Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema atatoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanadhibiti ufunguaji holela wa showroom za magari katika maeneo mbalimbali ya jiji.
RC Chalamila aliyasema hayo leo Ijumaa, Julai 11, 2025, wakati wa mkutano maalum wa viongozi wa Serikali na watoa huduma za kisekta za uzalishaji, uliofanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Katika mkutano huo, Chalamila alipendekeza kuwepo kwa eneo maalum litakalotengwa rasmi kwa ajili ya showroom, ili kuruhusu mji kuwa na mpangilio mzuri na kuepusha usumbufu kwa shughuli nyingine za uzalishaji.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa watendaji kubuni na kutekeleza mipango ya upangaji bora wa jiji, ili kuhakikisha maendeleo yanaendelea bila kero kwa wananchi.