KESI YA MAUAJI YA MUUZA MADINI MTWARA: Kutoka mipango, mauaji mpaka askari kunyongwa- 14

Dar es Salaam. Katika sehemu hii, Mahakama Kuu chini ya Jaji Hamidu Mwanga inafafanua majukumu ya kila mshtakiwa katika tukio hilo na kujibu kiini cha pili cha shtaka kama washtakiwa wanahusika na mauaji hayo au la.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gilbert Sostenes Kalanje aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Charles Onyango (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara) na Nicholous Kisinza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara.

Wengine ni Marco Chigingozi, Mkaguzi Msaidizi, John Msuya (Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara), Shirazi Mkupa (Mkaguzi Msaidizi) na Salim Mbalu alikuwa Koplo.

Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo  wilayani  Mtwara.

Katika sehemu iliyopita, tuliona namna Jaji Mwanga alivyoliondoa katika hatia kundi la kwanza la washtakiwa wanne, kati ya makundi matatu aliyoyatenga; leo anaendelea na mshtakiwa wa tano,Inspekta Msuya, daktari wa zahanati ya polisi.

Huyu ndiye aliyemdunga Mussa sindano ya Ketamine ambayo kama Mussa angeamka angekuwa na maluwe luwe.

Inspekta Msuya alieleza kila kitu kuhusu mipango ya uhalifu baada ya kutokubaliana na wao suala la kumdunga Mussa sindano ya sumu.

Katika utetezi wake, alidai kuwa Ketamine 1cc aliyomdunga haiwezi kusababisha kifo na alichokifanya kilikuwa ndani ya wigo wa miongozo ya Utendaji wa Jeshi la Polisi (PGO) hapa Tanzania.

‎Alidai kuwa, lengo lilikuwa kuzuia uhalifu alioambiwa mtuhumiwa (Mussa) alikuwa ameufanya na alifuata maadili ya kazi yake kutii maelekezo ya ya bosi wake, mshtakiwa wa kwanza, Kalanje, utetezi ambao Jaji Mwanga aliukataa.

Wakili wake, Felister Awasi naye alisisitiza hoja hiyo hiyo, huku akinukuu PGO namba 1 (5), inayohimiza heshima kwa wakubwa ndani ya Jeshi la Polisi na PGO namba 106 (44)(e), inayoeleza athari za kukataa kutii agizo halali.

Jaji achambua sindano ya usingizi

Jaji Mwanga alianza kwa kusema hakubaliani na hoja ya wakili Awasi aliyekuwa akimtetea mshtakiwa, akisema haikubaliki na haina msingi wa kitabibu.

“Sikubaliani na hoja hiyo, kwa sababu haina msingi wa kitabibu na ni jambo lisiloaminika hata kidogo, ukizingatia kiapo cha daktari na uelewa wake wa haki za binadamu na sheria ya jinai, ambavyo vingemfanya atambue tofauti,”alisema Jaji Mwanga.

“Daktari aliyehitimu kwa weledi angejiuliza agizo kama hilo na ajitafakari. Kwanini raia asiye na hatia au hata mtuhumiwa, apewe dawa ya usingizi akiwa mahabusu? Je, kuna sababu yoyote ya kitabibu inayohalalisha?

“Alikuwa na wajibu wa kitaaluma na wa kimaadili kukataa agizo hilo na ikiwezekana kuliripoti kwa mamlaka ya juu au vyombo husika vya usimamizi. Kuweka usahihi, PGO iliyotajwa na wakili, inazungumzia agizo halali,”alieleza Jaji Mwanga.

“Alichofanya mshtakiwa wa tano hakiwezi kuhesabiwa kuwa agizo halali. Hakikubaliki kisheria na kilikuwa ni mbinu ya mateso, kama zilivyo mbinu nyingine za mateso ambazo zimepigwa marufuku kisheria.

“Maarifa yake ya kitaaluma ya udaktari na wajibu wa kimaadili unamweka katika nafasi ya juu ya kutambua agizo lisilo halali na kutenda kwa mujibu wa kiapo chake cha udaktari,”alisisitiza Jaji Mwanga.

 “Hivyo, utetezi huo haumkingi na matendo yake bali unamuweka kwenye hatari ya kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu, kwani kwa kumfanya Mussa apoteze fahamu na kuwa mnyonge, huenda alirahisisha mno kushambuliwa kikatili na kuuawa bila uwezo wa kutoa upinzani au kupambana.”

Upenyo uliomnusuru kutiwa hatiani

Jaji Mwanga alieleza kuwa, ingawa mshtakiwa wa tano huenda alitenda kwa njia isiyo ya kitaaluma kwa kiwango kikubwa, lakini baada ya kumpa ushauri mshtakiwa wa kwanza, hali yake ya kiakili ilibadilika kutoka kwenye dhamira ya mauaji na kuelekea kwenye jambo jingine.

 “Kwa mujibu wa kifungu cha 23 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, hana nia ya pamoja, kwa kuwa ushahidi unaonesha taarifa pekee aliyokuwa nayo ni kuhusu kosa (la kutunga) alilodaiwa kulitenda marehemu (Mussa).

“Aidha, aliripoti tukio hilo kwa RCO (Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara), japokuwa kwa kuchelewa, na aliendelea kuwataja watu waliokuwa wanahusishwa na kupotea au kuuawa kwa Mussa. Angeweza kuchagua kutofanya hivyo kama hakuwa mkweli,”alisema Jaji Mwanga.

“Ukosefu wa ushahidi wa upande wa mashtaka unaokinzana na wake, unampatia manufaa ya kuacha shaka, hivyo itaaminika kuwa, alikuwa anasema ukweli. Kwa hiyo hoja ya pili pia inajibiwa kwa kumwondolea hatia mshtakiwa wa tano.”

Ushiriki wa Kalanje, Onyango kwenye mauaji

Sasa ni zamu ya kundi kwanza linalojumuisha mshtakiwa wa kwanza, Kalanje (aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara) na wa pili Onyango, (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara) waliopewa majukumu ya upelelezi na usimamizi kama wakuu wa ngazi ya wilaya.

Walikuwa watu wa mwisho kuonekana na marehemu akiwa hai Januari 5, 2022.

Jaji alisema kulingana na ushahidi wa shahidi wa tatu upande wa mashtaka,  mshtakiwa wa kwanza, Kalanje alimwagiza shahidi wa nne wa utetezi ambaye ni mshtakiwa wa nne, amwambie Mussa afike ofisini kwake.

“Agizo hilo lilitekelezwa na Januari 5, 2022, Mussa alifika kituoni hapo na kuonana na mshtakiwa wa kwanza ofisini kwake. Mshtakiwa huyo wa nne na shahidi wa pili, Salim Abdallah Ng’ombo aliyemsindikiza Mussa kituoni hapo siku hiyo, lakini mshtakiwa wa kwanza akamfukuza, walithibisha ushahidi huo,”alisema Jaji.

 “Ni kanuni ya kisheria kuwa, iwapo mshtakiwa anadaiwa kuwa mtu wa mwisho kuonekana na mtu na baadaye akabainika kufariki dunia, na kusipokuwepo maelezo ya kueleweka kuhusu mazingira yaliyosababisha kifo hicho, basi atahesabiwa kuwa ndiye aliyemuua,”alieleza Jaji Mwanga katika uchambuzi huo.

“Hivyo, kama ilivyowasilishwa ipasavyo na upande wa mashtaka, mshtakiwa wa kwanza na wa pili walikuwa watu wa mwisho kuonekana na Mussa, akiwa hai, hivyo walikuwa na wajibu wa kueleza alipo.”

“Kwa kukosekana kwa maelezo yanayoeleweka kuhusu mazingira ya kifo hicho, wanahesabiwa kuwa ndio wauaji,”alisisitiza Jaji Mwanga.

“Mbali na hilo, mshtakiwa wa kwanza alikuwa tayari ameeleza dhamira yake ya kumuua Mussa, kwa mshtakiwa wa tano, alipomuuliza kama ana sindano ya sumu awasaidie kumdunga.

“Kama alivyoeleza shahidi wa tano wa utetezi, mshtakiwa wa kwanza ndiye aliyemfunika Mussa puani na mdomoni kwa kitambaa hadi akafa kwa kukosa hewa,”alieleza Jaji Mwanga.

Katika hoja zake, Wakili Majura Magafu wa mshtakiwa wa kwanza, alipinga ushahidi wa shahidi huyo akidai kuwa, haukufikia kiwango cha kukiri shtaka kwa mdomo kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 3(1) cha Sheria ya Ushahidi, hivyo hauwezi kutumika kumtia hatiani mshtakiwa wa kwanza.

Kwa mujibu wa kifungu cha 33(2) cha Sheria ya Ushahidi,  Marejeo ya 2022, ili ushahidi wa mshtakiwa umtie hatiani mshtakiwa mwenza, sharti ushahidi uthibitishwe.

Jaji Mwanga alieleza kuwa, kanuni hiyo ilielezwa pia na Mahakama ya Rufani katika kesi mbalimbali ikisisiza kuwa, kama tahadhari, ushahidi wa mshtakiwa mwenza lazima uthibitishwe kabla ya kuzingatiwa kumtia hatiani mshtakiwa mwingine.

“Uthibitisho, kama unavyoeleweka kisheria, unaweza pia kutokana na maneno au matendo, kama Mahakama ya Rufani ilivyoamua kwenye kesi za Pascal Kitigwa na Mboje Mawe na Wengine watatu na kuweka msimamo wa kisheria,”alieleza Jaji Mwanga.

Fuatilia kesho kujua uamuzi uliofikiwa mwisho

Related Posts