Bwege apata janga jingine, asisitiza haki uchaguzi mkuu

Lindi. Imekuwa bahati mbaya kwa mbunge wa zamani wa Kilwa Kusini, mkoani hapa, Seleman Bungara maarufu ‘bwege’ kutokana kuvunjika mguu ikiwa ni wa pili baada ya awali kukatwa kwa sababu ya maradhi.

Bwege aliyekuwa akisifika kuwasilisha hoja zake bungeni kwa njia vichekesho na utani amevunjika mguu jana Jumapili usiku nyumbani Kilwa Kivinje wakati akijiandaa kuingia chumbani.

Mwanasiasa huyo aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF, kabla ya kuhamia ACT- Wazalendo, alifika Kilwa kwa lengo la kuhudhuria mkutano wa ndani na hadhara uliongozwa na kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe aliyembatana na viongozi wengine waandamizi.


Zitto yupo ukingoni kuhitimisha ziara ya siku 15 ya Operesheni Majimaji Oktoba Linda Kura, yenye lengo la kuwaamsha Watanzania kupiga kura, kuzilinda na kutambua thamani ya kura hizo.

Ni bahati mbaya kwa Bwege kuwa katika mfululizo wa kuugua maradhi mbalimbali ikiwamo kisukari kilichosababisha akatwe mguu wa kushoto huku figo zikifeli.

Kutokana na changamoto aliyoipata jana ndoto yake ya kuhudhuria mikutano hiyo zimekufa kwa sababu mguu aliovunjika ndio ulikuwa tegemezi pekee wa yeye kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“Sitoweza kuhudhuria tena mikutano hii, naitaji kupumzika kidogo, maana baada ya kwenda hospitali na kupigwa X – Ray imebainika mguu umevunjika na natakiwa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi,” amesema Bwege akizungumza na wanahabari leo Jumatatu Julai 14,2025 nyumbani kwake Kilwa Kivinje.

Katika maelezo yake, Bwege amesema kutokana kusumbuliwa na maradhi ya figo anayotakiwa kwenda kliniki kila baada ya wiki tatu, amebainisha kuwa amefika Kilwa kwa lengo la kuhamasisha shughuli za chama.

Ziara ya Operesheni Majimaji

Kuhusu ziara ya Operesheni Majimaji Oktoba Linda Kura, Bwege aliyewahi kuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya ACT-Wazalendo, amesema hotuba za viongozi hao zinawavutia watu wengi wanaohamasika kujiunga na chama hicho.


“Naamini kwa kanda ya kusini ACT- Wazalendo ikijipanga na kufanya kampeni, itapata majimbo yasiyopungua sita au saba, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba baadaye,”

“Nimefurahishwa na mapokezi ya Namtumbo, Tunduru, Mtwara, Lindi na leo hapa Kilwa, nimefurahi sana ndio maana nimefunga safari kuja lakini ndio hivyo si riziki tena,”amesema Bwege.

Bwege amesema  ziara ya Operesheni Majimaji Oktoba Linda Kura,  ‘imetiki kusini’ kutokana na mapokezi makubwa walioyapata viongozi waliopo katika msafara huo, akisema majimaji asili yake kusini.

“Naomba wasichoke viongozi wangu wasichoke, naomba watu wa kusini tukiunge mkono ACT- Wazalendo ndicho suluhisho la matatizo yetu yanayotukabilia hasa umaskini. Ikiwezekana chama chetu kimoja tu ACT kama zamani ilivyokuwa CUF tusigawanyike ili tuishinde CCM,” amesema Bwege.

Katika mazungumzo hayo, Bwege alilaani kile kinachodaiwa kuwa Zitto  alishikiliwa na polisi kwa madai ya kutoa taarifa za vitisho kuhusu Jeshi la Polisi katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Baraza la Eid wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma Julai 10,2025.


“Binafsi sioni kosa la Zitto pale, maana ametoa tahadhari kwamba yaliyojitokeza mwaka jana au miaka iliyopita sisi hatutakubali au yasijirudie tena. Naiomba Serikali ikae na vyama vya siasa vyote na kukubaliana mambo ya msingi watakayoyasimamia,” amesema Bwege.

Katika hatua nyingine, Bwege amemwagia sifa kada mpya wa ACT- Wazalendo, Maftaha Nachuma aliyejiunga na chama  hivi karibuni akitokea CUF, awali walikuwa wote pamoja na mbunge huyo wa zamani wa Kilwa Kusini.

” Nimefurahi ujio wake ameizindua Mtwara Mjini mara moja kuingia ACT- Wazalendo, niliongea Maftaha tulipanga kutembea mkoa wote, lakini ni vile naumwa tu ila namshukuru kwa ujio wake,” amesema Bwege.

Mbali na hilo, Bwege ametoa wito wa Tume Huru ya Uchaguzi ( INEC), kutenda haki katika uchaguzi wa Oktoba kwa hakikisha mchakato huo unakuwa wa weledi na anayeshinda atangazwe ndio demokrasia inavyotaka.

” ACT- Wazalendo imeamua kushiriki uchaguzi huu na imeshasaini kanuni za maadili, tunaomba haki itendeke kwa vyama vyote naomba sana Rais Samia Suluhu Hassan asimamie hili,”

“Katika mapambano kila mtu ana njia yake, ACT- Wazalendo tumeamua kushiriki, wale wengine wana msimamo wao, lakini lengo letu ni kuiondoa CCM madarakani, msisitizo wangu haki itendeke,” amesisitiza  Bwege.

Related Posts