Iringa. Ni vilio! Ndivyo unavyoweza kuelezea hali iliyotawala katika eneo la Soko la Mashine Tatu mjini Iringa baada ya moto kuteketeza vibanda 429 vya ndani, 86 vya nje ya soko hilo na kuathiri shughuli za biashara kwa zaidi ya wafanyabiashara 500 waliokuwa wakitegemea eneo hilo kwa maisha yao ya kila siku.
Moto huo, ambao imeelezwa kuwa ulizuka majira ya saa nane usiku, ukienea kwa kasi kubwa huku ukizidi uwezo wa kudhibitiwa kwa haraka na hivyo kuharibu mali kwa mujibu wa mashuhuda.
Mwenyekiti wa Masoko Manispaa ya Iringa, Raphael Ngulo, akizungumza na waandishi wa habari Julai 13, 2025 alithibitisha kuwa jumla ya vibanda 86 vya nje ya soko vimeteketea na vibanda 429 vya ndani ya soko pia vimeathirika kwa viwango tofauti.

“Hili ni pigo kubwa kwa wafanyabiashara wetu na tunaiomba Serikali na wadau mbalimbali kujitokeza na kusaidia hawa waathirika kuweza kuanza upya,” amesema.
Wakizungumza na Mwananchi Digital baadhi ya wahanga wa tukio hilo, wameeleza kuwa walianza kupokea taarifa za uwepo wa moto huo kutoka kwa wafanyabiashara wengine na baadhi ya wakazi jirani na eneo hilo.
”Nimepoteza kila kitu na hakuna hata mzigo wa kuuza uliosalia na kinachofanya nilie nilikuwa na mkopo benki sijui hata nitaanza wapi ni Mungu atusaidie,” amesema Sophia Mwakitalima, mfanyabiashara wa soko hilo.
”Nimewekeza zaidi ya milioni mbili sokoni hapa. Kwa sasa sina hata mtaji mwingine kwa kweli tunahitaji msaada wa dharura,” amesema Godfrey Mgonja Mfanyabiashara wa kuku.

Muonekano wa Soko la Mashine Tatu lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa likiwa linaungua usiku wa kuamkia leo Julai 12, 2025.
Baadhi ya wakazi jirani na soko la mashine tatu halmashauri ya Manispaa ya Iringa wameieleza Mwananchi Digital kuwa hali hiyo ilianza usiku wa kuamkia leo, ambapo wafanyabiashara na wananchi wa eneo hilo waliendelea kufika eneo la tukio ili kuokoa mali.
”Tuliona moshi mkubwa ukitokea sokoni. Ndani ya dakika chache, moto ulishika kila upande yaani ilikuwa ni balaa,” amesema Emmanuel Lyimo, mkazi jirani na eneo la soko.
Dereva bajaji Mussa Kipanga ameeleza, ”Moto ulianza kwenye kibanda cha katikati. Ilionekana kama mtego kwa sababu ulikuwa mkali sana na wa haraka.”
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Iringa, Mrakibu Mwandamizi Jackline Mtui, amethibitisha kupokea taarifa ya moto huo kupitia namba ya dharura 114 na kueleza kuwa walifika mapema, lakini gari lao la kwanza lilipata hitilafu hali iliyochelewesha udhibiti wa moto huo.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta amesema kuwa tathmini ya hasara inaendelea kufanywa, huku taratibu za kuwahudumia waathirika zikiwa zinapangwa.
”Tunaendelea kufuatilia kwa karibu kujua kiwango halisi cha uharibifu na namna bora ya kusaidia wahanga,” amesema Sitta.
Aidha Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoani Iringa kupitia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mjumbe wa Halmashauri ya CCM Taifa, Salim Abli (Asas) amesema watakaa na kuona ni kwa jinsi gani tunawasaidia waathirika wa tukio hilo.
Soko hilo la mashine tatu ni miongoni mwa masoko maarufu na ya zamani Manispaa ya Iringa, likihudumia mamia ya wafanyabiashara wa mali mbichi, vyakula, vifaa vya nyumbani na huduma ndogo ndogo.
Kwa mujibu wa viongozi wa soko hilo wameeleza kwamba tukio hilo ni la kwanza kutokea na kwa sasa wafanyabiashara wanasalia katika majonzi wakisubiri msaada kutoka kwa Serikalini, mashirika na watu binafsi, huku matumaini ya kurejea katika biashara yakiwa mbali kutokana na kiwango cha hasara kilichopatikana.