Chanzo watumishi wa afya kuvikimbia vituo  

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kupeleka watumishi wa afya mikoa ya pembezoni mwa nchi, baadhi huondoka hivyo wachache wanaobaki kubeba mzigo mkubwa wa kazi.

Miongoni mwa sababu zinazowakimbiza watumishi hao ni mazingira duni ya kazi na changamoto za miundombinu.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika baadhi ya zahanati za Mkoa wa Kigoma ulio pembeoni mwa nchi zikiwamo za Muhunga na Kitagala wilayani Kasulu, Kalalangabo iliyo umbali wa kilomita tisa kutoka Kigoma Mjini na Simbo iliyopo Kigoma Vijijini umebaini zina watumishi wawili kila moja wanaosaidiwa na watumishi wa afya ngazi ya jamii. Kituo cha Afya Bunyambo wilayani Kibondo kina watumishi sita.

Hali hii ya uchache wa watumishi husababisha wananchi kuchukua muda mrefu kupata huduma, moja ya zahanati ikianzisha huduma ya uji wa lishe kwa watoto siku wanapopelekwa kliniki. 

Mwongozo wa upangaji wa rasilimali watu kwa vituo vya kutolea huduma za afya wa mwaka 2014 uliotolewa na Wizara ya Afya unapendekeza kwa ngazi ya zahanati wawepo watu tisa ambao ni ofisa tabibu, muuguzi, mtalaamu wa afya ya uzazi (mkunga), wahudumu wa afya waliosajiliwa wawili, mtaalamu msaidizi wa maabara, ofisa afya na mazingira, mtakwimu na mtu anayehusika na usafi na ulinzi.

Mbali na huo, Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya awamu ya tano (Julai

2021 – Juni 2026) unazungumzia kuhusu uendelezwaji wa mifumo ya upangaji rasilimali watu katika sekta ya afya (HRH) kwa kuzingatia takwimu na uhalisia ili kuwezesha uwiano kati ya mahitaji, upatikanaji na uhitaji.

Mkakati pia, unazungumzia upangaji watumishi kwa kuzingatia mzigo wa kazi na mahitaji ya wagonjwa.


 

Katibu wa Afya, Ofisi ya Mganga Mkuu Mkoa wa Kigoma, Estomohi Ulomi anasema kuna upungufu wa wataalamu wa afya kwa asilimia 40 katika mkoa huo.

“Changamoto ya uhaba wa watumishi ipo. Tunaendelea kupanga wale waliopo kadri vituo vipya vinavyoanzishwa. Pia, kuna mabadiliko ya uhamisho wa watumishi kutokana na sababu mbalimbali kama za kifamilia au mahitaji ya kada husika,” anasema.

Anasema tatizo ni kubwa kwa sababu baadhi ya maeneo hayana miundombinu rafiki kwa maisha ya kawaida ya mtumishi.

“Kituo kinajengwa lakini hakuna nyumba ya mtumishi. Sasa mtu anaona hawezi kuishi eneo hilo,” anasema.

Ulomi anasema motisha kwa watumishi wa afya ni tofauti katika maeneo mbalimbali ili kuwafanya watumishi wabaki vituoni.

“Wapo wanaojengewa nyumba, wengine hupatiwa viwanja au malazi bure, huku baadhi wakilipiwa ada za masomo wanapoamua kujiendeleza kitaaluma. Haya yote yanalenga kuwahamasisha watumishi kubaki katika vituo vyao vya kazi,” anasema.

Hata hivyo, anasema wapo wanafunzi walioko kwenye hospitali za mafunzo wanaosaidia kupunguza uhaba kwa muda.

“Kwa sasa, Serikali inaendelea na mchakato wa kuongeza vituo vya afya na kuboresha huduma. Hata hivyo, mafanikio haya hayawezi kuonekana kikamilifu bila kuwapo rasilimali watu ya kutosha,” anasema.


Muuguzi katika Zahanati ya Muhunga, wilayani Kasulu mkoani Kigoma, Idrissa Bondo anasema huhudumia wananchi wengi kwa siku.

Machi 17, 2025 katika zahanati hiyo saa 8:00 mchana, Mwananchi ilishuhudia kina mama wengi wenye watoto wakiwa kliniki.

Katika zahanati hiyo palikuwa na sufuria kubwa la uji wa lishe uliokuwa ukigawiwa kwa watoto wakati wakisubiri huduma kutoka kwa watumishi wawili pekee waliopo.

“Hapa tupo wawili, kijiji hiki kina wakazi zaidi ya 14,000 tukiangalia kwa mgawanyiko ni wananchi wengi, kwa mwezi tunahudumia wagonjwa 200 hadi 300,” anasema.

Kwa mujibu wa Bondo hufanya kazi tangu asubuhi na ifikapo saa 9:30 alasiri hugawana majukumu na mwenzake kwa kuwa pia hutoa huduma za dharura zinapotokea.

Anasema uhudumia wajawazito 80 hadi 120 kwa siku wanapotoa huduma ya kliniki kuanzia asubuhi mpaka saa 10 jioni. Miongoni mwa hao wamo wajawazito takribani 45 wanaoanza huduma za kliniki.

“Wanaojifungua hapa ni wenye ujauzito wa pili hadi wa nne, wale wa mara ya kwanza na mimba ya tano kuendelea mwongozo wa wizara unataka wakajifungulie sehemu ambayo kuna huduma za kutosha kama za damu na huduma za upasuaji,” anasema.

Si hivyo pekee, anasema huwa pia wanakwenda kutoa huduma maeneo mengine (Mkoba) lakini kuna wakati inawawia vigumu. Kutokana na mazingira hayo ya kazi anasema huwa ngumu kupumzika.

“Muda wa kupumzika haupo, hamuwezi kutoka hapa kijijini labda atoke mmoja mwingine abaki. Tuna vijiji vitatu vipo mbali kidogo Katyazo, Nyandura na Lugongo umbali ni kuanzia kilomita tatu hadi mpaka nne,” anasema.

Mbali na hayo, anasema kila mwezi huwa wanatoa huduma za chanjo kwa wajawazito, chanjo shuleni na elimu ya afya, vilevile hufanya ukaguzi wa mazingira, vyoo na huduma za uzazi wa mpango.

Bondo ambaye yupo katika zahanati hiyo tangu mwaka 2023 anasema alipofika walikuwa watumishi watatu, mmoja akahamia Geita, mwingine aliondoka na sasa wapo wawili.

Anasema Machi, 2025 kuna mtumishi alipangwa kufanya kazi katika zahanati hiyo lakini hakuripoti kazini.

Bishaza Mchape, mtumishi wa afya ngazi ya jamii wilayani Kasulu, anasema wamekuwa wakitoa huduma kwa wananchi na kuna nyakati huwasaidia watumishi wa afya vituoni kutoa huduma kwenye kliniki za watoto na wajawazito ili kuwapunguzia mzigo wa kazi.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Vumilia Simbeye anakiri kuwapo uhaba wa watumishi wa idara ya afya, lakini anasema Desemba, 2024 Mkoa wa Kigoma ulipata watumishi walioajiriwa kwenye vituo vya afya.

“Tuliwasambaza katika vituo vya afya 23 na tuna zahanati zipo nyingi pia tuliwasambaza, bado tunafanya juhudi kuandaa mikakati kuona nini tunaweza kufanya. Kuna zahanati nyingine ina upungufu, wengine wana zaidi kidogo lakini bado tunaona kulingana na huduma zinazotolewa bado tuna uhitaji zaidi,” anasema.

Kuhusu watumishi wanaopangwa kuondoka anasema mtumishi mpya akiajiriwa lazima athibitishwe kazini ndani ya mwaka mmoja.

Anatoa mfano wa mtumishi aliyempelekea barua ya kutaka kuhama akiwa mjamzito. Mtumishi huyo alitakiwa kuripoti Desemba pamoja na wenzake lakini hakufanya hivyo, akaripoti Januari, 2025.

“Amefika anaomba likizo ya uzazi, ameruhusiwa baada ya muda amemtuma ndugu yake ameandika barua anaomba kuhamia Muhas hata miezi sita hajafanya kazi ina maana hata muda wa kithibitishwa hakukaa na angetimiza mwaka na kuonekana anafaa angepata namba ya mshahara,” anasema.

Anasema hiyo ni tabia ya watumishi wengi wa ajira mpya na kuongeza: “Uhamisho upo kwenye mfumo sasa nikipitisha barua ina maana angekuwa ameshaondoka lakini salama yake ya kazi ingekuwaje huko anakokwenda? hivyo sikuruhusu.”


Waziri wa Afya, Jenista Mhagama akiwasilisha bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2025/26 alisema wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo itaendelea kuweka mazingira mazuri na yenye kuvutia kwa watumishi wa sekta ya afya ili kuwabakiza watumishi katika maeneo yao ya kazi.

Waziri alisema wizara inaendelea kuwakumbusha waajiri kuweka mazingira mazuri yatakayowavutia na kuwabakiza watumishi wa sekta ya afya kama vile kujenga nyumba za makazi karibu na maeneo ya kutolea huduma.

Pia, kununua vyombo vya usafiri kwa ajili ya kuwahudumia watumishi, kuendelea kutoa posho ya saa za ziada na posho za kuitwa kazini, kutoa mikopo kwa watumishi wa afya na kuwaendeleza ili wabaki katika maeneo yao kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi. 

Jenista alisema Julai 2024 hadi Machi 2025, Serikali imeajiri watumishi 13,564 katika sekta ya afya na kufanya jumla yao kufikia 177,711.

Ongezeko hilo alisema limepunguza upungufu wa watumishi wa sekta ya afya kutoka asilimia 64 hadi kufikia asilimia 55 ya mahitaji ya watumishi wote 391,950 wanaohitajika katika sekta hiyo.

Alisema kati ya watumishi waliopo, 136,739 sawa na asilimia 77 wapo katika ngazi ya afya ya msingi na watumishi 33,765 sawa na asilimia 19 wanafanya kazi katika ngazi ya hospitali za rufaa za mikoa na kanda, hospitali maalumu za rufaa na Hospitali ya Taifa.

Waziri alisema asilimia nne ya watumishi wapo katika mashirika na taasisi.

Alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika sekta ya afya imeendelea kutoa ajira za mikataba ili kukabiliana na upungufu wa watumishi uliopo.

Katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, alisema wataalamu 8,146 waliajiriwa kupitia utaratibu huo kwa ajili ya kufanya kazi kwenye vituo vya kutolea huduma.

Katika kuhakikisha uwepo wa wataalamu wa kutosha, kwa uwiano sahihi na wanaotoa huduma zilizo bora za afya kwa wananchi; alisema wizara inasimamia vyuo vyote vya mafunzo vya kada za kati vinavyomilikiwa na Serikali, taasisi za dini na watu binafsi ili kuhakikisha vinazalisha wataalamu wenye ujuzi na weledi.

Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, ilifanya uchaguzi wa wanafunzi 33,353 sawa na asilimia 36 ya waombaji 92,820 waliotuma maombi ya kujiunga na vyuo vya afya ngazi ya kati.

Alisema kati yao wanafunzi 3,209 sawa na asilimia 10 walichaguliwa kujiunga na vyuo vya Serikali na wanafunzi 30,144 sawa na asilimia 90 walichaguliwa kujiunga na vyuo vinavyomilikiwa na watu binafsi na taasisi za dini katika programu za Sayansi Shirikishi za Afya, Uuguzi na Ukunga.

Jenista alisema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025 watalaamu 17,850 wamehitimu katika fani mbalimbali za kada za kati za afya ikilinganishwa na wataalamu 15,475 katika kipindi hicho kwa mwaka 2024.

Wahitimu ngazi ya shahada kwa kipindi hicho ni 5,415 ikilinganishwa na wataalam 2,891 katika kipindi hicho kwa mwaka 2023. Vilevile, wahitimu wa ngazi ya Shahada ya Uzamili wameongezeka kutoka 540 mwaka 2023 hadi kufikia 889 mwaka 2024.

Rehema Jongu, mkazi wa Kijiji cha Nyandura wilayani Kasulu anasema hutumia siku nzima akipeleka watoto wake kliniki kwenye zahanati iliyopo umbali wa kilomita nne kutoka kijiji anachoishi.

“Pale Muhunga (zahanati) kuna watumishi wawili pekee, tunajikuta kinamama na watoto ni wengi mnashinda pale siku nzima na ndiyo maana wanalazimika kupika uji wa lishe kwa ajili ya watoto,” anasema Rehema.

“Zamani licha ya kufuata huduma umbali mrefu, Bunyambo hapakuwa na watoa huduma kabisa. Walikuja watatu kutoka Halmashauri ya Kibondo ambao saa sita mchana waliondoka. Kwa wiki walikuja mara moja au mbili,” anasema James Simbu, mkazi wa Kata ya Bunyambo na kuongeza:

“Tuna miezi miwili sasa wamejiriwa watumishi wa afya sita, lakini hakuna daktari, ina maana licha ya kwamba kuna vifaa vyote lakini bado hawafanyi upasuaji.”

Katika Zahanati ya Kitagata kuna watumishi wawili. Aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Sabasi Matabura anasema:

“Katika vikao vyetu vya halmashauri zahanati inatakiwa kuwa na watumishi angalau watatu. Hapa kuna wawili pekee. Hali hii inasababisha mzigo mkubwa kwa watumishi hao wachache, ambao hulazimika kufanya kazi zaidi ya majukumu yao.”

Aliyekuwa Diwani wa Muhunga, Suku Leonard anasema kata hiyo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi akieleza wawili waliopo hawatoshelezi mahitaji.

“Tunafahamu lengo la Serikali ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Ni vema ikaangalia namna ya kuleta watumishi katika kata zilizopo pembezoni, kuna umbali mkubwa kutoka Muhunga kuja mjini kufuata huduma,” anasema.

Imeandikwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Gates Foundation

Related Posts