Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole amemwandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan ya kujiuzulu nafasi hiyo kwa sababu ya kile alichoeleza ni kusikitishwa na mwelekeo wa uongozi usiojielekeza katika kusimamia haki, amani na kuheshimu watu.
Katika barua hiyo aliyoiweka kwenye ukurasa wake wa Instagram leo Jumapili, Julai 13, 2025, yenye kichwa kisemacho “Taarifa ya kujiuzulu nafasi ya ubalozi na nafasi yangu ya uongozi wa umma,” Polepole ameeleza namna alivyofikia uamuzi huo mgumu baada ya tafakari ya kina.
Polepole amethibitisha kwamba, barua hiyo inayosambaa mitandao ni yake na ameandika mwenyewe kujiuzulu katika nafasi hiyo.
Mwananchi imeutafuta uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje kuzungumzia uamuzi huo wa Polepole, hata hivyo, sio Katibu Mkuu, Balozi William Shelukindo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Balozi Mindi Kasiga wala Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa waliopatikana kuzungumzia hilo.

Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema alichoeleza Polepole kwenye barua hiyo ni utashi wake na kwamba jambo la kufurahisha ni kuwa, amesema ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa chama hicho.
Polepole aliteuliwa na Rais Samia kuwa Balozi wa Cuba kuanzia Aprili 2023 hadi leo Julai 13, 2025 alipoandika barua hiyo ambayo nakala yake ameielekeza kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kabla ya kupelekwa Cuba, Polepole alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi alikotumikia kwa mwaka mmoja pekee kuanzia Machi 2022 hadi Aprili 2023.
Kabla ya hapo, Novemba 29, 2020, Hayati John Magufuli alimteua kuwa mbunge.
Mbali na kutumikia katika utumishi wa umma, Polepole alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, tangu alipoteuliwa Desemba 16, 2016.
Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo.
Katika barua yake ya kujiuzulu ya leo Julai 13, 2025, Polepole ameeleza kwamba, kwa muda ambao amekuwa akitumikia Taifa ndani na nje ya nchi, ameona na kushuhudia mambo ambayo yamemfanya akose amani ndani ya moyo wake, hivyo ameamua kukaa pembeni.

“Kwa heshima na unyenyekevu, naomba kukutaarifu kuwa, nimefikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi yangu ya Uongozi wa Umma nikiwa Balozi na Mkuu wa Kituo cha Uwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Havana Cuba, pamoja na uwakilishi wa eneo la Karibe, Amerika ya Kati na nchi rafiki za Colombia, Venezuela na Guyana.
“Uamuzi huu si mwepesi, bali umetokana na tafakari ya kina juu ya mwenendo wa uongozi katika nchi yetu, uzoefu wangu kama mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hatimaye kama Balozi katika vituo vya Lilongwe, Malawi na Havana, Cuba,” ameeleza.
Polepole amemweleza Rais Samia kwamba, alipokea kwa heshima uteuzi na dhamana aliyompa kuwa, mwakilishi wa Tanzania katika ngazi ya kimataifa. Aliamini na anaendelea kuamini lilikuwepo kusudi na kazi muhimu ya kuyashika, kuyasimika, kuyasimamia, kuyaimarisha na kuyaendeleza masilahi mapana ya nchi katika maeneo hayo.
Baada ya kuamua kukaa pembeni, Polepole amesisitiza kwamba, ataendelea kuwa mwanaCCM wa kawaida, mzalendo na raia mwaminifu kwa Taifa na nchi hii.
Ameeleza kuwa, anaamini siku moja nchi hii itaongozwa kwa misingi ya haki, maadili na dhamira njema.
“Ninamwamini Mungu wa mbinguni na ninahamasika na tumaini kuu kwamba, siku moja nchi yetu itaongozwa kwa misingi ya haki, maadili, usimamizi thabiti wa miiko na nidhamu ya uongozi, dhamira njema, siasa safi, uongozi bora na hofu ya Mungu,” ameeleza Polepole.
Alipoulizwa kuhusu barua ya Polepole, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amekiri kuisoma katika mtandao.
“Mwenye kudhibitisha kuwa ni barua halali ama sio ni yeye mwenyewe, lakini mimi na ninyi, tumeisoma katika mtandao na maudhui yake nimeyasoma naamini kuwa, mtapata nafasi ya kujiridhisha kwamba ni ya kweli ama si yakweli,” amesema Makalla.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya CCM, Amos Makalla akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma. Picha na Sharon Sauwa.
“Akisema ni ya kweli basi atakuwa amethibitisha kuwa barua ile ni yake na kabla sijaenda kujibu, nahoji tu uhalali wa kuthibitisha barua ni ya kweli ama si ya kweli,” amesema Makalla alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya CCM jijini Dodoma kuhusu yanayoendelea kwenye mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge na uwakilishi.
Makalla amesema yote ni utashi wake kama ni kweli ameandika yeye, lakini jambo la kumfurahisha ni kuwa amemalizia kwa kusema atabaki kuwa mwanachama mwadilifu wa CCM.
Amesema kama ni kweli, wanamshukuru kwa maoni yake aliyoyatoa lakini bado ni mwanachama wa CCM mwaminifu kati ya wanachama milioni 13.
Alivyoanza na ‘wahuni’
Siyo mara ya kwanza kwa Polepole kuigeukia CCM na Serikali yake, alipokuwa mbunge alianzisha ‘Kampeni ya Kataa Wahuni’ aliyoiendesha kupitia kipindi chake kwenye mitandao ya kijamii, kilichojulikana kama Shule ya Uongozi.
Polepole aliwahi kufafanua kauli yake kuhusu neno ‘wahuni’ akisema alilitumia kuwakilisha watu wanaotanguliza masilahi yao mbele badala ya masilahi mapana ya Taifa.
Alisema kuna watu ambao masilahi ya Taifa wanayaweka kando au mwishoni na wanaopanga hivyo ni ‘wahuni’ na kwamba neno hilo hakuanza nalo yeye. Alisema ‘wahuni’ wanapenda masilahi binafsi kwanza.
Wakati akiendelea na Shule ya Uongozi iliyoonekana kuwa mwiba kwa viongozi wa Serikali, Polepole aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi, kabla ya kuhamishiwa Cuba alikohudumu hadi leo alipotangaza kujiuzulu.
Mbali na nyadhifa hizo, Polepole aliwahi kuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Kabla ya kuzama kwenye siasa, Polepole alikuwa akifanya kazi kwenye Taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) zilizoshughulika na vijana na kupitia midahalo mbalimbali, alionesha uwezo wake wa kuzungumza kwa kujenga hoja kutetea masilahi ya vijana.