Dar es Salaam. Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), kinatarajiwa kufanya mkutano wake mkuu utakao toa fursa kwa wanachama kujadili mambo mbalimbali yanayoikabili sekta hiyo na kuja na maazimio ya pamoja.
Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kupewa msukumo zaidi katika mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Julai17, 2025, Ukumbi wa Ubungo Plaza Dar es Salaam ni kamatakamata ya mabasi na kufungia madereva inayofanywa na Jeshi la Polisi, na suala la tiketi mtandao ambalo bado halijakaa sawa kwa upande wao.
Akizungumza na Mwananchi, Msemaji wa Taboa, Mustapha Mwalongo amesema mkutano huo ni wa kikatiba na kutoa mrejesho wa mpango kazi kwa waliyofanya na kuwaeleza wanachama wamefikia wapi na yaliyoshindikana.
“Changamoto ambazo zinatusumbua zitajadiliwa kwa pamoja na kupata maazimio ya uelekeo mmoja. Muda wote tulikuwa tunafanya kazi kama uongozi na kamati tendaji lakini kupitia mkutano huu utatoa fursa wanachama wote kutoa maoni yao na kupendekeza cha kufanya,” amesema.
Mwalongo amesema kikawaida mikutano yao huwa wanafanya mwishoni mwa mwaka lakini kwa kuwa Tanzania unafanyika Uchaguzi Mkuu mwaka huu, wameamua kuufanya mapema.
“Baada ya mkutano huu tutaandaa mkutano mkuu wa dharura utakaojadili na kuitisha tarehe ya mkutano mkuu wa uchaguzi kupata viongozi wapya wa chama hicho.”
“Jumla tutakuwa na mikutano mitatu mwaka huu wa kwanza wa kesho kutwa, halafu kuna utakaofuata mkutano mkuu wa dharura tutakaoufanya mwezi ujao utakaojenga ajenda za mkutano mkuu wa Septemba,” amesema.
Amesema katika mkutano unaotarajiwa kufanyika mwezi huu hajui wajumbe watapendekeza hoja zipi, ingawa matarajio yao mambo yenye changamoto yatapata uelekeo mpya.
Akizungumza zaidi kuhusu mkutano huo Katibu wa Taboa, Priscus John ametaja mambo yanayotarajiwa kujadiliwa ni kamatakamata ya mabasi barabarani na kufungia madereva inayoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani, kwa lengo la kudhibiti wimbi la ajali zinazosababisha vifo na ulemavu.
Amesema hali hiyo imekuwa ikiwapa shida wao kama wamiliki kwanza madereva wao wanaofungiwa wakati ni wazoefu na wanalazimika kuajiri wengine wapya ambao nao wanaenda kusababisha ajali.
“Imefikia wakati tunashindwa la kufanya tunawekaje, na wamiliki wa mabasi hatutaki kutangaza mgogoro na Polisi, mtu anapigwa faini kwa kulipita gari linalotembea spidi 20 lakini anakamatwa anapigwa faini na anafungiwa,” amesema.
Amesema dereva sio bidhaa au kifaa kikiisha unaenda kununua, unakuta gari yako inatoka Moshi inafika Msata mkoani Pwani unapigiwa simu imekamatwa ina makosa na imepigwa faini na dereva wako amefungiwa inakuwa changamoto.
“Msata unapata wapi dereva, halafu fungiafungia hawa ni binadamu kuna makosa wanafanya mfano kuipitia gari mbele yako inayotembea spidi 20, unamfungia mtu leseni kweli, mtu hataki kupisha kweli hasa malori yana mchezo huo.”
“Ni kweli kuna mistari, sehemu hatarishi tutajadili hilo, lakini kuna suala la tiketi mtandao bado halijafanyiwa vizuri tunataka kwenda kutolea maazimio,” amesema.