Simba yateua watano kamati ya usajili

UONGOZI wa klabu ya Simba umeteua majina matano yatakayounda kamati mpya ya usajili ya timu hiyo ambayo ipo sokoni kusajili nyota watakaoibeba msimu ujao.

Kamati hiyo awali ilikuwa na Crecensius Magori, Mulamu Nghambi, Kassim Dewii na Sued Mkwabi ambao waliteuliwa kusimamia usajili mapema msimu ulioisha.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeiambia Mwanaspoti kuwa uteuzi umefanyika kwa usiri mkubwa na viongozi walioteuliwa watafanya kazi kwa ukaribu na benchi la ufundi kuanzia kwenye usajili.

“Ni kweli wameteuliwa viongozi watano wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed Dewji na kesho watatangazwa tayari kwa kuanza kazi,” kimesema chanzo cha taarifa hizi.

“Majina niliyoyapata hadi sasa ni manne lakini kamati hiyo inaundwa na Mo, Geofrey Nyange Kaburu, Said Tully na Salim Abdallah ‘Try Again’ hayo ndio majina niliyonayo huyo mmoja sijajua ni nami,” kimesema chanzo hicho.

Julai 4 2025, baada ya Simba kushindwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kikao cha viongozi wa klabu hiyo kilipitisha uamuzi wa kuvunja kamati ya usajili kwa kushindwa kutimiza malengo yao.

Kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam chini ya Mo kilitathimini mwenendo mzima wa msimu ulioisha wa Ligi Kuu Bara na kubaini kwamba  ilishindwa kusajili wachezaji wenye viwango.

Related Posts