Jinsi ‘power bank’, chaja zinavyoweza kuharibu simu yako

Dar es Salaam. Umewahi kujiuliza kwa nini unaweza kutumia chaja ya simu uliyonunua au ‘power bank’ halafu baada ya muda ikaharibu betri ya simu yako kwa kupunguza ufanisi ikiwemo kutokaa na chaji tena kwa muda mrefu?

Mwandishi wa habari hii anakupa majibu na nini cha kufanya kuepuka hilo kutoka vyanzo mbalimbali hususan vilivyobobea kwenye teknolojia. Ingawa mbali ya chaja na kifaa hicho cha kuhifadhi chaji kwa muda mrefu ‘power bank’, tuangalie kwanza sababu nyingine zinazoweza kuharibu betri ya simu yako.

Kimsingi kuharibika kwa betri ya simu hasa zile za Lithium-ion, kunatokana na muda wake na jinsi unavyoitumia.

Hata hivyo, kuna baadhi ya sababu kama vile joto ikiwemo kuacha simu kwenye jua kali, ndani ya gari lililoegeshwa juani, au kuichaji ikiwa katika eneo lenye joto sana kunaweza kusababisha madhara ya kudumu kwa uwezo wake wa kuhifadhi chaji.

Betri inapokuwa ya moto sana, zile kemikali ndani yake huharibika, na kufanya ipoteze uwezo. Joto linaathiri volti ya betri kadri joto linavyoongezeka, ndivyo volti inavyopungua. Hii husababisha betri kutoa nguvu kidogo na kupunguza uwezo.

Mawimbi ya joto yanaweza kusababisha betri kutoa gesi ya hidrojeni na oksijeni. Gesi hizi ni hatari kwa kuwa ni rahisi kuwaka, na zinaweza kusababisha betri kuvimba au kulipuka.

Kwa mujibu wa Texford Battery unapaswa kuepuka kuchaji kupita kiasi huongeza joto na kuharibu betri. Unapaswa kusoma mwongozo wa chaja ili ujue muda sahihi wa kuchaji na epuka kutumia chaja ambazo hazilingani.

Aidha, sababu nyingine inayoweza kuharibu betri ni kuchaji huku unatumia simu: Kucheza gemu au kutazama video ukiwa unachaji kunaweza kuzalisha joto jingi na kuweka mkazo mkubwa kwenye betri, hivyo kusababisha madhara.

Sababu nyingine ni uwepo wa programu zinazoendelea kuwa wazi bila ya wewe kujua (background apps) kama vile mitandao ya kijamii, (GPS) mara nyingi hula chaji nyingi bila wewe kujua.

Mwanga mkali ni miongoni mwa sababu kwani skrini ndiyo sehemu inayotumia nguvu nyingi zaidi kwenye simu. Kuweka mwangaza wa skrini mkubwa kwa muda mrefu kutamaliza chaji haraka na kuweka betri katika hali ya kufanya kazi zaidi.

Pia, kitendo cha kuwa na arifa nyingi (notification) vilevile zinaongeza matumizi ya betri. Pia kudondosha simu kunaweza kusababisha uharibifu wa ndani kwa betri au saketi za kuchaji.

Vilevile, mtandao unapokuwa chini (network) simu inapotafuta mawimbi ya mtandao mara kwa mara hutumia nguvu nyingi zaidi ya betri.

Betri zote za Lithium-ion hupoteza uwezo wake wa kuhifadhi chaji kadiri muda unavyokwenda. Baada ya miaka miwili hadi mitatu ya matumizi, ni kawaida kwa betri kupoteza kiasi fulani cha uwezo wake wa awali.

Turudi kwenye matumizi ya chaja isiyofaa, imeelezwa kutumia chaja isiyo halisi au zenye ubora wa chini kunaweza kutoa voltage au mkondo usio sahihi, na hivyo kuharibu betri au hata simu yenyewe.

Unapaswa daima utumie chaja halisi au chaja zenye vyeti vya usalama kutoka kwa kampuni zinazotambulika.

Matumizi ya ‘power bank’

Ingawa ni kifaa muhimu kwa kuwa kinasaidia  wanaokuwa mbali na umeme, ila unapoinunua lazima uzingatie baadhi ya vitu ili kuipa uhai betri yako.

Jambo la kwanza unapaswa kuzingatia voltage (presha kutoka kwenye umeme ambayo husukuma elektroni zilizochajiwa), mara nyingi simu za sasa voltage yake ni tano.

Hata hivyo, baadhi ya simu zinahitaji voltage ya juu zaidi. Lakini, si ‘power banks’ zote zinazendana na voltage za simu. Ikiwa voltage inayotolewa na ‘power bank’ ni ndogo, haitaweza kuchaji simu yako.

Kwa hivyo, kabla ya kuinunua ni muhimu kuangalia voltage ya chaja ya kifaa chako na voltage ya ‘power bank’, ili kuhakikisha kuwa zinaendana.

Jambo lingine la kuangalia ni uwezo wa kuchaji kwani ‘Power bank’ inapaswa kuchaji simu yako kikamilifu kutoka sifuri hadi asilimia 100. Ili kuhakikisha hili, unapaswa kuangalia uwezo wa simu yako ambapo itakuwa katika milliamperes-hour (au mAh).

Kisha, ni bora kuchukua ‘power bank’ yenye uwezo mara mbili, ikiwezekana mara tatu ya ule wa simu yako. Kwa mfano, kwa simu yenye 4,000 mAh, ni bora kutafuta ‘power bank’ yenye uwezo wa angalau 8,000 mAh.

Hatari nyingine ya usalama inaweza kuwa aina ya betri iliyowekwa kwenye ‘power bank’. Baadhi hususan za bei ya chini zinaweza kuwa na seli za betri za ubora duni, ambazo zina uwezekano mkubwa wa kuvuja, au hata kuhatarisha mlipuko.

Ili kuhakikisha usalama, tafuta ‘power bank’ yenye seli ya Lithium Polymer au Lithium Ion, ingawa zenye betri hizi zinaweza kuwa ghali kutokana na ubora wake

Vilevile yapo mambo ya kuzingatia unaponunua chaja ya simu yako kwani baadhi ya watu hudhani chaja zote ni sawa.

Kwanza hakikisha kiunganishi cha chaja kinalingana na tundu la kuchaji la simu yako. Aina zinazotumika sana kwa sasa ni zile za USB-C: ambayo inatumiwa na simu nyingi mpya za Android na iPhone (tangu iPhone 15). Hii inaweza kuingizwa pande zote mbili na inasaidia kuchaji kwa kasi zaidi.

Pia unaponunua chaja lazima uelewe kwamba si chaja zote zinatoa umeme kwa kiwango sawa. Angalia wati (W) kwenye chaja ikiwa kubwa kwa ujumla inamaanisha kuchaji kwa kasi zaidi. Mara nyingi huwa wati tano hadi 10.

Unaponunua chaja hasa zile za haraka (fast charger) ingawa simu za kisasa zinakubali, USB Power Delivery (PD), Qualcomm Quick Charge) ambapo zina chaja kuanzia 18W hadi 100W au zaidi.

Lazima uangalie vipimo vya simu yako: Tafuta ni wati ngapi za juu simu yako inaweza kukubali. Kununua chaja ya 60W kwa simu inayotakiwa 20W tu haitafanya ichaji haraka zaidi.

Unaponunua chaja pia angali alama za usalama kama vile CE, FCC, UL, au za nchi yako. Hizi zinaonyesha chaja imekidhi viwango fulani vya usalama.

Akizungumza na Mwananchi mfanyabiashara wa simu kutoka Kariakoo jijini Dar es Salaam,  Gutu Google Pixel Tz, anasema chaja zina watt zake na simu.

“Simu inatumia watts 18 hadi watts 25 hata kebo yenye 5A waya unaopokea ukizidisha hapo unaua betri miezi miwili tu unashangaa utendaji wake unapungua,” amesema.

Anasema kwa upande wa Power bank nikifaa kimewekwa kwa kutumia kwa dharua. Anasema endapo simu imezima chaji kabisa ukatumia power bank kuchaji hadi iwake pale inatumia nguvu na inapelekea kuuwa nguvu ya betri.

Related Posts