Askofu Malasusa: Dk Mono uwe Yusufu wa Mwanga

Mwanga. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa amemtaka  Askofu mteule  wa Dayosisi ya Mwanga, Dk Daniel Mono kuwa chombo cha kuunganisha watu na si chanzo cha migogoro na mifarakano.

Pia, amewataka viongozi wa kiroho kuacha kushughulika na mambo madogo yanayoweza kuwatoa kwenye mstari wa kiroho, badala yake waelekeze nguvu zao katika kazi kuu waliyotumwa na Mungu ya kuwachunga kondoo wake kwa hekima na upendo.

Dk Malasusa ametoa rai hiyo leo Jumapili Julai 13,2025 katika Kanisa Kuu la Mwanga, wakati akihubiri katika ibada ya kuwekwa wakfu na kumuingiza kazini Askofu Mteule wa Dayosisi ya Mwanga, Dk Daniel Mono.


Ibada hiyo imehudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na viongozi wengine wa chama, Serikali na dini mbalimbali.

Dk Mono alichaguliwa Machi 10, 2025 katika mkutano mkuu maalumu, baada ya askofu aliyekuwepo Chediel Sendoro kufariki kwa ajali, Septemba 9, 2024 iliyotokea katika eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Akihubiri Dk Malasusa amemtaka Askofu Mono kuwa mtu wa mazungumzo, mapatano, ujenzi wa mahusiano mema, kuwaunganisha watu na kuepuka kulipa kisasi.

Akitolea mfano wa Yusufu, Dk Malasusa amesema katika maisha watu hukutana na maumivu mengi lakini kama Mkristo, anapaswa kutenda mema  na kuepuka kulipa kisasi.

“Yusufu hakuwa na sababu yoyote ya kuwasaidia ndugu zake waliomuumiza, lakini alichagua kusamehe na kuwajali kwa sababu alimuangalia Mungu aliyemuweka katika jumba la kifalme. Yusufu ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wetu  kutenda mema licha ya historia za maumivu.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimia na viongozi mbalimbali wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kanisa kuu la Mwanga, wakati alipowasili kwa ajili ya kushiriki ibada ya kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini, Askofu Mteule wa Dayosisi ya Mwanga, Dk Daniel Mono.



Ameongeza kuwa; “Nikuombe baba Mteule uwe ni mtu wa kuhimiza upendo na amani, utulivu, mazungumzo, mapatano, mahusiano ndio kazi ya baba yule aliyekutuma kukalia kiti hiki. Usiwe mtu wa kisasi, kuwa mtu wa mazungumzo, mapatano na ujenzi wa mahusiano. Mungu anakutuma kama Yusufu wa Mwanga na si kuchochea bali kuunganisha.”

Amesema madaraka anayokabidhiwa kamwe yasimuondoe katika mstari, bali, “uwalete watu katika masikilizano, Mungu amekuita uwe Yusuph wa hapa Mwanga na  katika Kanisa letu la KKKT, lete amani na baba wa amani atakulinda na kukuongoza siku zote za maisha yako.”


Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwataka wachungaji na viongozi wengine wa dini kuacha kujiingiza katika mabishano na waumini au watu wengine na kuangalia lile kusudi la Mungu alilowaitia.

“Wachungaji wenzangu wakati mwingine tunahangaika na vitu vidogo sana, kuliko mambo makubwa ambayo Mungu ametupa, hasa kuchunga, kuelekeza hawa watu walio chini yetu. Leo tumuangalie Yusufu hakutaka kuhangaika na vitu vidogovidogo alihangaika na huyu aliye mkuu ambaye amemuweka katika jumba la kifalme,”amesema Malasusa.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi…

Related Posts