Majambazi Kigoma ‘wambipu’ Sirro, wateka basi la abiria

Kigoma. Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha, wamewapora na kuwajeruhi baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Kigoma kwenda jijini Mwanza.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumapili, Julai 13, 2025 eneo la Kibaoni karibu na Kambi ya Wakimbizi ya Nduta Kibondo.

Hata hivyo, Mwananchi ilimtafuta, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu ambaye amekiri kutokea kwa tukio hilo huku akisema yuko porini kikazi na atalizungumzia tukio hilo baadaye.

“Bado niko vijijini huku, baadaye labda nitatoa taarifa kamili lakini ni kweli kuna gari la Adventure na Kluger yalitekwa na majambazi inaoaminika kwamba walikuwa na silaha, wakapora na vitu lakini polisi wa Nduta waliwahi wakazuia ile hali,” amesema Makungu na kuongeza kuwa, hakuna mtu aliyepigwa risasi wala aliyeuawa huku akiwataka wananchi wasiwe na hofu kwa kuwa vyombo vya dola vimeimarisha doria saa 24.

Katika tukio hilo, baadhi ya abiria wamejeruhiwa, kupigwa na marungu huku fedha, simu na mabegi ya nguo vikichukuliwa na watu hao watano.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku moja imepita tangu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simon Sirro alipohitimisha ziara ya kikazo Wilaya ya Kigoma aliyoianza Julai 7 hadi 11, 2025.

Sirro ambaye amewahi kuwa, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) aliwasili mkoani huo Julai 8, 2025 kuanza kutumikia nafasi hiyo baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua nafasi ya Thobias Andengenye aliyestaafu.

Baada ya kumaliza ziara hiyo, Sirro alitoa wito kwa wananchi kuacha kushirikiana na wahalifu huku akitumia kauli kuwa ‘Sirro wa kipindi cha nyuma hajabadilika kwenye kupambana na uhalifu.’

“Naujua Mkoa wa Kigoma vizuri, nimeenda Operesheni Kimbunga kwa miezi sita, najua kila kijiji cha mkoa huu na njia za wahalifu, haitakuwa kazi kwangu kujikumbusha na kusimamia mpango wa kudhibiti uhalifu mkoani Kigoma,’’ alisema Sirro.

Akizungumza leo, Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Agrey Magwaza amesema tukio hilo lililotokea saa nne usiku wa jana  katika tukio hilo watu wanne walijeruhiwa kwa kupigwa na marungu huku fedha, simu na mabegi ya nguo vikichukuliwa.

Kanali Magwaza amesema kwa mujibu wa taarifa alizozipata kutoka kwa askari wanaolinda katika Kambi ya Wakimbizi Nduta, watu hao wanatajwa kuwa kama watano na walitoweka baada ya kutekeleza uporaji huo.

Amesema wahalifu hao waliweka vizuizi katikati ya barabara kuu ya kutoka Kasulu- Kakonko inayopita Kambi ya Wakimbizi Nduta na kufanikiwa kuzuia Basi la Adventure lililokuwa likielekea jijini Mwanza na gari jingine dogo.

“Hao watu walikuwa na silaha kwa sababu inasemekana walipiga risasi juu kuwatia hofu watu waliokuwa kwenye magari hayo, nani kweli walichukua mali za abiria, simu, fedha na mabegi ya nguo.

“Pia, waliwajeruhi watu wanne ambao hawakuwa wamejeruhiwa sana wakapata matibabu pale Nduta (Kambi ya Wakimbizi) na waliruhusiwa kuendelea na safari,’’ amesema Kanali Magwaza.

Katika tukio hilo,  kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa abiria waliokuwa katika magari hayo, inadaiwa idadi ya majambazi hao wanatajwa kuwa watano huku thamani ya mali zilizoporwa ikiwa bado haijafahamika kama alivyobainisha Kanali Magwaza.

“Hakuna aliyeuawa na thamani ya mali bado haijafamika ingawa kwenye gari dogo walisema kuna Sh3.5 milioni na hatuwezi kujua kila abiria aliporwa mali ya kiasi gani kwa sababu walichukua mpaka mabegi ya nguo,” amesema Kanali Magwaza.

Related Posts