Dar es Salaam. Baada ya kukamilika kwa vikao vya wilayani na mikoani, hatimaye Chama cha Mapinduzi (CCM), kinaingia rasmi kwenye wiki ya mtihani na uamuzi mgumu kwa ustawi na uhai wake.
Ni mtihani na uamuzi mgumu kwa sababu, ndiyo unaoamua majina yapi yatemwe na matatu yarudishwe kwa wajumbe kupigiwa kura za maoni, kwa wale walioomba kupeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi za ubunge, udiwani sambamba na viti maalumu.
Ugumu unatokana na kwamba, ndio uamuzi ambao aghalabu unaweza kuleta mpasuko au wagombea wasiokubalika na hatimaye chama hicho ama kupata ushindi mwembamba au kuanguka katika baadhi ya majimbo.
Inabaki kuwa wiki ngumu hasa ukizingatia, tayari kumeibuka tetesi za majina ya baadhi ya wanasiasa wakongwe kukatwa, wakiwamo wabunge wa zamani na hata walioacha nyadhifa za uteuzi na kuomba ridhaa ya kuwania ubunge.
Katikati ya yote hayo, yapo madai ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika baadhi ya majimbo, watiania wakijaribu mbinu za hapa na pale kuvishawishi vikao viamue mambo yenye masilahi kwa upande wao.
Hayo yanakuja, wakati Julai 17, mwaka huu Kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kitakaa, kupokea na kuchambua majina ya wagombea ubunge na ujumbe wa baraza la wawakilishi wa jimbo na viti maalumu kwa ajili ya maandalizi ya vikao vya uteuzi.
Wakati hali ikiwa hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa, wanasema haki ndiyo silaha pekee itakayoiwezesha CCM kuvuka salama katika kipindi hiki.
Hata hivyo, tayari kumeibuka hoja kuwa, pengine mchakato huo ukasababisha mpasuko ndani ya chama hicho, kutokana na madai ya baadhi ya waliopitishwa wanatuhumiwa kutumia rushwa.
Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Aviti Mushi anadai haoni kama kutakuwa na mpasuko kwa sababu, hakuna jukwaa mbadala ambalo wanasiasa hao watakimbilia.
Amesema mpasuko ulitokea katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 ulitokana na walioshindwa kupenya ndani ya CCM, waliamua kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), lakini kwa sasa hawana nafasi nyingine kwa kuwa chama hicho kimepoteza nguvu.
Amesema kwa sasa haoni chama kingine kinachoweza kuwa mbadala wa Chadema kinachoweza kuwavutia makada hao kutimkia huko.
“Hakutakuwa na mpasuko tena, ingawa kutakuwa na maneno maneno tu…atakayekatwa inapaswa atulie na kumuunga mkono aliyepitishwa, maana kule walikokuwa wakikimbilia sasa hivi nguvu zimepungua.
“Sidhani kama sasa hivi kuna kundi kubwa ambalo lina nguvu linaloshindana na uongozi wa sasa, kwa namna walivyokisuka chama chao. Majina yatakwenda na kurudi hata kama wengine wataachwa hawataleta madhara,” amesema.
Kuhusu kupata wagombea bora, Dk Mushi amesema hadhani kama watakuwa wazuri au wabaya kulingana na waliogombea ila watatoka katika mfumo huohuo ingawa wengine watakuwa bora zaidi kuliko wenzao.
“Aliyejiweka vizuri ndio atakayepitishwa sitegemei kama kutakuwa na maajabu makubwa…,” amesema Dk Mushi.
Wakati Dk Mushi akieleza hayo, mchambuzi mwingine wa siasa, Dk George Kahangwa amesema michakato ya namna hiyo kwa Taifa linaloendelea inatakiwa ifanyike kwa uwazi ili watu wajue vigezo na hilo ndilo litakaloiweka CCM salama.
“Kwa sababu anayepitishwa na kushinda ubunge au udiwani ndiye anakuja kuwa kiongozi atakayewawakilisha wananchi wa eneo husika. Ni vema makatibu wa vyama vya siasa na si CCM pekee, bali na vyama vingine vikaweka wazi vigezo wanavyovitumia kupitisha watiania,” amesisitiza.
Amesema kwa kufanya hivyo, kutaondoa hisia za kuwepo kwa mchezo mchafu na mpasuko ndani ya chama husika.
Dk Kahangwa ambaye ni Mhadhiri wa UDSM, ameshauri vyama vya siasa kuachana na utaratibu wa kutumia hisia bali kuweka vigezo.
“Makatibu wakuu wa vyama vya siasa watusaidie mambo yawe wazi, kama wanavyofanya wakati wagombea wanapochukua fomu na kupiga picha,” amesema.
Hata hivyo, akizungumza leo Jumapili Julai 13, 2025 na vyombo vya habari jijini Dodoma, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema vikao vinavyotoa maoni vimefanyika katika ngazi ya kata, Kamati za Siasa za Wilaya na Kamati za Siasa za Mkoa.
“Hapa makao makuu vikao vya ngazi ya kitaifa vimeanza rasmi, zoezi hili limeahimia katika makao makuu, leo tumeanza na sektarieti ya Chama cha Mapinduzi kwa maana ya kupokea taarifa kutoka katika mikoa mbalimbali ambayo wameshawasilisha taarifa,”amesema Makalla.
Lakini amewaomba watiania katika nafasi mbalimbali kuwa watulivu kwa kuwa vikao vimeshafanyika wilayani na mikoani na wanapokea taarifa hizo.
“Kubwa wawe watulivu hadi pale Kamati Kuu itakapotoa uamuzi wa mwisho. Kwa utaratibu wetu na mchakato ndani ya chama, hakuna mtu ambaye ameenguliwa au kukatwa,” amesema Makalla.
“Nimeona huyu kafyekwa huyu hayumo katika tatu bora. Naomba mtupelekee ujumbe hakuna aliyeenguliwa, aliyekatwa hakuna aliyefyekwa wote huo ni mchakato unaoendelea katika chama chetu.”
Mwenezi huyo amesema wanachama walioomba nafasi hizo ni wengi na wote wanania nzuri, lakini kwa sababu nafasi ni chache, wachache watateuliwa kulingana na nafasi zilizopo.
Amesema watakaokosa nafasi wanaamini kwa uzalendo na mapenzi yao kwa chama, wataendelea kuwa watulivu ndani ya chama hicho na kuendelea kuhakikisha hata baada ya kura za maoni kupita na kupatikana kwa wagombea, wataendelea kuwa wanachama watiifu kwa chama chao cha Mapinduzi.
Wabunge waliokaa muda mrefu
Katika maoni yake, Dk Kahangwa amegusia suala la wabunge kukaa muda mrefu kwa zaidi ya miaka 20, akishauri ifike mahali wakubali kwamba, hawawezi kukaa nafasi hiyo milele.
Amesema kama mbunge au diwani ametumikia nafasi hiyo kwa miaka 20, awapishe na wengine wenye nia na si lazima akalie nafasi hiyo milele.
Mchambuzi huyo amesema ifike mahali Taifa au chama kiweke ukomo wa ubunge na udiwani kwa sababu wengine wakienguliwa wanahisi wameonewa kwa sababu tu, ameshazoea kuitwa ‘mbunge’ au ‘diwani.’
Amesisitiza lazima haki itendeke katika mchakato huo na kama mtu ameonewa, chama kiruhusu utaratibu wa kukataa rufaa ili anayedai kuonewa awe na sehemu ya kukimbilia badala ya kubakia na dukuduku linalozalisha chuki na makundi yanayoweza kuchochea mpasuko.
Baadhi ya watiania ya ubunge wanaodaiwa kukatwa waliozungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina kutoka maeneo tofauti, wamedai kuchezewa rafu kubwa wakati wa mchakato wa awali.
“Mimi kwenye jimbo letu, tumetia nia watu 14, lakini haya majina tuliyoambiwa ndiyo yamepitishwa hatujaridhika, tumeshaandaa barua ya kupeleka kwa makamu mwenyekiti wetu na tutapeleka nakala kwa mwenyekiti, tusiporidhishwa na majibu, tutatafuta njia mbadala ya kufanya,” amesema.
Mwananchi pia imezungumza na baadhi ya watiania wa udiwani ambao kwa nyakati tofauti wamekiri hali kuwa mbaya na presha kubwa wakati huu wakisubiria kurejeshwa kwa majina matatu yaliyopendekezwa.
“Kwanza sijui kama nipo au sipo katika tatu bora kuanzia mapendekezo yaliyofanyika katika ngazi ya wilaya hadi mkoa kupitia vikao mbalimbali,” amesema mmoja wa watiania.
Mwingine amesema,”kila mmoja hivi sasa anaangaika kujua nani amerudi au kutorudi, hali hii itategemea mahusiano yaliyopo miongoni mwa viongozi wa CCM.
“Usiri mkubwa sana umeghubikwa kwa watiania wanaotaka kujua yumo au hayumo ndio maana kumekuwa na pilikapilika za hapa na pale za wagombea kutaka kujua yupo katika ngazi gani kabla ya majina kurejeshwa,” amesema mtiania huyo.
Nyongeza na Sharon Sauwa, Mwananchi – Dodoma