Tanzania kusaka watalii milioni nane hadi 2030

Dar es Salaam. Tanzania imedhamiria kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni nane mwaka 2030, ikiwa ni ongezeko kutoka watalii zaidi ya milioni tano waliokuwapo mwaka 2025.

Ili kuvutia idadi hiyo, imedhamiria kuboresha huduma zake na kupanua wigo wa utangazaji vivutio vilivyopo ili wageni na Watanzania waweze kuvitambua na kuvitembelea.

Hayo yamesemwa leo, Julai 12, 2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana wakati akizindua Siku ya Ngorongoro katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea jijini hapa.

Dk Pindi amesema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la idadi ya watalii wa ndani na nje wanaotembelea mbuga za wanyama, jambo ambalo limechochewa na utangazaji wa vivutio uliofanywa na Serikali, ikiwemo filamu ya Royal Tour na Amazing Tanzania.

“Kwa sasa wanaotembelea hifadhi ni wengi hasa nyakati za sikukuu, watu binafsi, familia, ofisi na hata kwaya, na hii imefanya idadi ya watalii kufikia zaidi ya milioni tano na sasa tunaitafuta milioni nane ambayo tumeambiwa kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na inawezekana,” amesema.

Ilani hiyo ni ile ambayo inatarajiwa kutumika katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kuanzia mwaka 2025 hadi mwaka 2030, iliyozinduliwa miezi michache iliyopita.

New Content Item (1)


New Content Item (1)

Dk Chana amesema wanatambua umuhimu wa sekta ya utalii, ndiyo maana wanaweka umakini ili iwanufaishe watu walio katika mnyororo wa thamani.

Akizungumzia uwepo wa Siku ya Ngorongoro katika maonyesho ya Sabasaba, amesema inasaidia kutangaza utalii wa ndani, ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutangaza vivutio mbalimbali.

“Tunaunga mkono kwa kuwa na Siku ya Ngorongoro katika viwanja vya Sabasaba, hili ni moja ya jambo linalosaidia kuipaisha Ngorongoro kwa kuongeza idadi ya watalii na mapato,” amesema.

Hali hiyo imefanya sasa mapato yaliyokusanywa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kufikia Sh269.9 bilioni ndani ya mwaka 2024/2025

“Kiwango hiki ni kikubwa na kinaashiria kuwa juhudi za kutangaza utalii zilizofanyika, sisi kama wizara lazima tuziunge mkono ili idadi ya watalii iweze kuongezeka zaidi,” amesema Dk Chana.

Amesema zimekusanywa ikiwa ni matokeo ya jitihada mbalimbali za kutangaza utalii wa ndani na nje ili watalii na mapato yaongezeke.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis amesema sekta ya uhifadhi ni kivutio kikubwa kwa wananchi, kwani mchango wake umeonekana hata ndani ya maonyesho ya Sabasaba.

Hiyo ni baada ya banda la Maliasili na Utalii kuvutia watembeleaji 659,604 tangu maonyesho yalipoanza Juni 28 hadi Julai 11 mwaka huu, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka zaidi pindi maonyesho yatakapofikia tamati.

“Hii inaonyesha namna sekta ya uhifadhi ilivyo kivutio kikubwa kwa wananchi, huku lengo la maonyesho haya likiwa ni kuhakikisha tunatangaza zaidi vivutio vilivyopo,” amesema.

Amesema Mamlaka ya Ngorongoro imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutokana na aina ya maisha yanayopatikana, ambayo yanaruhusu muingiliano wa wanyama na binadamu katika eneo moja.

“Siku hii iwe chachu ya kuitangaza Ngorongoro kimataifa na kushirikisha wananchi katika kulinda rasilimali, hasa kwa jamii inayoishi ndani ya hifadhi hiyo kwa ajili ya manufaa ya Taifa kwa ujumla,” amesema Latifa.

Amesema watahakikisha wanaendeleza sekta ya utalii kwani wanatambua jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuikuza.

“Ni vyema tushirikiane kukuza tasnia na mnyororo mzima wa thamani,” amesema.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa NCAA, Mariam Kobelo amesema watahakikisha historia na utamaduni uliopo ndani ya hifadhi hiyo zinaendelea kutunzwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.

Related Posts