BAADA ya kushindwa kufanya kile kilichotarajiwa na Simba, kiungo mkabaji mwenye uraia wa Angola na DR Congo, Debora Fernandes Mavambo anatajwa kutimkia Singida Black Stars msimu ujao.
Debora alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka mitatu mwanzo mwa msimu ulioisha akitokea Mutondo Stars ya Zambia.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti Mavambo hayupo kwenye mpango wa kikosi chao msimu ujao, wanachokifanya sasa ni namna ya kumalizana naye kwani bado ana mkataba wa miaka miwili na timu hiyo.
“Hayupo kwenye mpango wa mwalimu msimu ujao licha ya kuwa bado ni mchezaji wetu, mipango iliyopo ni kufanya mazungumzo ya pande zote mbili kujua tunaachanaje, lakini hadi sasa bado hatujamalizana,” kilisema chanzo.
Wakati Simba ikiwa hivyo, Mwanaspoti linafahamu nyota huyo anawindwa na Singida Black Stars kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao baada ya kiungo wao Mohamed Damaro kutajwa kutua Yanga.
“Huyo ni mchezaji wa Simba, sio rahisi kuanza mazungumzo na sisi, siwezi kulizungumzia hilo kwa mujibu wa kanuni za shirikisho hainipi mwanya wowote wa kumzungumzia mchezaji wa timu nyingine,” alisema bosi mmoja wa Singida Black Stars.