Pochinki City mabingwa Ngao ya Jamii Yamle Yamle

MABINGWA watetezi wa michuano ya Yamle Yamle Cup, timu ya Pochinki City imetwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mazombi FC katika mechi ya ufunguzi ya mashindano hayo msimu wa 2025.

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Mao Zedong Julai 12, 2025 na kuhudhuriwa na mashabiki wengi ambao walikuwa na hamu ya kushuhudia mwanzo wa msimu mpya, Pochinki City ilionesha ubora wao kuanzia mwanzo huku juhudi zao zikizaa matunda kwa kuibuka na ushindi huo.

Mashindano ya Yamle Yamle yanayoendelea kwa msimu wake wa saba, yanazidi kushika kasi huku timu 16 zikichuana kuwania taji hilo linalozidi kupata umaarufu visiwani Zanzibar. 

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa msimu wa 7 wa mashindano hayo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita aliwakabidhi Pochinki City Sh5 milioni kwa kuibuka na ushindi.

Kwa upande wa Mazombi FC, imevuna Sh3 millioni baada ya kupata nafasi ya pili katika mechi hiyo ambayo ni  ufunguzi wa mashindano ya Yamle Yamle.

Mashindano hayo yataanza rasmi mzunguko wa kwanza hapo kesho Julai 14, 2025 ambapo Mborimborini itavaana na Kajengwa katika Uwanja wa Mao A na Nyamanzi itavaana na Munduli Uwanja wa Mao B, saa 10:00 jioni.

Related Posts