Nkane afichua siri zake Yanga

KIUNGO mshambuliaji aliyemaliza mkataba wake na Yanga, Denis Nkane amekiri kunufaika na klabu hiyo ndani na nje ya uwanja, hivyo itabakia katika kumbukumbu ya maisha yake ya mpira wa miguu.

Nkane alijiunga na Yanga Januari Mosi, 2022 akitokea Biashara United ndani ya misimu mitatu alifanikiwa kuvaa medali za Ligi Kuu na Kombe la FA, lakini hadi sasa hakuna timu ambayo imepeleka ofa mezani baada ya kumaliza mkataba wake na Wanajangwani.

Mchezaji huyo aliliambia Mwanaspoti kuhusu maisha yake Yanga, kujifunza vitu vingi vya kiufundi kutoka kwa wachezaji wenzake na makocha waliyopita kwa nyakati tofauti katika timu hiyo.

“Nalizungumza hilo kwa herufi kubwa Yanga nimepata mafanikio ya ndani ya uwanja, ambayo ni mbinu za makocha mbalimbali ambao walikuwa wanatufundisha jinsi ya kujitambua katika maeneo muhimu kama nidhamu, kuzingatia soka linataka nini bila kufuatiliwa na mtu yoyote na kujituma katika mazoezi,” alisema Nkane na kuongeza.

“Yanga ilikuwa na wachezaji wazawa na wa kigeni ambao wana mafanikio makubwa katika mpira wa miguu, hivyo nilikuwa naangalia aina ya maisha yao ambayo yameniongezea kitu kikubwa katika kazi hiyo.”

Ingawa hakutaka kuweka wazi ni mafanikio gani aliyotapata nje ya uwanjani, lakini alisisitiza ana hatua kubwa ya kimaisha, kwani amepata kila kitu ambacho ni mahitaji muhimu ya binadamu.

“Kwa sasa nipo huru bado sijaanza mazungumzo na klabu yoyote, bado nina safari ndefu ya kuonyesha kipaji changu na nahitaji mpira wa miguu unilipe zaidi,” alisema.

Related Posts