Serikali yakumbushwa kuwashirikisha wasichana athari mabadiliko ya tabianchi

Dar es Salaam. Serikali imekumbushwa kuhakikisha watoto wa kike wanapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mikakati ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kwani wao ni waathirika wakubwa wa athari za mabadiliko hayo, hasa vijijini.

Wito huo umetolewa leo Julai 13, 2025 jijini Dar es Salaam, katika mkutano wa wadau wa mazingira ulioandaliwa na chama cha Tanzania Girl Guides Association (TGGA), ukilenga kupitia kwa pamoja sera ya mazingira ya Taifa kwa mtazamo wa kijinsia.

Mkutano huo umeongozwa na mtaalamu wa mabadiliko ya tabianchi, Msololo Onditi, ambaye amesisitiza kuwa watoto wa kike si tu waathirika, bali ni sehemu muhimu ya suluhisho.

“Serikali inapaswa kuwaleta watoto wa kike mbele, kwani wao ni waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Kuwatenga kunamaanisha kuikosesha jamii nguvu kubwa ya mabadiliko,” amesema Onditi.

Onditi amebainisha kuwa watoto wa kike wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika jamii kupitia elimu, uhamasishaji na uongozi wa kimazingira. Amehimiza kuwa ushirikishwaji wao haupaswi kuwa wa hiari bali wa lazima katika sera na utekelezaji wa mikakati ya tabianchi.

Valentina Gonza, Msimamizi wa Miradi kutoka TGGA, amesema chama hicho kimeamua kuanzisha mjadala wa kitaifa kufuatia kubainika kwa uwiano mdogo wa ushiriki wa watoto wa kike katika ajenda za mazingira.

“Athari za tabianchi haziangalii jinsia, lakini watoto wa kike ndio wanaoathirika zaidi. Tumeona ni muhimu kuwaita wadau kutoka maeneo mbalimbali ili kutengeneza mkakati wa pamoja wa kuwalinda na kuwawezesha,” amesema Valentina.

Ameendelea kusema kuwa ni wakati muafaka kwa makundi tofauti kushirikiana ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, na pengine kuondoa kabisa madhara hayo.

Naomi Nasorro, mwanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Chuo Kikuu cha Kampala kilichopo Gongolamboto jijini Dar es Salaam, ameeleza namna alivyoguswa na maudhui ya mkutano huo.

“Nimegundua kuwa hata sisi mabinti tuna haki ya kushiriki katika mijadala ya kisera kuhusu mazingira. Elimu niliyoipata leo inanipa ujasiri wa kupaza sauti yangu na kupigania haki za mtoto wa kike na mazingira,” amesema Naomi.

Wadau mbalimbali waliokutana kwenye mkutano huo walisisitiza haja ya kuwekeza zaidi katika elimu ya mazingira kwa watoto wa kike ili kuwapa uelewa wa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, baadhi ya washiriki walionyesha wasiwasi wao kuhusu vikwazo vya kijamii na mila zinazowazuia watoto wa kike, hasa vijijini, kushiriki katika masuala ya kijamii na kisiasa. Kwa mujibu wa Onditi, hali hiyo inaweza kutatuliwa kwa sera shirikishi zinazolenga kuondoa vizingiti vya kijinsia.

Amesema changamoto hizi zinahitaji kushughulikiwa kwa njia maalumu, ikiwemo kuanzisha sera ambazo zitahakikisha watoto wa kike wanapata fursa sawa za kushiriki katika masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Related Posts