Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefafanua sababu za kumkataa Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama, inayokikabili.
Chama hicho kimeibua sababu mbili, ya kwanza kikimtuhumu Jaji Mwanga kuwa na upendeleo kwa upande kinzani na ya pili kuwa na mgongano wa masilahi.
Kwa upande mwingine wakili wa upande kinzani, wamepinga sababu hizo wakidai hazifai kumtaka jaji ajiondoe kwenye kesi bali zinapasa kuwa sababu za rufaa.
Hata hivyo, hatima ya Jaji Mwanga kujitoa au kukataa badala yake kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo itajulikana Julai 28, 2025 wakati atakapotoa uamuzi kuhusiana na sababu za maombi hayo ya kumtaka ajitoe.

Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Taifa, Zanzibar; Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutokea Zanzibar.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa (mlakamikiwa wa kwanza) na Katibu Mkuu wa chama hicho (mdaiwa wa pili).
Juni 10, 2025, Mahakama hiyo ilitoa amri ya zuio dhidi ya wadaiwa kufanya shughuli za kisiasa na amri ya kuwazuia wao wadaiwa na watu wengine wanaofanya kazi kwa maelekezo au kwa niaba yao kutumia mali za chama hicho mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo kufuatia shauri la maombi ya zuio hilo yaliyofunguliwa na wadai katika kesi hiyo, baada ya Mahakama kutupilia mbali mapingamizi ya wadaiwa dhidi ya kesi ya msingi na dhidi ya shauri la maombi ya zuio.

Kutokana na uamuzi na amri hizo, Juni 23, 2025 walalamikiwa walimwandikia barua Jaji Mwanga wakimtaka ajitoe kusikiliza kesi hiyo kwa madai hawana imani naye kuwa atawatendea haki.
Maombi yao hayo ya kumtaka ajitoe katika kesi hiyo yamesikilizwa leo Julai 14, 2025, huku waombaji wakiwasilisha na kufafanua sababu zao mbele ya Jaji.
Sababu hizo zimewasilishwa na kufafanuliwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kabla ya mawakili wao kufafanua hoja hizo katika misingi ya kisheria.
Akiwasilisha na kufafanua sababu hizo, katika sababu ya kwanza, Mnyika amejenga hoja katika mwenendo wa kesi hiyo wa Juni 10 huku akirejea kusimulia yaliyojiri.
Mnyika amesema siku hiyo wakili Jebra Kambole aliomba Mahakama iahirishe mwenendo wa kesi hiyo akieleza kuwa, wakili mwenzake Hekima Mwasipu hayupo kwa kuwa, amepata msiba na yeye anajiandaa kusafiri kwenda kwenye msiba huo Mbeya.
Hata hivyo, Jaji Mwanga alikataa kuahirisha shauri hilo kutokana na mwenendo wa Jaji, wakili Kambole aliamua kumuomba Jaji aahirishe ili wateja wake wapate wakili mwingine, lakini Jaji Mwanga alikataa.
Badala yake aliendelea kusikiliza maombi ya zuio la muda na hatimaye kutoa uamuzi wa upande mmoja bila walalamikiwa kuwepo.
Alitoa amri ya kuwazuia walalamikiwa (Bodi na Katibu Mkuu) kufanya shughuli za kisiasa mpaka kesi ya msingi itakapoisha.
Pia, alitoa amri ya kuwazuia walalamikiwa, wakala wao na watu wengine wowote wanaofanya kazi kwa maelezo yao au kwa niaba yao kutokutumia mali za chama hicho mpaka kesi ya msingi iishe.
“Kwa maana hiyo sisi walalamikiwa ulitunyima haki ya uwakilishi unaostahili, hayo wakati yanatokea hatukuwepo mahakamani pengine tungeweza kujiwakilisha,”amesema Mnyika.

Amesema kutokuwapa nafasi ya kusikilizwa Jaji Mwanga alitenda kosa la kimaadili.
Amedai amri za zuio alizozitoa Jaji Mwanga, zina madhara kwao kama chama ambacho kazi yao ni kufanya siasa lakini pia zinalenga kudhuru mali chao.
Amedai lengo la zuio ni kulinda hali iliyopo ya kitu au mali ili isiharibiwe, lakini amri alizozitoa zinahatarisha mali zote za chama.
Mnyika amefafanua baada ya kuwazuia wao, viongozi na wanachama hakusema zikabidhiwe kwa mamlaka yoyote ya kuzilinda na kwamba hivyo zinaweza kuchukuliwa na mtu mwingine yeyote yule asiye mfanyakazi au mwanachama wa Chadema.
Amesema wakati anatoa amri hiyo walikuwa ziarani mikoani hivyo ilimaanisha kuwa viongozi na wafanyakazi wakiwamo madereva watelemke kwenye magari hayo na hakusema waziweke kwa nani, vilevile majengo hayatakiwi kuwa chini ya wadhamini, viongozi na wanachama.
“Kwa amri yako hiyo wafanyakazi wote wa Chadema kimsingi wamesimamishwa, hawatakiwi kwenda ofisini na kufanya kazi za chama kwani fedha zote wamezuiwa kuzitumia,” amedai Mnyika.
“Kuzuia chama cha siasa wakati wa mwaka wa uchaguzi wakati chama hicho kinafanya kampeni ya kupigania mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi ni kutuhujumu.”
Katika sababu ya pili, Mnyika amedai Jaji Mwanga ana mgongano wa masilahi.
Amefafanua hiyo inatokana na historia ya utumishi wake kwamba amekuwa mtumishi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) (sasa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ambazo wao wana mgogoro nazo.
“Mwisho, sisi tumekufungulia malalamiko katika Kamati ya Maadili ya Majaji kupitia kwa Katibu wa Tume ya Maadili ya Majaji, kwa msingi wa malalamiko hayo kwenye tume tunaona una mgogoro na sisi ni vema ujiondoe kusikiliza kesi hii.”
Hata hivyo, Wakili Mwasipu amefafanua hoja hizo katika misingi ya kisheria huku akirejea kesi mbalimbali zilizowahi kuamuriwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa kuhusu sababu za Jaji kujiondoa katika kesi.
Amesema malalamiko ya upendeleo ni moja ya sababu za kisheria Jaji kujiondoa na kwamba, kwa mwenendo wa Juni 10, 2025 haikuwa haki kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa dhidi yake katika Tume ya Maadili ya Majaji na historia ya utumishi wake, ni vema ajiondoe.
Mawakili wa walalamikaji, Shabani Marijani, Gido Simfukwe na Alvan Fidelis wamesema waombaji hawajaeleza sababu za msingi na kwamba sababu nyingine walizozitoa zilipaswa kuwa sababu za rufaa au mapitio.
Wakili Marijani amesema siku hiyo walalamikiwa hao hawakuwepo mahakamani, hivyo mambo mengi waliyoyaeleza ni ya kusimuliwa ambayo kisheria ni uzushi tu.
Amesema hoja ya kuahirisha kesi ni utashi wa Mahakama na hakuna mahali ambako walalamikaji na mawakili wao wameeleza kuwa katika kukataa kuahirisha kesi hiyo ni wapi Jaji Mwanga alipokiuka sheria za uendeshaji kesi za madai.
Kuhusu suala la wakili Kambole, amesema alifika mahakamani lakini wajibu maombi hawakufika mahakamani na hakukuwa na sababu ya msingi kwa nini hawakufika mahakamani iliyotolewa.
“Hivyo Mahakama iliamua kusikiliza pingamizi la awali na kutoa uamuzi ambao haukumfurahisha Kambole ndipo suala la kujitoa kwenye kesi likaibuka,” amesema wakili Marijani.
Jaji Mwanga baada ya kusikiliza hoja hizo ameahirisha kesi hiyo mpaka Julai 28, 2025 atakapotoa uamuzi wa kujiondoa au la.