Katika maisha ya kila siku, tunaumia kwa sababu ya matendo ya wengine kwa maneno ya kuumiza, vitendo vya hila, usaliti, au hata dhuluma. Lakini Biblia inatufundisha kwamba, kama Wakristo, tunapaswa kusamehe, siyo kwa masharti au kwa kubadilishana na kitu, bali kusamehe kutoka moyoni.
Mfano mkuu wa kusamehe bila masharti unaonekana wazi katika maisha ya Yusufu, mwana wa Yakobo.
Yusufu alipitia mateso kwa sababu ya ndugu zake. Walimchukia kwa sababu ya ndoto zake, walimvua vazi lake la rangi nyingi, wakamtupa shimoni, na hatimaye wakamuuza kwa wafanyabiashara Waishemaeli waliompeleka Misri. Kwa miaka mingi, Yusufu aliishi kama mtumwa na baadaye mfungwa, kwa kosa ambalo hakufanya. Pamoja na hayo yote, moyo wake haukuwa wa kisasi, bali wa huruma na msamaha.
Miaka mingi baadaye, baada ya kuinuliwa kuwa waziri mkuu wa Misri, Yusufu alikutana tena na ndugu zake waliomdhulumu.
Nguvu, mamlaka na nafasi alizokuwa nazo zingempa uwezo wa kulipiza kisasi kwa urahisi. Lakini Yusufu alifanya kinyume kabisa na matarajio ya wengine. Alilia kwa uchungu wenye kuonyesha upendo, akawakumbatia, na kuwaambia maneno haya:
“Lakini Yusufu akawaambia, Msiogope; je! Mimi ni badala ya Mungu? Ninyi mlikusudia mabaya juu yangu; bali Mungu alikusudia mema, ili afanye kama ilivyo leo, kuwaokoa watu wengi maisha.” (Mwanzo 50:19-20)
Maneno haya yanafunua msamaha wa kweli: msamaha usio na masharti, unaotambua kwamba Mungu anaweza kutumia hata uovu wa watu kuleta matokeo mema. Yusufu hakusema, “Nitawasamehe kama mtaomba msamaha,” au “Nitawasamehe kama mtanirudishia miaka yangu ya mateso.” Aliwasamehe kwa moyo mkunjufu, kwa sababu alijua mpango wa Mungu ulikuwa mkuu kuliko maumivu yake.
Yesu Kristo mwenyewe, ambaye ni mfano mkuu wa msamaha, alifundisha wazi:
“Msameheane; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo hivyo na ninyi.” (Wakolosai 3:13)
Katika Mathayo 18, Yesu alimfundisha Petro kuhusu msamaha. Petro alimuuliza, “Bwana, ndugu yangu akinikosea mara ngapi nitamsamehe? Mpaka mara saba?” Yesu alijibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.” (Mathayo 18:21-22). Hii inamaanisha msamaha wetu haupaswi kuwa na kikomo wala masharti.
Yesu aliendeleza somo hili kwa mfano wa mtumishi asiye na huruma. Alikuwa na deni kubwa ambalo hasingeweza kulilipa, na bwana wake alimsamehe. Lakini yeye alikataa kumsamehe mwenzake aliyekuwa na deni dogo. Yesu alihitimisha mfano huu kwa kuonyesha kuwa Mungu hataridhika nasi ikiwa hatutawasamehe wengine kama yeye alivyotusamehe sisi.
Kusamehe bila masharti haina maana ya kupuuza makosa au kuhalalisha mabaya. Badala yake, ni kuamua kutobeba maumivu yoyote, kutoyatumia kama silaha dhidi ya aliyekukosea na kuachilia kisasi mikononi mwa Mungu. Paulo anasema:
“Msilipize kisasi, wapendwa, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi, Mimi nitalipa, asema Bwana.” (Warumi 12:19)
Msamaha ni zawadi tunayotoa kwa wengine, lakini pia ni uponyaji tunaojipa sisi wenyewe. Mtu ambaye hasamehi hubeba mzigo mzito wa chuki, hasira, na maumivu. Yusufu hakubeba mzigo huo alichagua njia ya amani na upendo.
Wapo watu kutokana na waliyotendewa wamediriki hata kujiapiza kwamba fulani sitamsamehe hadi ninaingia kaburini. Fulani sitaki kumwona nikimwona najisikia kichefuchefu kwa aliyonifanyia. Mpendwa Mkristo leo unaposoma ujumbe huu, achilia moyo wako kwa Mungu wetu aliyehai, kubali kusamehe bila masharti yoyote upate kupona.
Somo tunalopaswa kujifunza ni kwamba: kusamehe si kwa ajili ya yule aliyekukosea tu, bali ni kwa ajili ya nafsi yako, kwa ajili ya uhusiano wako na Mungu na kwa ajili ya uzima wako wa milele. Yesu alitusamehe tulipokuwa bado wenye dhambi (Warumi 5:8), hatukuwa tumestahili msamaha wake. Vivyo hivyo, tunapaswa kuwasamehe wengine hata kama hawastahili. Yesu alivyotufundisha: “Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tumewasamehe wadeni wetu” (Mathayo 6:12). Hii ni sala ya kutafakari kila siku kuwa watu wa msamaha, kwa moyo mweupe, bila masharti. Neno la Mungu lipo hai jana, leo na milele yote, hivyo kama Yusufu, tuitikie wito wa Mungu wa kusamehe bila masharti.
Tuwasamehe waliotuumiza, tukijua kuwa msamaha hauhitaji sababu kubwa unahitaji utii kwa Mungu na upendo kwa wanadamu. Pia kama Yesu alivyotufundisha msalabani aliposema, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo” (Luka 23:34), tuwe tayari kusema vivyo hivyo. Msamaha ni ushindi wa upendo juu ya chuki.