Jukwaa la wakurugenzi wakuu kuchochea mabadiliko biashara, uchumi

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wakurugenzi Wakuu wa Kampuni Tanzania (CEOrt), Santina Benson amesema jukwaa hilo limekuwa muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara nchini na uchumi kwa ujumla.

Santina amesema hayo katika maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa CEOrt ambapo zimefanyika mbio zinazojulikana kama ‘CEOrt Legacy Walk’ Jumamosi Julai 12, 2025, Masaki jijini Dar es Salaam.

“Kupitia majukwaa ya juu ya mazungumzo na ushawishi wa sera, CEOrt imekuwa chombo muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara nchini, kuwezesha mazungumzo ya wazi kati ya sekta binafsi na Serikali, na kuchochea mageuzi katika maeneo muhimu kwa mabadiliko ya kiuchumi,” amesema.

Matembezi hayo ya kihistoria yamewakutanisha watendaji wakuu kutoka taasisi mbalimbali, wadau wa Serikali na washirika wa maendeleo kwa pamoja kusherehekea robo karne ya uongozi, ushirikiano, na mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa.

Mwenyekiti wa CEOrt, David Tarimo, amesema:”Kutimiza miaka 25 ni ishara ya mafanikio ya sekta binafsi nchini katika kujieleza, kushiriki kwenye sera na kudumisha maadili muhimu.”


“Maadhimisho haya yanathibitisha nafasi ya CEOrt kama mshirika wa kuaminika wa maendeleo ya kitaifa na tunaendelea kujitolea kukuza uongozi wa maadili, utawala bora, na majadiliano ya dhati kati ya sekta binafsi na Serikali,” amesema.

Kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita, CEOrt inayowakilisha  wakurugenzi wakuu 220 kutoka sekta mbalimbali imekuwa kinara katika kukuza uongozi wa maadili, utetezi wa sekta binafsi na kuimarisha majadiliano ya pamoja kati ya sekta binafsi na serikali kama nguzo kuu za maendeleo ya taifa.

Simon Shayo, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti anayesimamia Masuala ya Uendelevu na Mahusiano ya Kijamii barani Afrika, amesema:“GGML inaamini biashara yenye uwajibikaji ndio biashara endelevu.”

“Legacy Walk ya CEOrt ina maana ya kipekee kwetu, tunasherehekea miaka 25 ya uwepo wetu nchini Tanzania pamoja na CEOrt, tukisisitiza dhamira yetu ya ushirikiano, uwazi, na athari chanya kwa taifa,” amesema.

 Philip Besiimire, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania amesema wakati kampuni hiyo ya simu ikiadhimisha miaka 25 ya kuiunganisha Tanzania kupitia Vodacom, wanajivunia kushiriki safari hii na ya miaka 25 ya CEOrt katika kuendeleza maono ya pamoja ya mustakabali bora na jumuishi.

“Uwazi wetu katika ujumuishaji wa kidijitali na kifedha, ubunifu, na ushirikiano wa lengo unaendelea kuleta mabadiliko chanya na kuwawezesha Watanzania kwa miaka 25 ijayo na zaidi,” amesema.

Related Posts