Nimca kuwatunuku tuzo Mwinyi, Nyerere

Dar es Salaam. Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (Nimca) unatarajia kuwatunuku tuzo maalumu marais wastaafu wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Ali Hassan Mwinyi kwa mchango wao katika kukuza tasnia ya habari kusini mwa Afrika.

Tuzo hizo zitatolewa katika mkutano mkuu wa Nimca utakaoanza kesho Julai 14 hadi 17, 2025 jijini Arusha ukitarajiwa kuhudhuriwa na wageni wanaowakilisha mabaraza ya habari kutoka mataifa mbalimbali Afrika.

Mbali na utoaji wa tuzo hizo, mkutano huo utajadili masuala mbalimbali na kutathmini hali ya tasnia ya habari Bara la Afrika na namna ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza zikiathiri uhuru wa habari kwenye mataifa hayo.

Akizungumzia tuzo kwa viongozi hao, Mkuu wa Timu ya Ushauri wa Kiufundi – Nimca, Bryan Toshi amesema awamu za viongozi hao zilikuwa na mchango wa pekee katika kukuza na kuendeleza tasnia ya habari.

Amesema waandishi wa habari wakongwe wa ndani na nje ya Tanzania wametambua mchango wa Rais wa awamu yapili, Mwinyi kwa mchango wake katika kukuza tasnia ya habari katika kipindi kigumu cha mageuzi.

Toshi amesema kauli yake ya rukhsa ilitoa msukumo wa kuanzishwa kwa vyombo vya habari nchini na uzoefu unaonesha kwamba, hakuna nchi kusini mwa jangwa la Sahara iliyotoa huo uhuru, hivyo ulikuwa ni ujasiri mkubwa.

“Ulikuwa ni uamuzi wa kijasiri kuviachia vyombo vya habari kuwa huru. Kwa hilo anastahili pongezi na tunaona kabisa kwamba, waandishi wa habari wa Kitanzania, viongozi wa kesho wa kesho wajaribu kumuiga,” amesema.

Amesema Mwinyi alifanya uamuzi wa busara ambao hautakiwi kusahaulika na hilo limeweka msingi wa ustawi katika sekta ya utalii Zanzibar kwa kuwafanya kuwa vivutio vya utalii kama ilivyo kwa mataifa mengine kama Marekani.

Kuhusu Mwalimu Julius Nyerere, Toshi amesema suala la kutambua mchango wake katika tasnia hiyo umechelewa kufanyika kwa kuwa, ni mtu aliyekuwa na chango mkubwa uliojenga msingi wa kukuza tasnia ya habari.

“Kwenye mkutano huu wa Nimca tutatoa pendekezo, kwamba kwa nini wizara zote za habari za Afrika, vyombo vya habari vya Afrika hususani katika nchi zile ambazo Mwalimu Nyerere alisaidia ukombozi wao, ni muda mwafaka sasa turidhie kuanzisha makumbusho maalumu ya vyombo vya habari na mawasiliano,” ameeleza.

Amesema hiyo itasaidia kutunza kumbukumbu ya harakati za ukombozi kusini mwa jangwa la Sahara na mbinu za mawasiliano zilizotumika ziwekwe kwenye makumbusho hayo ili kuhifadhi historia kwa vizazi vijavyo.

“Mimi nadhani tungetumia fursa hii kuwa na kitu tunachoweza kukiita ‘Tanzania Declaration’ kwamba tuanzishe African Media and Communication Museum (Makumbusho ya Vyombo vya Habari na Mawasiliano) na tumuombe Rais atupe ardhi hapa Arusha au Dodoma tumuenzi Mwalimu Nyerere katika hili,” amebainisha.

Mwenyekiti wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambaye pia ni Rais wa NIMCA, Ernest Sungura amesema Mwalimu Nyerere aliruhusu uwepo wa vyombo vya habari kwa wakati huo na pia alitumia vyombo vya habari kuleta umoja wa kitaifa).

“Kuna wakati hakukubaliana na chombo cha habari kuwa mouthpiece (mdomo) ya chama cha kisiasa na kutaka sauti za wananchi zisikike katika vyombo vya Habari. Itakumbukwa kuwa yeye mwenyewe alikuwa Editor-In-Chief (mhariri mkuu) na alihimiza suala la umoja wa kitaifa,” amesema.

Sungura amesema kumtunukia Nyerere tuzo hiyo hakutoshi, kwa maana ya kuwa mchango wake hauwezi kufananishwa na kitu chochote hapa nchini hata kama wangesema wajenge mnara wake pia usinge tosha.

“Hiki ambacho baraza inakifanya ni kutambua mchango wake, na kuiambia dunia kuwa huyu baba hakuwa tu mwanasiasa lakini pia alikuwa na mchango kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari,” amesema.

Amesema miaka mitano ijayo anaiona Nimca ikija na miradi kabambe ya kuikwamua tasnia ya habari hapa Afrika. Pia, amesema anaona mabaraza ya habari yakiwa na sauti moja kuhusu masilahi ya waandishi wa habari, wamiliki wa vyombo vya habari na vyombo vya habari.

Related Posts