MASHABIKI wa Yanga wana uhakika wa kutamba sasa, baada ya klabu yao kujihakikishia dili la kumnasa mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Celestin Ecua ambaye atasaini mkataba wa miaka miwili na timu hiyo.
Uhakika wa Yanga unatokana na bosi wao injinia Hersi Said kufanya umafia kuiwahi saini ya mshambuliaji huyo mwenye kasi akimalizana na klabu yake.
Yanga imemalizana na Zoman, iliyokuwa inammiliki Ecua, ambaye msimu uliopita, alifanya balaa akiwa na ASEC Mimosas kwa mkopo.
Ecua ndiye Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu ya Ivory Coast akifunga mabao 15 na asisti 12, ataungana na staa aliyewahi kubeba tuzo kama hiyo nchini humo, anayeitumikia Yanga, Pacome Zouzoua.
Awali Simba ndio walikuwa wa kwanza kupigania saini ya mshambuliaji huyo, kabla ya Yanga kuingilia kati na kufanya mambo fasta wakiwatibulia watani wao hao.
Awali dili hilo liliingia utata kwa mawakala kupishana lakini hata hivyo, Zoman imewasaidia Yanga kujiepusha na kufunguliwa kesi Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ikiwaweka sawa na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara kumaliza kila kitu.
Kwa sasa Yanga inaandaa mkataba wa miaka miwili wa kumpa mshambuliaji huyo, ambaye tayari Mwanaspoti linafahamu Hersi alishapitisha mkataba wa awali kimafia kwa Ecua.
Ecua bado yupo nchini Ivory Coast na Yanga ilitaka kumleta nchini mapema wikiendi hii lakini akaomba muda apone sawasawa malaria yanayomsumbua kisha aje nchini kusaini mkataba kamili.
Simba haikukata tamaa kirahisi, Mwanaspoti linafahamu juzi, ilirudi kwa nguvu kwa Zoman lakini wekundu hao wakajibiwa Yanga imeshamaliza biashara.
Kampuni ya Wa Football Agency inayomsimamia Ecua katika masuala yake ya kimkataba, imethibitisha kufanyika kwa dili hilo.
“Rasmi baada ya mazungumzo marefu na majadiliano makali, mchezaji wetu Ecua Celestin amesajiliwa rasmi na Yanga SC.
“Ukurasa mpya unaanza katika moja ya klabu maarufu zaidi Afrika Mashariki. Mkataba huo sasa umekamilika, na mchezaji huyo atasafiri kwenda Tanzania hivi karibuni kujiunga na timu yake mpya.
“Asante kwa pande zote zinazohusika katika kufanikisha hatua hii kabambe. Songa mbele kwa changamoto mpya!” Ilieleza taarifa ya wasimamizi hao wa Ecua.
Mbali na wakala kuthibitisha, pia mchezaji mwenyewe kwenye utambulisho wake wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Instagram, ameiweka Yanga ndiyo timu mpya kwake.
Ujio wa Ecua Yanga, moja kwa moja anakwenda kuchukua nafasi ya mshambuliaji Kennedy Musonda ambaye tayari ameondoka kikosini hapo na kutua Israel baada ya mkataba wake kumalizika.
Pia usajili huo utaongeza nguvu eneo la ushambuliaji la Yanga huku kukiwa na taarifa za kinara wa mabao kikosini hapo katika Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika, Clement Mzize yupo njiani kutimka baada ya ofa kibao kutua Yanga.
Endapo Mzize aliyefunga mabao 14 ataondoka, Ecua atakuwa na kazi kubwa ya kufanya kwa kushirikiana na Prince Dube aliyemaliza ligi na mabao 13 kuendelea kuibeba Yanga kutetea mataji ya ndani iliyochukua ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la Muungano, huku pia kuifikisha mbali timu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.