MSHAMBULIAJI wa Azam FC raia wa Senegal, Alassane Diao amethibitisha hatokuwa sehemu ya kikosi hicho msimu ujao, huku taarifa zikieleza yupo katika mazungumzo ya kujiunga na Etoile du Sahel ya Tunisia iliyoonyesha nia ya kumuhitaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Diao alisema baada ya kukitumikia kikosi hicho kwa misimu miwili, ameamua kutafuta changamoto sehemu nyingine, ingawa timu atakayochezea msimu ujao hawezi kuiweka wazi kwa sasa, kwa sababu mazungumzo yanaendelea.
“Nimekuwa na wakati mzuri Tanzania na nashukuru kuitumikia Azam, kiukweli nimefarijika na ni muda sasa wa kutafuta changamoto mpya, nafikiri baada ya muda sio mrefu mashabiki wangu watajua ni timu gani nitakayoichezea,” alisema Diao.
Kuhusu ofa ya Etoile du Sahel kumuhitaji, Diao alisema ni mapema kuzungumzia hilo kwa sababu zipo nyingi ila hajafanya uamuzi wa mwisho wa sehemu atakayoenda, ingawa Mwanaspoti linatambua APR kutoka Rwanda pia imeonyesha nia ya kumhitaji.
Nyota huyo alijiunga na Azam Julai 4, 2023, akitokea US Goree ya kwao Senegal ambako mkataba wake umeisha Juni 30, 2025, huku kukiwa hakuna tena mazungumzo mapya, kutokana na kutokuwa na misimu mizuri kwa sababu ya majeraha ya mara kwa mara.
Katika misimu miwili aliyoitumikia Azam, mshambuliaji huyo amefunga mabao matatu ya Ligi Kuu, ambapo msimu wa kwanza wa 2023-2024, alifunga mawili, huku huu wa 2024-2025, akifunga moja tu tena alilolifunga mara ya mwisho, Desemba 17, 2024.
Bao hilo alilolifunga, Desemba 17, 2024, alilifunga dakika ya 90, katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-0, dhidi ya Fountain Gate, kwenye Uwanja wa Azam Complex, likiwa ni la pili baada ya Gibril Sillah kufunga la kwanza dakika ya 30.
Nyota huyo alisajiliwa na aliyekuwa kocha wa Azam Msenegal, Youssouph Dabo aliyejiunga na timu hiyo, Mei 1, 2023, baada ya kuachana na Klabu ya ASC Jaraaf de Dakar, ingawa aliondoka kikosini humo, Septemba 3, 2024.