Arusha. Wakuu watatu wa wilaya wastaafu wameungana na wakazi wa Wilaya ya Arumeru na maeneo jirani kuuga mwili wa aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya mbalimbali nchini, Elias Goroi aliyefariki dunia Julai 8,2025 katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre alikokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza kwa niaba ya wastaafu wenzake, Lembis Kipuyo alimwelezea marehemu Goroi alikua mchapakazi hodari aliyependa kuwatumikia wananchi katika wilaya zote alizopangiwa bila ubaguzi, hofu wala upendeleo.
“Kila nilipokutana naye wakati wa utumishi wetu alikua akinikumbusha kuwa sisi tunaotoka kwenye jamii ya wafugaji tunapaswa kufanya kazi kwa bidii pasipo kumwangusha Rais aliyetuamini ili tuwe mfano bora kwa vijana wengine watakaopata nafasi kama hizo katika siku za baadaye,” amesema Kipuyo
Amesema wakati wa utumishi wake, Goroi alikua akipangiwa wilaya zenye migogoro ya ardhi pia za wakulima na wafugaji na kwa sehemu kubwa aliweza kushirikiana na viongozi wenzake kuimaliza migogoro hiyo kwa wakati.
Kipuyo ambaye alikua na wakuu wa wilaya wastaafu,Novatus Makunga na Edward Ole Lenga amesema marehemu Goroi alisimamia ujenzi wa shule za sekondari za kata na shughuli za ulinzi na usalama kwenye maeneo magumu alikofanya kazi.
Akisoma wasifu mtoto wa marehemu Goroi, Ebenezer Goroi amesema baba yake kitaaluma alikua mwandishi wa habari aliyesoma katika Chuo cha Uandishi wa Habari (TSJ) alipotunukiwa stashahada na baadaye alijuunga na Chuo cha Texas Lutheran nchini Marekani, ambapo mwaka 1991 alitunukiwa Shahada ya Sanaa katika Mawaliano.
Amesema mwaka huohuo aliendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Incarnate World nchini Marekani na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika Sanaa ya Mawasiliano na kufanya kazi sehemu mbalimbali kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya mbalimbali nchini.
Ebenezer amesema aliteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1993 kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro baadaye kuwa Mkuu wa wilaya za Makete, Iringa, Kilosa, Lushoto, Mbulu, Nachingwea na Rorya mwaka 2015 hadi alipostaafu baada ya kusumbuliwa na maradhi.
“Marehemu baba yetu alikua akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa miaka mingi,hata hivyo kufikia mwaka 2015 alipata shida ya kutokuona na miaka michache baadaye alipata shida ya figo, hivyo kuanza matibabu yake na Julai 8,2025 alianza kutojisikia vizuri na kuwahishwa hospitali kwa matibatu mpaka alipofikwa na umauti,”amesema
Marehemu Goroi ameacha watoto watatu na mwili wake umesafirishwa kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho Jumatatu Kijijini cha Samunge Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.