Kasi wanawake kuchepuka yapanda Marekani

Dar es Salaam. Unaweza kusema kuchepuka imeanza kuonekana ni jambo la kawaida, awali hili lilifanywa zaidi na wanaume lakini sasa wanawake nao hawako nyuma.

Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Institute for Family Studies (IFS) wa mwaka 2024  na ripoti yake kuchapishwa mwaka 2025 unaoonesha kasi ya wanawake kuchepuka imeanza kuongezeka ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.

Kulingana na utafiti huo uliofanyika nchini Marekani unaonesha asilimia 20 ya wanaume walio kwenye ndoa na uhusiano rasmi wamekiri kuchepuka huku wanawake wakiwa asilimia 13.

Utafiti huo umekwenda mbele na kuonesha endapo vipimo vya vinasaba vitafanyika katika kila familia kubaini upo uwezekano familia nyingi zikaingia kwenye migogoro kwa kuwa, wapo watoto watakaobainika kuzaliwa nje ya ndoa au uhusiano rasmi.

Kwa mujibu wa utafiti huo imebainika kadiri umri unavyokwenda mwanamke anapoteza hofu ya kutoka nje ya uhusiano wake rasmi na hilo mara nyingi hutokea baada ya kuchoka kuvumilia changamoto anazokutana nazo kwenye uhusiano huo.

“Tafiti zinaonesha kuwa, wanawake wakifikia umri mkubwa hujihisi kuwa na ujasiri zaidi katika matamanio yao, wanakuwa hawana ile hofu kwamba jamii itawatazama vipi. Vilevile, kutoridhika katika uhusiano wa muda mrefu au hamu ya kupata uzoefu mpya kunaweza kuongeza hatari ya usaliti.

“Wanawake wanaojitegemea kifedha pia hupata uhuru wa kufanya uamuzi bila kuogopa kutegemea mwenza wao.

“Hata hivyo, si wanawake wote wakubwa hujihusisha na usaliti tabia hii hutegemea uamuzi binafsi na hali uhusiano wao,” amesema mkurugenzi wa tafiti wa IFS, Wendy Wang.

Mwananchi imezungumza na baadhi ya wanawake na wanaume ambao wamekiri suala la kuchepuka limekuwa tatizo sugu linalohatarisha uimara wa taasisi ya ndoa na uhusiano.

“Kwa asili, mwanamume hawezi kuwa na mwanamke mmoja, huo ndio uhalisia labda kama unataka kubishana na asili, ila ni ajabu kuona wanawake nao wanaiga huo utaratibu. Kwanza mwanamke akishaanza hayo mambo dharau inaanza ndani ya nyumba ndiyo maana wala hawatakiwi kujaribu,” amesema mmoja wa wanaume ambaye hakutaka jina lake liandikwe.

“Binafsi sijafikiria kufanya hivyo, lakini siwalaumu wanawake wanaochepuka kwa sababu wakati mwingine anaona ni heri afanye hivyo ili apate faraja, hiyo hutokea hasa pale anapovumilia sana matukio maana hawa wenzetu wana matukio sana,” amesema Katija Almasi mkazi wa Yombo Dovya.

Matokeo ya utafiti hayapishani sana na ripoti ya tathmini ya miaka mitatu ya Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia kilicho chini ya Mahakama ya Tanzania iliyoonesha uzinzi ni miongoni mwa sababu inayochangia ndoa nyingi kuvunjika.

Ripoti hiyo inazitaja sababu sababu tano kuu zinazochangia kuongezeka kwa mashauri yanayolenga kuvunja ndoa ni pamoja na kutengana, ambayo inaongoza kwa asilimia 25 ya kesi zote, ikifuatiwa na uzinzi inayochangia asilimia 16.

Mei 27, 2025 akiwasilisha bajeti bungeni, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima alisema wizara hiyo imeandaa mkakati wa kukabiliana na changamoto hiyo na Sh10.3 bilioni zimetengwa kwa ajili ya huduma ya usuluhishi wa ndoa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara hiyo kufikia Aprili 2025, mashauri 97,234 ya ndoa yameshughulikiwa kupitia vitengo vya ustawi wa jamii kuanzia ngazi ya halmashauri hadi Taifa, idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la mashauri 31,380 yaliyowasilishwa kipindi kama hicho mwaka 2023/24.

Kati ya mashauri hayo, 81,820 yalipatiwa ufumbuzi huku mashauri 15,414 yakipelekwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Teknolojia yatajwa kurahisisha usaliti

Licha ya sababu kadhaa ikiwamo hali ya kiuchumi, migogoro na kukosekana mawasiliano kwa wenza, mmomonyoko wa maadili kutajwa kuchangia hali hiyo, maendeleo ya teknolojia nayo yanatajwa kuchangia kwa kiwango kikubwa cha usaliti kwenye uhusiano kwa sasa.

Mitandao ya kijamii, programu za mawasiliano na tovuti za kutafuta wapenzi zimefanya kuwa rahisi zaidi kwa watu kuanzisha uhusiano wa siri.

Programu za kutafuta wenza zimefanya iwe rahisi zaidi kwa watu kuanzisha uhusiano wa muda mfupi au ya siri.

Kwa mujibu wa ripoti ya Jarida la Computers in Human Behavior, asilimia 18 hadi 25 ya watumiaji wa Tinder wako kwenye ndoa au uhusiano wa kudumu ilhali wanatumia programu hiyo.

Ripoti hiyo ilichunguza kwa nini watu walioko kwenye uhusiano bado wanatumia programu ya kutafuta wapenzi licha ya kuwa na wapenzi wao.

Kulingana na ripoti hiyo, asilimia 42 ya watumiaji wa Tinder walioulizwa nchini Marekani walikiri kuwa wameoa au wako kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Mshauri wa ndoa Deogratius Temba anakiri kuwa mitandao ya kijamii imekuwa chombo kikuu kinachochochea usaliti katika ndoa na uhusiano.

“Siku hizi kupitia mawasiliano ya faragha watu wanatumiana picha na kujenga uhusiano wa kihisia mtandaoni hapo ndipo mambo yanapoanza. Urahisi wa kuficha mawasiliano huwapa watu ujasiri wa kufanya mambo ambayo wasingeweza kufanya kwa uwazi. Hii inaongeza changamoto katika kuelewa na kudhibiti usaliti katika uhusiano wa sasa.

Wasemavyo viongozi wa dini

Akizungumzia hilo, Askofu wa Kanisa la Anglican Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosteness amesema hayo ni matokeo ya mmonyoko wa maadili kwenye jamii hivyo kazi kubwa inapaswa kufanyika.

“Tukiri kwamba huenda tunaopaswa kufundisha maadili hatujafanya kazi yetu sawa, taasisi ya familia nayo imeshindwa kuwandaa vijana katika misingi ya kwenda kudumu kwenye ndoa. Kutokana na ukweli huu basi tunapaswa kuweka nguvu kubwa kwenye kizazi kijacho ili kuzuia tatizo hili lisiendelee,” amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amesema ni muhimu kwa wanajamii kurudi katika misingi ya dini na kuzingatia inachoelekeza kuhusu ndoa.

“Ukisimamia misingi ya dini huwezi kupata shida, tukija kwenye suala la ndoa turudi katika dini tuangalie inatuelekeza kufanya nini. Tukiyajua na kuzingatia maelekezo basi kila kitu kitakwenda sawia.

“Mwanamume atajua wajibu wake na mwanamke atafahamu vitu gani azingatie kama mke ndani na nje ya nyumba. Dini inazuia masuala ya kutoka nje ya ndoa sasa kama unazingatia mafundisho hayo suala la michepuko halitakuwa na nafasi kwako, amani, upendo na utulivu vitatawala kwenye ndoa yenu,”amesema Sheikh Mataka.

“Wanandoa ni zao la jamii, kuna mporomoko mkubwa wa maadili kwenye jamii. Jamii yetu haiishi kidini, uongo umekuwa sehemu ya maisha, kukosa uaminifu inaonekana ndio ujanja. Hapa ndoa haiwezi kudumu.”

Related Posts