Wajasiriamali walia kukosekana kwa vifungashio, ZEEA yaeleza ufumbuzi

Unguja. Wajasiriamali kisiwani Unguja wamesema ingawa wamefaidika kwa kupata punguzo kwenye alama za ubora wa bidhaa zao na fursa ya kujitangaza, bado wanakumbwa na changamoto ya ukosefu wa vifungashio vya bidhaa.

Wamesema hali hiyo inawalazimu kuagiza vifungashio kutoka nje ya nchi, jambo linaloongeza gharama na kuwa mzigo kwao.

Kauli hiyo wameitoa leo Jumapili Julai 13, 2025, walipokuwa wakizungumza na Mwananchi Digital katika eneo lao la biashara huko Paje, Mkoa wa Kusini Unguja.

Asya Waziri Mwishame, amesema changamoto ya kuagiza vifungashio inasababisha bidhaa zao kuuzwa kwa bei ya juu na kushindwa kuingia kwenye soko la kimataifa kwa sababu si kila mjasiriamali anayeweza kumudu gharama hizo.

“Tunaomba ZEEA (Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar), itafute wawekezaji ili tuwe na kiwanda cha vifungashio. Bidhaa zetu zinashindwa kuingia sokoni kimataifa na wakati mwingine zinabadilika rangi kwa kukosa sehemu bora ya kuhifadhia, ikiwamo sabuni, jambo linalotukosesha wateja,” amesema Asya.

Kwa upande wake, Tatu Suleiman Abdulla ameiomba ZEEA kutoa mafunzo kwa wajasiriamali kuhusu kuongeza thamani ya bidhaa na mbinu za upatikanaji wa masoko.

Baadhi ya vifungashio ambavyo wajasiriamali wanaagiza kutoka nje ya Tanzania.



Amesisitiza pia umuhimu wa kuhakikisha bidhaa zinakuwa na ubora unaowawezesha kushindana sokoni.

Naye, Amina Juma Amour ameiomba ZEEA kuwasaidia kupata soko la nje kwa sababu soko la ndani pekee halitoshi.

Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhan Mohamed amekiri kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa vifungashio na kusema tatizo hilo linakwamisha bidhaa za wajasiriamali kuingia katika soko la kimataifa.

Amesema ZEEA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (Zipa) inatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza kisiwani humo ili kujenga kiwanda cha vifungashio na kuondoa changamoto hiyo.

“Changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali kisiwani hapa ni ukosefu wa vifungashio. ZEEA tutalifanyia kazi kwa kushirikiana na wawekezaji mbalimbali ili tuwe na kiwanda cha vifungashio,” amesema Juma.

Mkurugenzi huyo amewapongeza wajasiriamali kwa kueleza changamoto zao na kuahidi kuwa taasisi yake itaendelea kushirikiana nao ili kuyapatia suluhu.

Related Posts