Mtwara. Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka wananchi wa Mtwara na Lindi kuchagua upinzani ili kuwaletea mabadiliko kama walivyofanya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Amesema katika uchaguzi wa mwaka 2015, majimbo ya Mtwara Mjini na Tandahimba, Kilwa Kusini na Kaskazini, Ndanda yalinyakuliwa na upinzani, hivyo ni wakati mwafaka kwa wananchi wa Lindi na Mtwara kuirejesha heshima kwa kuichagua ACT Wazalendo.
Ameeleza hayo jana Jumamosi Julai 12, 2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mtaa wa Sinani katika Jimbo la Mtwara Mjini katika mwendelezo wa ziara ya operesheni majimaji linda kura yako, yenye lengo la kuwaamsha Watanzania kujua thamani ya kura zao.
Kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara, Zitto akiambatana na viongozi waandamizi wa Mtwara walifanya ziara ya ufunguzi wa matawi matatu likiwemo Magomeni ikiwa ni sehemu ya kukieneza chama mkoani humo.
Katika maelezo yake, Zitto amesema: “Mnapaswa kukitaa CCM, na kuchagua chama kingine mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 2015 majimbo ya Mtwara Mjini na Vijijini na Tandahimba.
“Sio dhambi kuikataa CCM, ukiikataa CCM ni kama vile umekikataa chama kingine na unachagua chama kingine kama ilivyokuwa 2015, sasa tufanye mwaka 2025.”
“Hata mkikipa kura namna gani nyie hamtakuwa kipaumbele, angalieni utajiri mlionao na hali zenu za maisha na mkoa kwa ujumla. Kiwango cha fedha kinachoingia ndani ya Lindi na Mtwara kutokana na korosho ni kikubwa sana lakini maendeleo yanasuasua,”amedai Zitto.
Zitto amedai katika mikoa ya Lindi na Mtwara kumekuwa na uwekezaji mkubwa unaofanyika lakini bado wananchi wa mikoa hiyo wanaishi pasipo kupata ajira za uhakika.
“CCM hawawataki na nyinyi hamna sababu ya kuikumbatia, ishara ya kuonyesha kuikataa ni katika sanduku la kura. Tunajua mwaka 2019, 2020 na 2024 tumeona yaliyotokea lakini msikate tamaa,” amedai.
Amesema Mungu amewaumba binadamu namna ya kutafakari ili kuikabili CCM, hivyo kulingana na mazingira yalivyo chama tawala hakipaswi kukimbiwa katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
“Twendeni tukapige kura na kuishinda CCM kwenye sanduku la kura ili tufanye mabadiliko ya mikoa ya Lindi na Mtwara. Kusini ni tajiri sana, lakini utajiri wenu bado hautumiki, sasa ACT Wazalendo inataka kuutumia utajiri wenu ili mnufaike pamoja na Taifa kwa ujumla,” amesema Zitto.
Amesema wananchi wa Mtwara na Lindi wakiichagua ACT Wazalendo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba kuanzia kwenye ubunge na udiwani watapigania masilahi yao kwa sababu chama hicho kina sera bora ya kuifanya mikoa hiyo kuwa kitovu cha huduma.
Awali, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, mkoani humo, Marijani Ndandavale amesema hivi sasa mkoa huo umeanza kuitika kuhusu chama hicho, kumekuwa na mapokeo mazuri ya watu kukipenda chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar.
Ndandavale amesema ana imani wananchi wa Mtwara watazinduka kwa sababu wanapenda mabadiliko na thamani ya mkoa huo ikiwemo uwepo wa bandari, gesi pamoja na ardhi nzuri ya kilimo cha korosho.
“Ila kwa sasa bado wananchi hawajazinduka kutokana na maisha magumu yaliyosababishwa uwakilishi mbovu wa watu wanaowachagua katika uchaguzi mkuu,” amedai Ndandavale.
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Kiza Mayeye amesema wakati anatoka CUF na kujiunga na chama hicho, alionekana msaliti, lakini hivi sasa anaonekana yupo sahihi huku akimkaribisha Nachuma kwa mara nyingine.
“Tumeanzia kule Kigoma, kila tulipopita watu wanalalamika maisha magumu, nafarijika kuona kina mama naomba msimame imara na kusema basi. Ni wakati sasa wa kuipa kura ACT Wazalendo tukaleta mabadiliko katika huduma za afya,” amesema.
“Simameni imara tumpeleke Nachuma akafanye mabadiliko ya kuzisemea bungeni changamoto zinazowakabili,” amesema Mayeye ambaye ni waziri kivuli wa fedha wa ACT Wazalendo.
Kada mpya wa ACT Wazalendo na mtia nia wa Jimbo la Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma amewashukuru wananchi wa jimbo kwa kukubali kubadili njia ya mapambano.
“Leo wengi watakuwa wanashangaa Maftaha alikuwa CUF lakini amejiunga na ACT Wazalendo… naombeni ushirikiano wenu kama ilivyojukwa mwaka 2015,” amesema Nachuma ambaye amewahi kuwa makamu mwenyekiti wa CUF ( bara).