Moshi. Wakati mfanyabiashara maarufu mjini Moshi na Dodoma, Ronald (35) Malisa akitarajiwa kuzikwa kesho, daktari bingwa wa watoto wa Hospitali Teule ya Kibosho, Magreth Swai (30) naye anadaiwa kujiua kwa kujinyonga.
Daktari huyo ambaye ni mkazi wa Longuo, wilayani hapa anadaiwa kujiua Julai 10, 2025 kwa kujinyonga kwa kutumia waya wa antena alioufunga kwenye nondo ya mlango wa chumbani kwake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema chanzo ni msongo wa mawazo uliotokana na afya ya akili.
“Mnamo Julai 10, 2025 majira ya saa 3 usiku huko Longuo, Wilaya ya Moshi, Magreth Swai ambaye ni daktari amejiua kwa kutumia waya wa antena alioufunga kwenye nondo ya mlango wa chumbani katika nyumba anayoishi,” amesema Kamanda Maigwa.
Kamanda Maigwa amesema chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo uliotokana na tatizo la afya ya akili.
Akizungumzia kuzikwa kwa mfanyabiashara huyo, mdogo wa marehemu, Lucy Malisa amesema kaka yake atazikwa kesho nyumbani kwake eneo Msufuni, Msaranga.
“Tunamzika kesho hapa nyumbani kwake, Msufuni, ratiba itaanza asubuhi, ambapo baada ya kuchukua mwili hospitali taratibu nyingine zitaendelea,” amesema Lucy.
Tukio la kujiua kwa mwanamume huyo lilitokea Julai 10, 2025 huku chanzo cha tukio hilo ikidaiwa ni msongo wa mawazo uliotokana na kuugua afya ya akili kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda Maigwa Julai 11, 2025 mfanyabiashara huyo inadaiwa sio tukio la kwanza la kutaka kujiua na kwamba kwa mara kadhaa alifanya jaribio la kutaka kunywa sumu na alikuwa akiokolewa na familia.
“Mnamo saa 12:30 asubuhi Julai 10, 2025 huko Msaranga, mfanyabiashara mkazi wa Dodoma na Msaranga aligundulika kufariki kwa kujinyonga kwenye dirisha la choo kilichopo chumbani kwake kwa kutumia shuka,” amesema Kamanda Maigwa.