Watia nia ubunge CCM presha inapanda, inashuka

Dar/Mikoani. Presha inapanda na kushuka kwa watia nia wa ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndivyo unavyoweza kusema baada ya kamati za siasa za chama hicho kuhitimisha mchakato wa kupendekeza majina ngazi za wilaya na mikoa.

Katika ngazi hizo, kamati za siasa zimewajibika kupendekeza majina matatu miongoni mwa watia nia wote wa ubunge, kisha kuyawasilisha ngazi ya Taifa kwa ajili ya vikao vya mwisho vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.

Usiri uliogubika mchujo huo umesababisha kuibuka kwa tetesi kuwa baadhi ya waliokuwa wabunge na vigogo ama wamependekezwa ngazi ya wilaya na baadaye wakarejeshwa na kamati za siasa mkoa au hawakuwamo kabisa.

Taarifa kutoka korido za ofisi za CCM na baadhi ya makada zimekuwa zikitaja majina ya makada ambao majina yao hayakuingia tatu bora, licha ya kwamba vikao hivyo ni vya siri na hakuna kiongozi aliye tayari kuitoa.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, taarifa za ndani na kutoka kwa wasiri ambao ni baadhi ya makada wa CCM, inadaiwa kuwa baadhi ya wabunge 19 wa zamani wa viti maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliojiunga na CCM wakachukua fomu kutia nia kugombea ubunge hawakupendekezwa.

Katika mapendekezo hayo, inadaiwa baadhi ya wanasiasa wazoefu si sehemu ya waliopendekezwa, ingawa bado wana nafasi katika vikao vya kitaifa ambavyo kimsingi vina mamlaka ya kuamua yeyote kati ya watia nia arejeshwe.

Mchakato unaofanyika sasa unalenga kurudisha majina matatu kwa ajili ya kupigiwa kura na wajumbe, tayari kupewa bendera ya kuipeperusha katika mbio za ubunge katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Kwa mujibu wa viongozi wa CCM, waliopendekezwa na ngazi hizo wana nafasi zaidi ya kupitishwa na vikao vya mwisho, kisha kurudishwa kwa wajumbe au baadhi ya majina kutorudi kama ilivyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumzia mchakato huo, mmoja wa makatibu wa CCM katika moja ya mikoa ya Tanzania Bara aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa sababu za kiitifaki amesema, kilichofanywa na mikoa ni kupendekeza majina matatu kati ya watia nia wote.

Lakini, kupendekezwa huko amesema haina maana kuwa majina ya watia nia wengine hayakwenda ngazi ya Taifa, bali yote yamepelekwa na kila mmoja akiwa amepewa alama ambazo zitavisaidia vikao vya juu vya uchujaji.

“Tulichofanya ni kupendekeza watatu kati ya watia nia wote katika kila jimbo, hao tumewapendekeza kwa kuwapa alama A hadi C. Kisha wao pamoja na watia nia wengine tumepeleka majina yao Taifa,” amesema.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa chama tawala amesema hatua ya kupendekeza majina matatu haina maana kuwa hao ndio watakaorudishwa kwa wajumbe, bali Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ndizo zenye mamlaka ya mwisho.

“Inawezekana tumependekeza hao watatu, lakini Kamati Kuu na Halmashauri Kuu zikaona hawastahili na zikaamua kuleta majina mengine kati ya watia nia waliopo,” amesema akisisitiza hakuna mwenye uhakika asilimia 100.

Kwa upande wake, mmoja wa wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho Taifa amesema kanuni inazitaka ngazi za mikoa kupendekeza majina matatu kati ya watia nia wote, lakini haziifungi mikoa au wilaya kupendekeza majina zaidi.

“Bado vikao havijakaa, lakini kwa kiwango kikubwa majina yaliyopitishwa na mikoa yana nafasi kubwa ya kurudishwa kwa wajumbe,” amesema na kuongeza:

“Kule Taifa tunapokaa vikao tunazingatia zaidi mapendekezo ya wilaya au mkoa husika kwa sababu ngazi hizo ndimo wanamoishi wagombea na wanazijua tabia zao, nguvu zao na kukubalika kwao ndani na nje ya chama.”

Amesema: “Kwa hiyo, pendekezo la wilaya na mkoa huwa linachukuliwa kwa uzito mkubwa, mara nyingi tunarudisha kwa wajumbe, wao waamue mmoja ili akagombee.”

Katika majimbo mbalimbali, hali ni ya wasiwasi kati ya watia nia ambao walikuwa wabunge, walioomba kutetea nafasi zao, walioomba uchaguzi mkuu 2020 wakaenguliwa na vikao vya juu, na waliohamia CCM kutoka vyama vya upinzani.

Kwa kile kinachotokea majimboni, ni wazi baadhi ya watia nia presha inapanda na wengine inashuka, kutokana na taarifa wanazozipokea kuhusu vikao vya mchujo, ambavyo vimehitimisha kazi yake na matokeo kuwa ya siri.

Uchukuaji fomu za ubunge na udiwani ndani ya CCM ulianza Juni 28, 2025 hadi Julai 2, 2025.

Taarifa ya hivi karibuni ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla ilieleza watiania wa nafasi ya ubunge katika majimbo 272 ya Tanzania Bara na Zanzibar wako 4,109.

Makalla katika taarifa alisema waliochukua fomu kwa majimbo ya Tanzania Bara wako 3,585 na Zanzibar 524.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchujaji, walianza kujadiliwa na kamati za siasa za mikoa Julai 9 hadi Julai 10. Kamati hizo zimetoa mapendekezo ya kukata majina 3,293 na kubaki majina 816 yakiwa matatu kwa kila jimbo, kisha yatapelekwa kwenye Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Kamati Kuu itafanya kazi ya kuondoa majina 544 na kubakiza 272 ya ambao watakuwa wagombea wa CCM watakaochuana na wa vyama vingine vya upinzani.

Katika hatua nyingine, makada kadhaa wa CCM wakiwemo wa kamati za siasa za mkoa, wilaya, watia nia na wapambe wao wamehojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya rushwa.

Tuhuma hizo zimetolewa katika kipindi hiki cha mchujo ndani ya CCM kuwapata wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani.

Alipotafutwa na Mwananchi leo Julai 12, 2025, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo amethibitisha kuwapo tuhuma hizo za rushwa, akieleza ikiwa watuhumiwa watathibitika kuhusika na vitendo hivyo, watawafikisha katika mamlaka husika.

Bila kutaja majina na nafasi zao, Ndimbo amesema wamewahoji wajumbe wa kamati za siasa za mkoa, wilaya, watia nia na wapambe.

“Tunachokifanya kwa sasa ni kukusanya ushahidi kwa watuhumiwa wote ngazi ya mkoa ambao wanatajwa, wilaya, watia nia na wapambe wao. Takukuru kazi yake ni kuzuia vitendo hivi na tumejipanga kila kona,” amesema na kuongeza:

“Tunachotaka ni kuona wanaotia nia au kuchaguliwa wanakuwa wasafi ili kuwatumikia wananchi. Hatutaki kuona mtu anatumia vibaya nafasi yake kwa masilahi binafsi.”

Amesema: “Idadi tuliyonayo kwa sasa ni kama tisa hivi, japokuwa inaweza kuongezeka. Kamati za siasa wilaya watatu na watia nia pamoja na wapambe wao, tunaendelea kuwahoji juu ya tuhuma hizo na wakithibitika, hatua nyingine zitafuata.”

Ndimbo amesema taasisi hiyo inaendelea kufuatilia mwenendo mzima wa uchukuaji na urejeshaji fomu kwa vyama vyote, lakini pia mchujo unaoendelea kwa vyama vya siasa mkoani humo ili kuhakikisha haki inatendeka.

Related Posts