Polisi yamshikilia kigogo mwingine wa Chadema

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limesema linamshikilia Mtaalamu wa Rasilimali, Miradi na Uwekezaji wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Leonard Magere kwa tuhuma za jinai.

Taarifa ya Polisi iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi leo Jumapili Julai 13, 2025 imeeleza kuwa Magere alikamatwa jana Jumamosi.

“…Leonard Josephat Magere alikamatwa jana Julai 12, 2025 kutokana na tuhuma za jinai zinazomkabili na anaendelea kushikiliwa kwa mahojiano ili kukamilisha ushahidi ambao ulishakusanywa,” imeeleza taarifa hiyo.

Awali, Chadema kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mambo ya Nje na Diaspora, John Kitoka ilitoa taarifa kwa umma ikisema Magere alikamatiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA), akijiandaa kusafiri kwenda nchini Uingereza.

Chadema ilidai Magere alikuwa anakwenda kushiriki mafunzo maalumu ya kubuni mikakati ya rasilimali yaliyotarajia kufanyika kuanzia leo Jumapili hadi Julai 17, 2025.

Katika tukio lingine, Polisi wanamshikilia Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Brenda Rupia kwa mahojiano.

Brenda alikamatwa jana Jumamosi na uhamiaji kisha kumnyang’anya hati yake ya kusafiria na amekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi.

Taarifa ya Jeshi la Polisi ilieleza kuwa Brenda alikamatwa na maofisa wa uhamiaji akiwa ofisi za uhamiaji katika mpaka wa Namanga alikokuwa anafanya mchakato wa kusafiri kwenda nchini Kenya.

Taarifa ya msemaji wa polisi juu ya tukio hilo ilieleza:“…limemkamata Brenda Rupia Jonas kwa ajili ya mahojiano kutokana na tuhuma zinazomkabili za kutoa taarifa za uongo na za uchochezi. Baada ya mahojiano taratibu nyingine kwa mujibu wa sheria za nchi zitafuata.”

Chadema ilidai Brenda alikuwa anakwenda Kenya kisha asafiri kwenda Munich nchini Ujerumani ambako alitarajiwa kushiriki mafunzo kuhusu demokrasia na uchaguzi.

Related Posts