KIPYENGA cha usajili tayari kimepulizwa. Kikimaanisha kwamba klabu mbalimbali zimeingia sokoni kusaka nguvu mpya tayari kwa msimu ujao wa michuano mbalimbali.
Yanga, Simba pamoja na Azam na Singida Black Stars ni miongoni mwa timu zilizowekeza nguvu kubwa kwenye usajili zikiangalia zaidi ushiriki wao kimataifa msimu ujao.
Staa wa Yanga, Maxi Nzengeli ameingia kwenye rada za Simba baada ya duru za usajili kuonyesha kuwa klabu hiyo ilimpelekea ofa mchezaji huyo kupitia mmoja wa wasimamizi wake hivikaribuni.
Tetesi za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka kwa mmoja wa wasimamizi wa Maxi ni kwamba mkataba wake ulikuwa umeisha mwisho wa msimu uliopita ingawa Yanga walishampa nakala mpya ya miaka miwili kwa mujibu wa Mwanaspoti, lakini Simba wakapenyeza karata yao.
Mmoja wa watu wa karibu na Nzengeli, amelidokeza Mwanaspoti kuwa Simba ilipeleka ofa ya dola 250,000 (zaidi ya Sh 650 milioni) ili kumshawishi mchezaji huyo lakini alipoambiwa habari hiyo akashtuka na kuingiwa uoga wa kufanya uamuzi.
Habari zinasema kwamba licha ya kwamba alionyesha kuitamani ofa hiyo lakini akahofia ugomvi na uhasama utakaotokea baada ya yeye kufanya uamuzi wa kutaka kuhama haswa kwa kurejea rekodi za nyuma za watani wa jadi.
“Simba iliweka dola 250,000 ili kuhitaji huduma yake, alizikataa na akataka maisha yake ya soka kwa Tanzania yaishie Yanga, kwani alikuwa anasikia na kuziona changamoto za wachezaji walihama kutoka sehemu moja kwenda nyingine,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Nzengeli ni mchezaji mpole hapendi mambo ya vurugu, hivyo ikawa ngumu kwake kufanya maamuzi, ukiachana na Simba ujio wa kocha mpya wa Azam, Florent Ibengé alikuwa anamtaka Nzengeli katika kikosi chake bado likawa gumu kufanyika.
“Siwezi kusema imeshindikana kabisa pesa ina nguvu na anaweza akaamua lolote lile, Yanga ilikuwa asaini miaka miwili mechi ya mwisho ya Kombe la FA, sasa kilichoendekea sijajua,”kiliongeza chanzo hicho huku watu wa Yanga wakiwa wagumu kufafanua kinachoendelea dhidi ya Maxi pamoja na wachezaji wengine wa msimu uliopita.
Habari zinasema Ibenge kabla hajasaini Azam alikuwa akitumia ushawishi wake kumpata mchezaji huyo lakini mpaka sasa amekata tamaa na huenda akanunua mastaa wengine kadhaa nje ya Tanzania hususani kutoka kwao DR Congo.
Nzengeli msimu uliopita alimaliza na mabao sita na asisti nane, huku ule wa 2023/23 alikuwa na mabao 11, asisti mbili alicheza dakika 2090.
Habari za uhakika zinasema kwamba Simba ipo kwenye mawindo ya kimyakimya ya kupanga upya kikosi chake kwa kununua wachezaji kadhaa wenye uzoefu mkubwa na huenda baadhi yao wakawa wa ndani ya Tanzania ikiwemo kutoka kwa wapinzani wake wakubwa Yanga, Azam na Singida.
Usajili wa msimu huu umeanza Julai 1 na utafungwa Septemba 7 kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) huku likisisitiza hakuna muda wa ziada utakaoongezwa baada ya hapo.