AYE kupeleka vijana Marekani kupitia ufadhili wa masomo

KATIKA hatua ya kuibua na kukuza vipaji vya vijana wa Kitanzania, taasisi ya African Youth Empowerment (AYE) imetangaza kuanza rasmi mpango wa kutoa ufadhili wa masomo (scholarship) kwa vijana wenye vipaji maalum kwa ajili ya kusoma na kuendeleza ndoto zao nchini Marekani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi Mtendaji wa AYE, Muyimba Gerald amesema kuwa mpango huo ni sehemu ya dira ya taasisi hiyo ya kuhakikisha vijana kutoka familia za kawaida wanapata nafasi ya kujieleza kitaaluma na kiubunifu katika majukwaa ya kimataifa.

“Tumeanzisha rasmi mpango wa scholarship kwa vijana wa Kitanzania ambao wana vipaji vya pekee katika nyanja mbalimbali kama vile sanaa, michezo, teknolojia, sayansi, na uongozi. Lengo ni kuwasaidia kufikia fursa za kimataifa, hasa nchini Marekani ambako mazingira ya kukuza ndoto zao yako wazi zaidi,” alisema Muyimba.

Kwa mujibu wa Gerald, vijana watakaonufaika na mpango huu watapata nafasi ya kusoma katika shule na vyuo mbalimbali vya Marekani, huku taasisi hiyo ikihusika moja kwa moja katika maandalizi ya nyaraka, maombi ya visa, ushauri wa kitaaluma na uratibu wa usafiri.

“Tunafanya kazi bega kwa bega na taasisi za Marekani ambazo zimekubali kuwakaribisha vijana wetu. Tunapima zaidi uzalendo, maadili, na uwezo wa kijana kuleta mabadiliko chanya katika jamii anayotoka,” alisisitiza.

Mpango huu unatarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia Septemba 2025 ambapo kundi la kwanza la vijana litachaguliwa kupitia mchakato wa wazi, wenye vigezo vya kitaaluma na vipaji halisi.

Related Posts