Askofu Mono: Mchakato wa katiba mpya uanze, ukamilike kwa wakati

Mwanga. Wakati Mkuu wa Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Daniel Mono akipongeza dhamira ya Rais, Samia Suluhu Hassan ya kuhuisha mchakato wa utekelezaji wa Katiba mpya, Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa amewataka viongozi wa kisiasa na Serikali kumuheshimu Mungu na kuwa watu wa ibada.

Amesisitiza kuwa msingi wa uongozi bora huanzia kwenye kumcha Mungu na kushikilia maadili ya kijamii na kiutamaduni.

Viongozi hao wameyasema hayo leo Jumapili Julai 13, 2025 katika Kanisa Kuu la KKKT Mwanga, wakati wa Ibada ya kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini kwa Askofu Mteule wa Dayosisi ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Dk Mono.


Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa baada ya kuwekwa wakfu, Askofu Dk Mono amewaomba Watanzania kuombea mchakato wa Katiba mpya uanze na kukamilika kwa wakati.

Amepongeza dhamira ya Rais Samia na Serikali ya kutaka kuanza kwa mchakato huo akisema, “nitumie nafasi hii kuipongeza nia ya Rais ya kuhuisha mchakato wa kuandika Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uamuzi huu una maana kubwa kwa Taifa letu, ni matarajio ya Watanzania wengi kwa kauli hiyo ya Rais, sasa Katiba mpya inaenda kuandikwa na haitaishia kuwa ahadi tena,” amesema Dk Mono.

Amesema kuandikwa kwa Katiba mpya kunakwenda kutatua changamoto nyingi za kiuongozi zinazolikabili Taifa na itaendana na mahitaji ya sasa ya nchi.

“Mimi binafsi na watu wote wenye mapenzi mema na nchi yetu, tunamuombea Rais na wasaidizi wake wote wakasimamie mchakato huu uanze na kukamilika kwa wakati,” amesema askofu huyo.

Aidha ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Watanzania kuliombea Taifa katika mwaka huu wa uchaguzi, ili haki na amani viendelee kutawala.

“Natoa wito kwa watu wote tuliombee taifa letu katika mwaka huu wa uchaguzi ili haki na amani vidumu na mapenzi ya Mungu pekee yatimie ili tupate viongozi watakaotuongoza kwa ustawi wa watu wote na si kwa masilahi yao binafsi,” amesema Dk Mono.


Wakati huohuo, Mkuu wa KKKT, Askofu Malasusa amesema viongozi wa kisiasa na Serikali wanapaswa kumuheshimu Mungu kwa kuwa watu wa ibada.

Amesema kufanya hivyo, kutawasaidia kufanya mambo yanayompendeza Mungu na jamii wanayoiongoza.

“Sina mashaka na Mkuu wetu wa Mkoa (Nurdin Babu,) kila Ijumaa humkosi msikitini. Na wengine wote endeleeni kupenda ibada. Kama unapenda uongozi, mpende Mungu pia ili akupe hekima ya kuwaongoza wanadamu,” amesisitiza Askofu Malasusa.

Amegusia pia hatari inayoweza kuikumba jamii iwapo misingi ya maadili itaendelea kuporomoka, akieleza kuwa katika kipindi cha miaka 20 ijayo, Taifa linaweza kukumbwa na kizazi cha lugha chafu, matusi, kutoheshimiana na chuki.

“Maadili hayana dini. Maadili ni utamaduni wetu kama Waafrika. Tukiyashika tutakuwa tunaendeleza Taifa lenye kupendana na kuheshimiana,” amesema Askofu Malasusa.

Akitoa salamu za Serikali katika Ibada hiyo, Majaliwa amewataka wananchi kupima na kutafakari ushawishi inapotolewa na wagombea na kuepuka kuliingiza Taifa katika hatari.

Majaliwa amesema katika kipindi hiki cha uchaguzi, mara nyingi wagombea huja na sera mbalimbali na wale watakaoleta zenye ushawishi wa kuliingiza Taifa katika hatari ya kuvunja amani, utulivu na mshikamano wanapaswa  kuwaepuka.

“Naomba Watanzania wenzangu tusikilize sera zao na ushawishi wao, lakini lazima tuwe makini katika kutafakari shawishi zote, shawishi ambazo Tanzania tunazikubali ni zile ambazo zinashawishi kutuletea maendeleo na sio zinazotuingiza katika hatari ya kubomoa tunu ya Taifa hili,” amesema Majaliwa.


Amesema tunu ya amani ni muhimu ndiyo maana Tanzania imekuwa kimbilio kwa nchi zilizokosa amani.

“Je, sisi tutaenda kukimbilia wapi? niwaambie panapoharibika amani na utulivu katika nchi tutasambaratika. Tukisambaratika wanaopata shida kwa kiasi kikubwa ni mama zetu na watoto wetu, tusiruhusu hilo,” amesema Majaliwa.

Amesema haki ya demokrasia kila Mtanzania kushiriki katika uchaguzi mkuu na serikali kama wadau wataendelea na jukumu la kusaidia ratiba hiyo ya uchaguzi na kuitangaza.

Pamoja na mambo mengine, Majaliwa amewaomba viongozi wa madhehebu yote ya dini nchini kuendelea kuliombea Taifa katika kudumisha amani, utulivu na mshikamano.

“Kwa viongozi wa dini, maaskofu, wachungaji, mashehe tusiache kuliombea Taifa letu, tunaamini kupitia maombi yenu lakini niwaombe, endeleeni kuombea viongozi mbalimbali wa nchi kwa sasa, muombeni  sana Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye  ndiye mkuu wa nchi na hata sisi ili tumsaidie vizuri,” amesisitiza Majaliwa.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini nchini katika nyanya mbalimbali ili kuimarisha ustawi wa wananchi wake.

“Ninachowahakikishia serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuimarisha ustawi wa wananchi wetu katika nyanja zote za utoaji wa huduma huku tukisimamia uwepo wa amani, upendo na utulivu katika jamii,” amesema Majaliwa.

Related Posts