeamua kujipanga upya kwa kuzingatia kuchukua wenye vipaji vikubwa tutakavyovikuza.”

Mgosi alisema kwa sasa mpira wa miguu wa wanawake umeanza kukua, hivyo lazima watumia muda mwingi kusaka vipaji ambavyo vitakuja kuwalipa baadaye.

“Ninaposema kutulipa namanisha timu ambayo itakuwa inanyakua mataji baki tu baki, wachezaji ambao timu za nje zitakuwa zinatamani kuwanunua, ndiyo maana tuona tujipange na matunda yataonekana katika hilo tunalolifanya,” alisema Mgosi nahodha wa zamani wa Simba.

Related Posts