Twiga Stars, Banyana Banyana zagawana pointi WAFCON 2025

Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ imeipa mshtuko Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ baada ya kuilazimisha sare ya bao 1-1 katika mchezo uliomalizika muda mfupi uliopita wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2024 kwenye Uwanja wa Honneur, Oujda Morocco.

Katika mchezo huo, Twiga Stars ilitangulia kupata bao katika dakika ya 24 kupitia kwa Opa Clement akimalizia pasi ya Ester Maseke lakini Afrika Kusini ikasawazisha katika dakika ya 70 kupitia kwa Bambanani Mbane.

Twiga Stars kwenye mchezo huo ilipata kadi nyekundu ambayo ilionyeshwa kwa Winfrida Gerald kwa kosa la kumkanyaga mchezaji wa Afrika Kusini.

Hata hivyo Twiga Stars imeondoka na heshima ya tuzo ya mchezaji bora wa mechi ambayo imeenda kwa Diana Msewa.

Twiga Stars sasa imebakiza mchezo mmoja kwenye kundi C ambao itacheza na Ghana, Julai 14, 2025 na iwapo itapata ushindi, inaweza kutinga robo fainali kwa kigezo cha kuwa miongoni mwa timu za nafasi ya tatu zenye matokeo mazuri (best losers)

Sare hiyo imeifanya Twiga Stars kuandika historia ya kupata pointi ya kwanza katika mashindano hayo.

Kabla ya hapo, Twiga Stars haikuwahi kuambulia pointi katika fainali hizo kwenye mechi nne ambazo ilikuwa imecheza, tatu zikiwa za fainali za mwaka 2010 na moja ya fainali za awamu hii.

Katika fainali za Afrika Kusini mwaka 2010, Twiga Stars ilianza kwa kufungwa mabao 2-1 na Nigeria kisha ikachapwa mabao 3-2 na Mali na mechi ya mwisho ikafungwa mabao 3-0 na Nigeria.

Katika fainali za awamu hii, mechi ya kwanza, Twiga Stars ilifungwa kwa bao 1-0 na Mali.

Related Posts