KIUNGO Mtanzania Suzana Adam, ambaye alikuwa anakipiga FC Masar ya Misri, anawindwa na timu za Ligi Kuu nchini humo na Morocco.
Nyota huyo amemaliza mkataba wa miaka miwili aliokuwa anatumikia FC Masar, alipojiunga mwaka 2023 akitokea Fountain Gate Princess ya Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, meneja wa mchezaji huyo, James Mlaga, alisema ni kweli amemaliza mkataba na hawajaongeza, lakini ana ofa kutoka nchi mbili.
“Tulikuwa na mkataba wa miaka miwili na FC Masar, 2023/2025. Sasa umeisha rasmi na ni mchezaji huru, hajasaini popote. Tuna ofa za timu tatu kutoka Misri na moja Morocco. Tunasubiri kufanya chaguo sahihi,” alisema Mlaga na kuongeza:
“Sina kumbukumbu sahihi kabisa ila hatukuwa na misimu bora Misri, maana alikaa nje karibu msimu mzima 2023/2024. Alicheza mechi kama mbili tu za mashindano. Msimu wa 2024/2025 ulikuwa wa ‘ingia-toka’ kutokana na kuumwa na kupona kwa goti, hivyo kama asilimia 40 hivi za msimu wa 2024/2025 alicheza.”
Msimu wake wa kwanza, kiungo huyo wa zamani wa Alliance Girls ya Mwanza alipata jeraha la goti likamuweka nje msimu mzima, na baadaye FC Masar ikamtoa kwa mkopo kwenda Maad Ladies.
Kama Suzana ataondoka kikosini hapo, basi atasalia Mtanzania mmoja, Hasnath Ubamba, aliyejiunga na timu hiyo mwaka 2024 naye akitokea katika klabu ya Fountain Gate.