NANDI KUUNGA MKONO NEMBO YA MADE IN TANZANIA AHAIDI KUITUMIA KWENYE BIDHAA NA MZIKI WAKE

Msanii wa muziki wa kizazi Kipya, Faustina Charles Mfinanga, maarufu kwa jina la Nandy, ameonyesha dhamira ya dhati ya kuiunga mkono nembo ya ‘Made in Tanzania’ kwa kuitumia katika shughuli zake za muziki na biashara.

Akiwa miongoni mwa wageni waliotembelea Banda la Made in Tanzania katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Nandy amesema amepata elimu kuhusu umuhimu wa nembo hivyo atahakikisha anatumia nafasi yake aliyekuwa nayo kuitambulisha kimataifa kupitia bidhaa na kazi zake za ubunifu.

Nandy amesema amevutiwa sana na namna nembo hiyo inavyotambulisha bidhaa za Tanzania duniani na kusisitiza kuwa kupitia elimu aliyoipata kumbe anaweza kuzalisha bidhaa zake hapa nchini na kutumia nembo hiyo.

“Mimi nafanya biashara ya urembo na bidhaa zangu nyingi natoa nche ya nchi, baada ya kupata elimu leo kumbe naweza kutengeneza na kuzalisha bidhaa zangu hapa nchini na kutumia nembo hii ya Made in Tanzania haisee hili ni kitu kikubwa sana.

“Kupitia maonesho haya nimepata elimu na imenipa motisha kubwa kwamba naweza kuzalisha bidhaa zangu na kuitangaza Tanzania, tutaendelea kupata elimu ili tuwe mabalozi wazuri wa kuitangaza nembo hii,” amesema Nandy ambaye anajulikana pia kama African Princess

Nembo ya Made in Tanzania inasimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na imelenga kuimarisha utambulisho wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.


Related Posts